Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea
wanachama saba kutoka vyama vitatu vya upinzani ambao wameamua kurejea Chama
cha Mapinduzi (CCM) na wengine 82 kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambao
walikuwa wapiga debe.
Wanachama hao wamepokelewa leo
mchana Mei 25, 2018 wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua uwanja
mpya wa michezo unaojengwa katika kijiji cha Dodoma, kata ya Nachingwea,
wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Waziri Mkuu ambaye pia ni mjumbe wa
Kamati Kuu ya CCM, alipokea kadi nne za CUF, moja ya ACT na mbili za CHADEMA
kutoka kwa wanachama hao saba kabla hajawakabidhi kadi za CCM. Wanachama hao
saba waliokabidhiwa kadi mpya za CCM pamoja na wenzao 82, walikula kiapo cha
uaminifu mbele ya Waziri Mkuu.
Shangwe zililipuka uwanjani hapo
wakati aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA kata ya Nachingwea, Bw. Ismail
Hamisi alipokabidhi kadi yake kwa Waziri Mkuu.
Akisoma risala kwa niaba ya
wanachama wenzake walioamua kujiunga na CCM, mkazi wa Ruangwa mjini, Bw. Fred
Mnimbo amesema wameamua kurudi kwa sababu yale waliyotarajia yafanyike upinzani
hayaonekani.
“Tumegundua upinzani wa sasa ni
maslahi binafsi na si wa kuwatumikia wananchi, kinachosemwa sicho kinachotendwa
na wapinzani na pia tumeamua kuunga mkono juhudi anazofanya Rais John Pombe
Magufuli,”amesema Bw. Mnimbo
Mnimbo amesema wameamua kuhamia CCM
kwa sababu serikali iliyopo madarakani kwa sasa inatekeleza mahitaji ya
watanzania kwa asilimia 90 na pia wanataka kumuunga mkono mbunge wao wakiwa
katika chombo kimoja ili waijenge vizuri Ruangwa na Tanzania kwa ujumla.
Novemba 5, mwaka jana, Waziri Mkuu
alipokea wanachama 37 kutoka vyama vya CUF na CHADEMA kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika kijiji cha Mbekenyera, wilayani Ruangwa.
Pia Desemba 29, 2017,
alipokea wanachama 60 kutoka CUF kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
kijiji cha Nkowe kata ya Nkowe, wilayani Ruangwa.
Saba toka upinzani wajiunga CCM rasmi leo
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 25, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment