Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo ameahidi
kuwa shule ya sekondari ya Wasichana Iringa iliyopo mkoani Iringa
itafanyiwa ukarabati ikiwa ni muendelezo wa serikali katika kuzikarabati shule
zake kongwe hapa nchini.
Waziri Jafo alitoa kauli hiyo jana wakati akiwa njiani kurudi
Dodoma akitokea mkoani Iringa ambapo pamoja na kuhudhuria sherehe za Mei Mosi
alihudhuria pia ufunguzi wa hospitali ya Wilaya ya Kilolo.
Ilimlazimu Waziri Jafo kufanya ziara ya kushtukiza shuleni hapo,
ili aweze kujionea miundombinu mbalimbali katika shule hiyo iliyo anzishwa toka
mwaka 1967.
Akizungumza na walimu, watumishi wasio walimu pamoja na wanafunzi
wa shule hiyo mara baada ya kujionea hali ya miundombinu ya shule hiyo, Mhe.
Jafo alieleza kuwa shule hiyo ni miongoni mwa shule kongwe zilizo kwenye mpango
wa ukarabati mkubwa ili kuwa na mazingira bora ya kusoma na kujifunzia.
“Katika mwaka wa fedha wa 2017/18 tulikarabati shule kongwe
43 na katika mwaka huu wa 2018/19, shule hii pamoja na zingine kongwe 45 hapa
nchini zitakuwa katika mpango kamambe wa kukarabatiwa kama tulivyokwisha fanya
kwenye shule kama 43 za awali ambapo shule 89 zote kongwe tuwe tumezimaliza”
alisema Waziri Jafo.
Aliongeza kuwa shule ya Wasichana Iringa imekuwa ni moja ya shule
bora na hivyo kufanya wanafunzi wengi kupenda kuhamia kwenye shule hiyo.
Sambamba na ukarabati huo Mhe. Jafo ameahidi kuzifanyia kazi
changamoto zote ambazo ziliainishwa mbele yake ikiwepo upungufu wa walimu wa
Fizikia na Hisabati pamoja na stahiki za walimu.
“Mama yetu Nkondola amewasilisha changamoto za walimu wa
Hesabu na Fizikia lakini pia maslahi ya walimu, naomba nieleze kuwa suala hilo
nimelichukua lakini niwaahidi kutuma wataalam kutoka kwenye wizara yangu pamoja
na wizara nyingine za kisekta kuja kufanya tathmini ya kina juu ya haya mliyoniambia,”
alisema waziri Jafo.
Aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii huku akitoa
ahadi kwa jumuiya hiyo kuwa endapo katika mitihani yao ya mwisho ya
kidato cha sita watapata daraja la kwanza (DV.1) zaidi wanafunzi ya 30
atawandalia sherehe ndogo ya kujipongeza na wale watakaopata daraja la kwanza
kati ya pointi 3-5 wataalikwa bungeni kwa gharama zake yeye Mhe.Jafo.
Mhe. Jafo akiwa katika ziara hiyo, alikagua miundombinu ya shule
ikiwapo Mabweni, Vyoo, Bwalo la Chakula, Jiko na Ofisi za Walimu na kisha
kufanya mazungumzo na walimu, watumishi wasio walimu wanafunzi sambamba na
wananchi wanaozunguka eneo la shule hiyo.
Huo umekuwa ni utamaduni wa kiongozi
huyo mwenye dhamana na OR TAMISEMI kila anapopata fursa kutembelea mikoani
kutembelea shughuli za maendeleo kwa wananchi na sekta zote ili kujionea
maendeleo ya watu na shughuli zao.
Serikali yaahidi kuikarabati Sekondari ya Wasichana Iringa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 03, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 03, 2018
Rating:





No comments:
Post a Comment