Mahakama Kuu imeamuru Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa
ya Fahamu Muhimbili (Moi), kumlipa fidia ya Sh100 milioni Emmanuel Didas
aliyefanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu kutokana na madhara aliyoyapa
kimwili na kiufahamu
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa amri hiyo baada
ya Didas kushinda kesi ya madai aliyoifungua dhidi ya taasisi hiyo, Katibu
Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (wakati huo) na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG
Didas alifanyiwa upasuaji usio sahihi wa kichwa badala ya
mguu ambao ulikuwa na tatizo mwaka 2007
Akitoa mchanganuo wa fidia katika hukumu ambayo Mwananchi
imeiona nakala yake, Jaji Zainabu Muruke alisema Sh1,076,620 ni fidia maalumu
kwa kukosa kipato kwa kipindi cha miezi 21
Huo ni muda ambao Didas alikaa hospitalini tangu Novemba
Mosi, 2007 alipofanyiwa upasuaji hadi Agosti 24, 2009 alipoajiriwa na Moi kama
mhudumu wa karakana
Jaji Muruke alisema kipindi kabla ya kuajiriwa na Moi, Didas
ambaye ni fundi pikipiki kulingana na ushahidi wake, alikuwa akijipatia kati ya
Sh15,000 na Sh25,000 kwa siku
“Anastahili fidia ya hasara maalumu kwa mapato aliyoyakosa
kwa miezi 21,” anasema Jaji Muruke katika hukumu.
Alisema katika
kukokotoa fidia aliyostahili, alitumia waraka wa Serikali namba 2 wa mwaka 2007
kuhusu kima cha chini cha mshahara
Katika hukumu iliyotolewa na mahakama wiki iliyopita kwa
matumizi rasmi, Jaji Muruke amebainisha Sh10.6 milioni ni gharama za huduma za
nyumbani
Amesema kiasi hicho ni fidia ya miaka 40 (wakati akiruhusiwa
kutoka hospitalini), muda ambao alikuwa amebakiza kufikia umri wa kustaafu kwa
lazima ambao ni miaka 60
Jaji alisema kwa mujibu wa ushahidi wa Didas ambao
haukupingwa na wadaiwa, kutokana na madhara aliyoyapata, ni mtu ambaye
anahitaji msaada kwa watu wengine kwa maisha yake yote akiwa nyumbani.
Alisema Sh88,323,380
ni fidia ya maumivu na mateso aliyoyapata kutokana na upasuaji usio sahihi
uliotokana na uzembe wa wataalamu katika kumhudumia
Jaji Muruke alisema ametafakari namna tukio hilo
lilivyotokea na kujiridhisha kuwa ni ajali isiyokusudiwa, pamoja na utayari wa
mdaiwa (Moi) kumwajiri Didas kama sehemu ya uponyaji na kipato kwa njia ya
mshahara.
Alisema amezingatia
kuwa mdai anaishi katika hali ya kutokujiweza katika maisha yake yote
yaliyosalia, huku akikosa kufurahia huduma muhimu ambazo angeweza kuzipata
ikiwamo kuoa, kama alivyodai mahakamani kuwa kwa hali aliyo nayo, wasichana
wamekuwa wakimkataa.
Alisema licha ya
madhara aliyoyapata ikiwa ni pamoja na kupooza upande mmoja wa mwili na
matatizo ya kiufahamu, hakuna kiwango chochote cha fidia kinachoweza kumrejesha
katika hali yake ya awali
“Mdai anastahili fidia kwa maumivu na mateso. Kwa kuzingatia
hayo ninampa Sh88,323,380 kwa maumivu na mateso,” anasema Jaji Muruke katika
hukumu hiyo
Jaji Muruke ameiamuru Moi kumlipa Didas riba ya asilimia
saba kwa fidia ya hasara ya kukosa kipato kwa miezi 21 na kwa fidia ya maumivu
na mateso yaliyotokana na makosa hayo, kutoka siku ya hukumu hadi malipo yote
yatakapokamilika
Pia, alisema iwapo Moi itakatisha mkataba wa ajira kwa
sababu zozote zile, italazimika kumlipa mshahara na mafao mengine kwa muda wote
atakaokuwa amebakiza kustaafu kwa lazima
Wakili Cornelius Kariwa aliyemwakilisha Didas katika shauri
hilo alisema kuwa Moi imewapatia taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga
hukumu hiyo iliyotolewa Agosti 30, mwaka jana
Msemaji wa Moi, Almas Jumaa alipoulizwa kuhusu hukumu hiyo
alisema hana taarifa kwa kuwa shauri hilo lilishughulikiwa na Wizara ya Afya
Kesi hiyo namba 129 ya mwaka 2012, ilifunguliwa na Sisti
Marishay kwa niaba ya Didas kutokana na hali yake ya kupooza
Didas alifanyiwa upasuaji wa kichwa alipofikishwa
hospitalini Moi kutokana na ajali aliyoipata na kuumia mguu. Wakati akifanyiwa
upasuaji wa kichwa badala ya mguu, mgonjwa mwenzake aliyekuwa amelazwa hapo,
Emmanuel Mgaya alifanyiwa upasuaji wa mguu ambao haukuwa na tatizo badala ya
kichwa
Kutokana na makosa hayo, wagonjwa wote wawili walipelekwa
katika hospitali ya Indraprastha Apollo, nchini India kwa matibabu zaidi. Mgaya
alifariki dunia baadaye
Moi yaamriwa kulipa fidia ya Sh100 milioni
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 21, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment