Kim Jong-Un asema yuko tayari kuzungumza na Trump


Pyongyang, Korea Kaskazini. Serikali imesema iko tayari kwa “mazungumzo wakati wowote na kwa njia yoyote” na Rais Donald Trump ikiwa ni muda mfupi baada ya Marekani kufuta mkutano wa kilele na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un

Msimamo huo ulitolewa na naibu waziri wa mambo ya nje Kim Kye-gwan akisema uamuzi wa Trump "unasikitisha sana".

Rais Trump aliilaumu Korea Kaskazini kwa "uhasama wa wazi" uliosababisha mkutano huo kufutwa.

Mkutano huo wa kilele uliokuwa umepangwa kufanyika Juni 12 nchini Singapore ulitarajiwa kuwakutanisha kwa mara ya kwanza rais wa Marekani aliyeko madarakani na kiongozi wa Korea Kaskazini

Kadri siku zilivyokuwa zinapita maelezo kuhusu mkutano huo hayakuwa wazi. Mazungumzo yangejikita katika suala la kuondoa silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea na hivyo kupunguza uhasama katika eneo hilo

Saa kadhaa kabla ya Trump kutoa tangazo la kufuta mkutano huo, Korea Kaskazini ilisema ilitekeleza ahadi ya kubomoa tanuru lililojengwa eneo la kurushia makombora ya nyuklia

Korea Kaskazini imeelezea kusikitishwa kwake na hatua ya rais Donald Trump kujitoa katika mazungumzo yaliyopangwa kufanyika Juni 12 huko Singapore

Kwa mujibu wa mashirika ya habari nchini humo, uamuzi huu umekuwa kinyume na matarajio ya dunia.

Inadaiwa kuwa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un alikuwa amefanya jitihada zote katika maandalizi ya mkutano huo na kwamba Pyongyang ilikuwa tayari kuhakikisha tofauti zilizopo kati ya taifa lake na Marekani zinasuluhishwa kwa namna yoyote na popote, lakini Trump mwenyewe amesema uwezekano wa kufanyika mazungumzo hayo bado upo

Kauli ya UN

Taarifa hizo pia zimeleta mshtuko kwa jumuiya ya kimataifa, ambapo Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres ameelezea kusikitishwa kwake na hatua hiyo ya Marekani huku Rais wa Korea Kusini Moon Jae-In akitoa wito wa kuwepo kwa mkutano wa dharura wa viongozi wa juu wa usalama kuhusiana na suala hilo

Mnamo Aprili, viongozi wa Korea zote walifanya mkutano wa kihistoria mpakani, na kuahidi kusitisha uhasama na kushirikiana kuelekea kusitisha matumizi ya silaha za nyuklia katika rasi ya Korea
Nchini Marekani, seneta wa Republican, Tom Cotton amempongeza

 Trump kwa kuona aliouita “udanganyifu wa Kim Jong-un” lakini seneta wa Democratic Brian Schatz amesema hatua hiyo ni sawa na kinachotokea wakati “wasanii wanapokutana na wachochezi wa vita”
Kim Jong-Un asema yuko tayari kuzungumza na Trump Kim Jong-Un asema yuko tayari kuzungumza na Trump Reviewed by KUSAGANEWS on May 25, 2018 Rating: 5

No comments: