Waliomteka na kumdhalilisha Mwandishi wa habari akiwa Utupu ,Mikononi Mwa Polisi


Jeshi la polisi mkoani Arusha limewashikilia watu wanne akiwemo ofisa itifaki kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha,Swalehe Mwindadi kwa tuhuma za kumteka na kisha kumpiga mwandishi wa habari wa kujitegemea mkoani Arusha,Lucas Myovela.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mapema leo,Mey 15 mwaka huu,kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha(RPC),Charles Mkumbo amesema kwamba tayari jeshi lake linawashikilia watuhumiwa hao ambao walikamatwa katika nyakati tofauti jijini hapa.

Kamanda Mkumbo alisema kwamba watuhumiwa hao walikamatwa juzi usiku na wameachiwa jana majira ya saa 3 ;00 usiku kwa dhamana na sasa wanaandaa taratibu za kuwafikisha mahakamani.

Hatahivyo,alisema kwamba mbali na kuwashikilia watuhumiwa hao pia jeshi hilo linashikilia simu ya mkononi ya ya mmoja wa watuhumiwa  kielelezo kilichotumika katika  katika tukio hilo.

Wakati huo huo mwandishi aliyejeruhiwa Myovela amehojiwa na gazeti hili na kusema kwamba hali yake sio nzuri kwa sasa na bado anaendelea kupata matibabu katika hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mt Meru.

Mvyovela,alisimulia kwamba katika tukio hilo mbali na watu hao kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake pia walichukua baadhi ya mali zake kama simu ya mkononi na fedha.

Hatahivyo,mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoani Arusha(APC),Claud Gwandu ametoa taarifa ya kulaani tukio hilo na kutaka mamlaka kuwachukulia hatua wanaohusika.

Katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari Gwandu alisema kwamba Myovela hakustahili kuteswa wala kupigwa kwa namna yoyote na endapo kulikuwa na suala la kijinai wahusika walipaswa kufuata taratibu na sio kujichukulia sheria mkononi.

Kwa upande wake ,Myovela amesema tukio hilo limemvunjia heshima mbele ya jamii kutokana na wahusika kumdhalilisha kwa kumtesa kwa kipigo akiwa utupu huku wakimpiga picha na kumrekodi kwa kutumia simu zao.

Waliomteka na kumdhalilisha Mwandishi wa habari akiwa Utupu ,Mikononi Mwa Polisi  Waliomteka na kumdhalilisha Mwandishi wa habari akiwa Utupu ,Mikononi Mwa Polisi   Reviewed by KUSAGANEWS on May 15, 2018 Rating: 5

No comments: