Sikutarajia kuwakuta wafungwa wenye ugonjwa wa akili gerezani

Wengi wetu tumezoea kuwaona watu wenye matatizo ya akili wakiokota makopo majalalani, huku wengine wakiwekwa kwenye maeneo maalumu kama vile hospitali kupatiwa matibabu

Hata hivyo, hayo ni tofauti na aliyojionea mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye wakati akitumikia kifungo cha miezi mitano jela katika Gereza Kuu la Ruanda mjini hapa, anadai alishuhudia watu wa aina hiyo wakiwa ndani ya gereza hilo wakitumikia vifungo vyao

Katika mwendelezo wa mahojiano na Mwananchi, Sugu anasema akiwa kiongozi alitarajia kukutana na changamoto zinazowakabili wafungwa kama vile za chakula, malazi, matibabu na msongamano gerezani

Pia anasema alitarajia kushuhudia changamoto wanazokumbana nazo askari magereza, lakini hakutarajia kuona kuwa kuna nyingine zaidi ya hizo

“Hayo niliyatarajia na nimeyakuta sema tu sikujua kama mengine yapo kwa kiwango cha juu zaidi, sikujua kama Taifa hili linashindwa hata kununua sare za wafungwa ili watoke nje wakafanye kazi,” anasema

“Sikutarajia kama magereza nitakuta kuna wafungwa ambao ni wagonjwa wa akili, vichaa, badala ya kupelekwa Mirembe (mkoani Dodoma) na maeneo mengine unawakuta wamefungwa kwenye gereza letu lile. Nilimkuta kijana mle ni mgonjwa wa akili, lakini amekaa gerezani tangu mwaka 2001.”

Mbunge huyo anasema hilo ni jambo ambalo lilimshangaza ikizingatiwa kwamba watu hao wanastahili haki tofauti uraiani zikiwamo za matibabu

“Kwa hiyo sikutarajia kuwakuta watu wenye matatizo ya akili wapo mle wamechanganywa na wafungwa wengine wa kawaida badala ya kupelekwa Mirembe wakapate msaada,” anasema Sugu

Anasema watu wenye matatizo hayo muda wote wanakuwa wamekaa tu gerezani na hawafanyi kazi yoyote, lakini wanaendelea kutumikia kifungo na kwamba, kazi yao ni kula na kulala tu
Sugu anasema kuna wafungwa wameingia gerezani wakiwa ni wagonjwa, lakini wengine wamekumbwa na maradhi wakiwa ndani ya gereza

Ajiita mtu mashuhuri
Anasema kitu kingine ambacho hakukitarajia ni baada ya kutoka gerezani na kuona namna watu walivyompokea uraiani, jambo ambalo limemfanya kwa sasa ajione kuwa mtu mashuhuri na si maarufu tena

“Nilichokitarajia ndicho nilichokutana na nacho baada ya kutoka gerezani. Kabla ya kufungwa kwangu nilikuwa maarufu sana, lakini baada ya hili kwa sasa nimekuwa mtu mashuhuri,” anasema mbunge huyo

“Awali nilikuwa naombwa kupiga picha na watu mtaani nikipita kwa siku picha 10 hadi 20, lakini sasa hivi nikipita tu mtaani kwa siku naombwa kupiga picha na watu hadi 100.”
Awalilia askari
Sugu anasema unapozumguzia shida za gerezani, hazipo kwa wafungwa pekee, bali pia kwa askari anaodai kuwa wana hali ngumu tofauti na watu wengine wanavyoweza kuwafikiria na kuwazungumzia
Anasema hali hiyo inawakosesha ari ya kufanya kazi kwa moyo
“Shida hazipo tu kwa wafungwa, zipo kwa askari magereza. Askari wana hali mbaya. Kwa hiyo hata mtu anaposema wale wafungwa lazima wafanye kazi, si lazima wawepo watu wa kuwasimamia, sasa watu hao hawana morali, “ anasema
“Askari amepandishwa cheo hadi nyota tatu na miaka imepita, lakini cha kushangaza bado anaendelea kupokea mshahara wa nyota moja, haujapanda.”
Sugu anasema sio kwamba sare ni tatizo kubwa kwa wafungwa pekee, bali hata kwa askari na wapo wanaolazimika kujishonea nguo zao jambo linalonatia doa nchi kushindwa kuwashonea sare nyingi watakazobadilisha mara kwa mara. “Uniform (sare) kwa askari wenyewe ni shida.

Ukikuta askari wanne wamekaa, unakuta uniform rangi nne tofauti, ni kwamba kila mtu ananunua kivyake. Kwa hiyo unakuta mwingine ni cotton (pamba), mwingine tetroni, mwingine polista. Hawapewi uniform, bali wananunua wenyewe na wanalalamika.”
Anasema zaidi askari hao wanachopewa ni vifungo pekee hivyo kinachofanyika ni askari kubadili vifungo kutoka kwenye nguo ya zamani na kuweka kwenye nguo nyingine atakayokuwa ameshona
“Zaidi wanachopewa ni vifungo tu vya chuma na mwingine alipewa miaka minne iliyopita na kwa vile haviishi, hivyo sare yake ikichakaa basi anatoa vifungo anakuja kuwekea nguo mpya,” anasema Sugu
“Na wengine inafikia nguo inachakaa anapeleka kwa fundi na kichofanyika ni kubadilishwa nje inakuwa ndani na ndani inakuwa nje na hii nimeishuhudia mwenyewe kwa kuwa mafundi wanaowatumia ni wafungwa mlemle ndani. 

Kwa hiyo unakuta askari anasema ‘eee!! bwana hebu nipigie nje ndani’ kwa sababu inakuwa imepauka sana. Kwa hiyo inabadilishwa pale inakuwa nguo mpya na mtu anaigonga pale anaendelea kuivaa
Sikutarajia kuwakuta wafungwa wenye ugonjwa wa akili gerezani Sikutarajia kuwakuta wafungwa wenye ugonjwa wa akili gerezani Reviewed by KUSAGANEWS on May 20, 2018 Rating: 5

No comments: