Wakulima pamba wafutiwa deni la Sh30 bilioni


Ni kama vile Serikali imetumia mtindo wa kung'ata kupuliza baada ya kutangaza kushuka kwa bei ya kununua pamba msimu huu na papo hapo kutangaza kufuta deni la zaidi ya Sh30 bilioni kwa wakulima wa zao hilo linalolimwa katika mikoa 17 nchini

Bei mpya ya Sh1, 100 kwa kilo imetangazwa  leo Mesi Mosi na Waziri wa Kilimo Dk Charles Tizeba wakati wa hafla ya uzinduzi wa msimu wa ununuzi uliofanyika katika kijiji cha Bukama wilayani Igunga, ni pungufu kwa Sh100 ukilinganisha na bei ya Sh 1, 200 ya msimu uliopita

Wakiwa bado wanajitafakari kuhusu bei mpya, wakulima waliohudhuria uzinduzi walilipuka kwa shangwe baada ya Dk Tizeba kutangaza neema ya Serikali kufuta deni la zaidi ya Sh30 bilioni kwa wakulima hao lililotokana na mkopo wa viuatilifu

"Bei ya pamba imeshuka kutokana na kuyumba kwa bei katika soko la dunia," amesema Dk Tizeba

Amesema ili kuwapunguzia gharama wakulima, Serikali imeamua kuwasamehe wakulima mkopo wa viuatilifu na sasa watalipa mkopo wa mbegu pekee

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba (TCB), Marco Mtunga, zaidi ya kilogramu 600 milioni zinatarajiwa kuvunwa msimu huu kutoka kwenye ekari milioni tatu zilizolimwa na wakulima zaidi ya 500, 000 kutoka mikoa 17 na wilaya 54 zinazolima pamba

Kuhusu mikakati ya msimu ujao wa Kilimo, Dk Tizeba alisema Serikali itasambaza bure mbegu na viuatilifu na kuimarisha huduma ya ugani kwa wakulima ili kuongeza tija
Wakulima pamba wafutiwa deni la Sh30 bilioni Wakulima pamba wafutiwa deni la Sh30 bilioni Reviewed by KUSAGANEWS on May 01, 2018 Rating: 5

No comments: