Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbrod Slaa amejitosa
katika mjadala wa Sh1.5 trilioni ulioibuka baada ya kutolewa kwa ripoti ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Sakata la Sh1.5 trilioni liliibuliwa na Mbunge wa Kigoma
Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ambaye alihoji kutoonekana kwa matumizi ya
fedha hizo katika ripoti ya CAG, kama zilivyoidhinishwa na bunge
Akizungumza kwa njia ya simu katika mahojiano maalumu na
Mwananchi juzi, Dk Slaa ambaye alitangaza kuachana na siasa za vyama muda mfupi
kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alisema kutoonekana kwa fedha hizo ni
matokeo ya kanuni na mfumo uliopo katika Bunge ambao unaruhusu wabunge
kupitisha bajeti hewa
Alisema sheria ya fedha inaruhusu wabunge kupitisha bajeti
za wizara bila kuwa na kiasi halisi na kiasi hicho kinawekwa mara tu baada ya
fungu hilo kupatikana ama kwa wafadhili au mchakato mwingine wowote.
“Unaporuhusu katika
vitabu vya bajeti yaani volume (Juzuu) 1, 2, 3 mpaka 4 kuwepo kwa neno ‘T’ au
kuandikwa 100 ina maana hapo huna fedha na unatarajia kuzipata wakati bajeti hiyo
ishapitishwa, hapo unawezaje kuhoji matumizi ambayo hukuyajua mapema?” Alihoji
Dk Slaa
Dk Slaa, ambaye alikuwa mbunge wa Karatu (Chadema) kuanzia
mwaka 1995 mpaka 2010, alisema huo ni uzembe mkubwa unaofanywa na wabunge na
kutoa mfano wa yeye akiwa mbunge aliwahi kukataa kupitisha bajeti ya wizara
moja
“Niligoma kupitisha bajeti ile, jambo lililosababisha
aliyekuwa Spika wa Bunge hayati Samuel Sitta anisihi sana kwani hakukuwa na
jinsi alisema hatuwezi jua maana wakati mwingine fedha za wafadhili zinachelewa
hivyo zikija kipindi cha bajeti kinakuwa kimeshamalizika. Nililazimika
kukubaliana naye hivyo hivyo, lakini mpaka leo sikubaliani na utaratibu huo,”
alisema
“Kama fedha nyingi zinatumika bila kupitishwa na Bunge kwa
sababu ndiyo mfumo wetu uliopo unawezaje kuhoji fedha hizo zilitumikaje?”
Alisisitiza Dk Slaa ambaye aligombea urais mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili
kwa kupata asilimia 27 ya kura zote
Hata hiyo, Dk Slaa alisema kuwa huenda fedha hizo zilitumika
katika ujenzi wa miradi moja kwa moja bila kufuata taratibu
Dk Slaa, ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa Chadema, alisema
takwimu za miradi hasa mikubwa haziwezi kupatikana katika kipindi cha mwaka wa
fedha wa Serikali kwani utekelezaji wake huwa unaendelea
“Ndiyo maana hata taarifa za CAG haijadiliwi kipindi tu
inapowasilishwa inabidi watendaji wapewe muda wa kwenda kujibu hoja ingawa
haikatazwi kama kuna jambo limejitokeza mawaziri kutoa ufafanuzi.”
“Cha ajabu wabunge wetu sasa huwezi kumsikia akihoji na
badala yake wanafanya vitu vingi kwa ushabiki tu. Siku hizi hakuna mtu
anayekuja na hoja, matokeo wana-conclude (wanahitimisha) tu,” alisisitiza Dk
Slaa.
Dk Slaa alijigamba kwamba wakati wake alikuwa hatoki
hadharani hata siku moja bila kuwa na data
“Nilikuwa nafanya utafiti na kama ni suala la kupambana na
ufisadi nilihakikisha kila kitu nakipata ndiyo maana uliona wakati huo niliweza
kuwachachafya baadhi ya mawaziri kwa kuwa nilikuwa sikurupuki,”alisema
Hata hivyo, Dk Slaa alisema jambo la msingi kwa wabunge
wenyewe ni kuwa makini kusimamia fedha za bajeti ya maendeleo zinazopangwa
kupelekwa katika maeneo yao
“Kwanza siku zote fedha za maendeleo zinazopangwa katika
wizara hazizidi hata asilimia 40, lakini wabunge wenyewe hawako makini katika
kufuatilia fedha zinazopaswa kufika katika maeneo yao,”alisema.
Alisema anafahamu kwa
jinsi gani wizi ulivyo mkubwa katika halmashauri mbalimbali huku baadhi ya
miradi ikishindwa kutekelezwa kwa wakati, lakini wabunge wake au diwani ama
hawaoni au hawana muda wa kufuatilia fedha hizo.</p></div><div><p>“Wabunge
wanashindwa kufuatilia fedha zinazoenda katika maeneo yao hivyo kurahisisha
ulaji kwa watu wasio na maadili,”aliongeza
Dk Slaa, ambaye aliteuliwa kuwa balozi akiwa nchini Canada
mara baada ya kutangaza kuachana na siasa za vyama, alipoulizwa anakumbuka nini
katika siasa za Tanzania alisema hana anachokumbuka.
“Sina ninacho-miss nyumbani, sasa dunia ni kijiji kila kitu
au taarifa yoyote ninayotaka kuipata naipata,” aliongeza
Akizungumzia changamoto anazokutana nazo katika kazi yake
mpya ya ubalozi, Dk Slaa alisema yeye kama balozi anayesimamia nchi tisa
ikiwamo Sweden anapata wakati mgumu kutokana na taratibu za kidiplomasia
Alisema mpaka sasa amepata utambulisho nchini Sweden tu,
lakini bado barua yake ya utambulisho katika nchi nyingine nane hazijapokelewa
hivyo kumlazimu kufanya kazi za nchi hizo akiwa Sweden.
Changamoto nyingine
alisema ni upungufu wa watumishi katika balozi hizo
Dk Slaa ajitosa sakata la Sh1.5 trilioni
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 14, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment