Nape: Mawaziri igeni mfano wa Dk Kalemani


Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amewataka mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano kutoona aibu kumuiga Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani aliyedai kuwa ni msikivu hata kwa mambo asiyoyapenda

Akizungumza katika mjadala wa bajeti ya Nishati mwaka 2018/19 leo Mei 25, 2018 bungeni mjini Dodoma, Nape ameanza kwa kuipongea Serikali kwa hatua ya kuiweka mikoa ya Lindi na Mtwara katika Gridi ya Taifa ambayo itafungua fursa za uwekezaji

“Nadhani ni vizuri kuboresha miundombinu ya kusambaza  umeme, kwani mvua ikinyesha kwa dakika tano miundombinu inakuwa hoi kabisa. Ni vizuri kubadili miundombinu iliyokaa muda mrefu ili iweze kubeba mzigo mzito na jambo hili litafungua fursa ya uwekezaji,” amesema

“Nampongeza Kalemani, ni kati ya mawaziri wasikivu, ukimfuata anakusikiliza na naibu wake (Subira Mgalu). Mawaziri wengine waige mfano wa huyu bwana.”

Huku akishangiliwa, Nape amesema , “katika siasa ni vizuri kusikiliza hata yale tusiyopenda kusikia, Kalemani ni kati ya mawaziri wanaosikiliza hata wasiyopenda, nina heshima kubwa kumpongeza na akienda hivi atafika mbali.”

“Tuigeni mfano wa Kalemani, akiambiwa jambo usilolipenda wewe kiongozi ni jalala kubali na utakwenda vizuri na ziko changamoto utafanikiwa kama utasikia na tutakuunga mkono.”

Kuhusu Tanesco, Nape amesema umefika wakati Serikali kuligawa shirika hilo, “igawanywe katika usambazaji na uzalishaji. Katika hili la kuzalisha umeme, Serikali tufungue milango ya sekta binafsi kwenda kuzalisha hata kama tukiingia nao ubia. Tukiruhusu sekta binafsi kushirikiana na serikali, tutakwenda vizuri.”
Nape: Mawaziri igeni mfano wa Dk Kalemani Nape: Mawaziri igeni mfano wa Dk Kalemani Reviewed by KUSAGANEWS on May 25, 2018 Rating: 5

No comments: