Silinde ataka wananchi vijijini kuunganishiwa umeme bure


Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde amelishauri Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwaunganishiwa umeme bure wananchi wa vijijini na kukata gharama hizo watakapokuwa wakilipia nishati hiyo kadri wanavyotumia (Luku

Pia, ameliomba Bunge kuunda kamati ya kuchunguza ufisadi uliofanywa na kampuni ya Shell mwaka 2016 wa Sh1.1 trilioni kwa kununua vitalu ya kampuni ya British Gas (BG) kwa kutokulipa tozo ya kuhamisha hisa

Akizungumza katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati leo Ijumaa Mei 25, 2018 bungeni mjini Dodoma, Silinde amesema  mradi wa Umeme Vijijini (Rea) umeshindwa kuwafikia wananchi wengi kutokana na kutokumudu gharama ya Sh27,000.

 “Tanesco inahitaji wateja, lakini kwa sababu inahitaji wateja katika miradi ya Rea kulipa Sh27,000 inakuwa ngumu kwao,  endapo Tanesco inahitaji wateja wengi itabidi  mradi wa Rea watu waunganishiwe bure vijijini ili gharama ya kuwaunganishia ilipiwe watakapokuwa wakilipia katika matumizi ya nishati hiyo,” amesema.

Kuhusu ufisadi wa Kampuni ya Shell,  Silinde amesema Serikali inapinga ufisadi na inahangaika kutafuta fedha za kutekeleza miradi mbalimbali lakini kiwango cha Sh1.1 trilioni ni kikubwa hivyo Bunge linahitaji kuchukua hatua.

Amesema kampuni hiyo imefanya ufisadi kama huo nchini Nigeria kwa kuwatumia maofisa wa Serikali, “Sasa sijui na hapa kwetu kuna waliopewa fedha, nitaomba baada ya Bunge hili kumalizika, tuunde kamati ya kuchunguza ufisadi huu.”
Silinde ataka wananchi vijijini kuunganishiwa umeme bure Silinde ataka wananchi vijijini kuunganishiwa umeme bure Reviewed by KUSAGANEWS on May 25, 2018 Rating: 5

No comments: