Kesi ya mauaji ya kukusudia ya
mfanyabiashara Erasto Msuya, imefikia ukingoni huku upande wa mashtaka
ukiegemea mashahidi 32 na vielelezo 26 kujenga msingi wa kesi yao
Wakati upande wa mashtaka ukiishia mashahidi
32 kati ya 50 waliotarajia kuwaita, utetezi kwa upande wao uliita mashahidi
nane na vielelezo vinne kupangua ushahidi wa mashitaka
Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi
kadhaa jijini Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi na bunduki ya kivita ya Sub
Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai
Katika eneo la tukio, kuliokotwa maganda ya
risasi za SMG 22 huku gari ya marehemu aina ya Range Rover T800 CKF, bastola
zake na simu zake mbili zikikutwa eneo la tukio
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi,
chini ya Jaji Salma Maghimbi aliyesikiliza kesi hiyo, ilipokea vielelezo kadhaa
vya kesi hiyo ikiwamo bunduki ya SMG na maganda 25 ya risasi
Pia, ilipokea pikipiki mbili, moja aina King
Lion T751 CKB na Toyo 316 CLG zinazodaiwa na mashahidi wa upande wa mashtaka,
kuwa zilitumika kusafirisha wauaji
Mbali na vielelezo hivyo, Mahakama ilipokea
vielelezo vya nyaraka ambavyo ni maelezo ya onyo ya kukiri kosa ya washtakiwa
watatu na maelezo ya ungamo yaliyotolewa kwa mlinzi wa amani
Maelezo hayo ya onyo ni ya mshtakiwa wa
kwanza, Sharifu Mohamed, mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu, mshtakiwa wa saba,
Ally Majeshi na maelezo ya ungamo ni ya mshtakiwa Karim Kihundwa
Pia, Mahakama ilipokea maelezo ya mashahidi
watano wa upande wa mashtaka na kuyasoma mahakamani baada ya jitihada za upande
wa mashtaka kuwapata kugonga mwamba
Mtiririko wa tukio hilo lililovuta hisia za
wananchi wengi katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara na linaloendelea
kuvuta hisia hizo kwa sasa ulikuwa kama ifuatavyo
Agosti 7, 2013
Mfanyabiashara wa tajiri Mererani, Arusha na
Moshi, bilionea Erasto Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi sehemu mbalimbali za
mwili wake katika eneo la Mjohoroni wilayani Hai
Agosti 11, 2013
Polisi ilitangaza kukamatwa kwa washukiwa
muhimu wakihusishwa katika mtandao wa wahalifu waliofanya mauaji hayo
Agosti 21, 2013
Watuhumiwa watatu, Sharifu Mohamed, Shaibu
Jumanne na Mussa Mangu walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kujibu
shtaka la kumuua kwa makusudi bilionea Msuya
Septemba 16, 2013
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro wakati
huo, Robert Boaz alitangaza kukamatwa kwa watuhumiwa wanne zaidi kuhusiana na
mauaji ya bilionea Msuya
Watuhumiwa hao ni mfanyabiashara tajiri wa
Mirerani na Arusha, Joseph Mwakipesile au Chussa, Sadick Mohamed, Karim
Kihundwa na Jalila Said
Septemba 18, 2013
Mfanyabiashara Mwakipesile au Chussa,
Sadick, Karim na Jalila walifikishwa mahakamani kujibu shtaka la kumuua kwa
makusudi bilionea Msuya
Aprili 16, 2014
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP),
alimfutia mashitaka mfanyabiashara Mwakipesile au Chussa akitumia kifungu Na 91
cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya Jinai (CPA) ya 2002
Juni 10, 2014
Upande wa mashtaka ulifanya mchakato wa
kuwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi 50 wa kesi hiyo na kutaja vielelezo
vitakavyotumika wakati kesi hiyo
Februari 10, 2015
Kwa mara ya kwanza washtakiwa walisomewa
shtaka la mauaji ya kukusudia mbele ya Jaji Amaisario Munisi na wakakana kumuua
Msuya
Oktoba 5, 2015
Kesi ya mauaji ya kukusudia ya bilionea
Msuya ilianza rasmi kusikilizwa na Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Arusha aliyeteuliwa kusikiliza kesi hiyo
Ushahidi wa upande wa mashtaka
Ushahidi wa mashahidi wa mashtaka, ulidai
kuwa njama za kumuua Msuya zilianza Julai 2013; watuhumiwa waliofanya mauaji
hayo waliahidiwa kulipwa Sh17 milioni kila mmoja
Ilidaiwa kortini kuwa katika kupanga mauaji
hayo, simu mpya tano na laini tano zilisajiliwa kwa majina ya kimasai,
kununuliwa kwa pikipiki mbili na kununuliwa kwa bunduki aina ya SMG
Katika ushahidi huo, inadaiwa mshtakiwa wa
saba, Ally Mussa Majeshi, ndiye aliyemvuta marehemu hadi eneo la tukio,
akijifanya yeye na Karim walitaka kumuuzia madini ya Tanzanite
Kulingana na maelezo ya ungamo ya mshtakiwa
Karim na maelezo ya onyo ya kukiri kosa ya mshtakiwa wa saba, Majeshi, Karim
ndiye anayedaiwa kumfyatulia risasi marehemu
Katika ushahidi wake, Dk Paul Chaote
aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Msuya, alidai kuwa ulikuwa na majeraha 26 ya
risasi yaliyosababisha mfumo wa damu na upumuaji kusimama
Dk Chaote alidai kwa kuutazama kwa nje,
mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha madogo 13 na majeraha makubwa 13
yaliyosababishwa na risasi zilizoingia na kutokea upande wa pili
Alidai baada ya kuupasua mwili wa marehemu,
walikuta utumbo mwembamba umekatika huku risasi hizo zikiharibu figo, mishipa
ya damu na bandama lilikuwa limepasuliwa kabisa
Dk Chaote alidai mapafu yote mawili
yaliharibiwa vibaya kwa risasi huku mishipa ya damu inayoingia kwenye mapafu,
figo na bandama nayo ikiwa imechakazwa kwa risasi
Katika ushahidi wao, mashahidi wote
waliegemea katika ushahidi wa mazingira ambapo maofisa wa polisi walieleza
namna washtakiwa walivyoshiriki tukio hilo na namna walivyowakamata
Mshtakiwa wanne aachiwa huru
Mei 14, 2018 Jaji Maghimbi alisema baada ya
kupitia ushahidi wa 32 wa mashtaka na vielelezo 26, amemuona mshtakiwa wa nne,
Jalila hana kesi ya kujibu
Alisema wakati washtakiwa wanafunguliwa
mashtaka mwaka 2013, walikuwapo nane, lakini kuna mshtakiwa mmoja ambaye hata
hivyo hakumtaja kwa jina aliachwa njiani
Mfanyabiashara Mwakipesile alikuwa miongoni
mwa washtakiwa lakini mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa kutumia mamlakaka yake,
alimfutia shtaka hilo Aprili 17,2014
“Suala la ni kwanini aliachiwa njiani hilo
ni suala la DPP. Kwa sasa hivi Mahakama inaona ushahidi unaonyesha washtakiwa
sita mliobaki mna kesi ya kujibu na mtapaswa kujitetea,”alisema Jaji
Utetezi wa washtakiwa ulivyokuwa
Katika utetezi wao, washtakiwa wote
waliegemea ushahidi wa kutokuwapo eneo la tukio (alibi), wakidai kuliteswa na
maofisa wa polisi wakiri kosa hilo na kuweka saini katika maelezo ya onyo
Mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohammed alidai
siku ya tukio alikuwa katika machimbo ya madini ya dhahabu huko Londoni, Ikungi
mkoani Singida na alirejea Arusha Agosti 11,2013
Mshtakiwa wa pili, Shaibu Jumanne alidai
siku ya mauaji,hakuwapo Arusha wala Kilimanjaro,alikuwa shambani Babati
akivuna, kuanzia Julai 13 hadi Agosti 7,2013
Mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu, alidai siku
ya tukio alikuwa Singida akimuuguza baba yake na aliondoka Arusha Agosti 1,2013
kwa basi la Mohamed Classic na kurudi Arusha Agosti 7,2013
Mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa alidai
siku ya tukio alikuwa shambani kwake huko West Kilimanjaro akivuna karoti na
alirejea nyumbani Bomang’ombe Agosti 10,2013
Mshtakiwa wa sita, Sadik Jabir, alidai siku
ya tukio alikuwa Jijini Dar es Salaam na baadaye alikwenda Kaliua Tabora na
kukamatwa na polisi Septemba 13, 2013
Mshtakiwa wa saba, Ally Majeshi alidai siku
ya tukio alikuwa Magugu huko Babati akiwa katika mapumziko ya Fungate, baada ya
kufunga ndoa Agosti 6, 2013 na Mwanaisha Juma
Majumuisho ya mwisho Mei 24, 2018
Upande wa utetezi ulifunga kesi yao Ijumaa
na uliiomba Mahakama chini ya Jaji Maghimbi, kufanya majumuisho ya mwisho huku
upande wa mashtaka ukasema nao utafanya hivyo
Jaji Maghimbi alikubali maombi hayo na
kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 24 mwaka huu na kwamba mawakili wa pande zote
mbili watawasilisha majumuisho ya mwisho ya ushahidi wa pande zote.
Mwanzo mwisho kesi ya mauaji ya Bilionea Msuya
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 20, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 20, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment