Chuo Kikuu Mzumbe chazindua kituo cha msaada wa kisheria


Chuo Kikuu cha Mzumbe kimezindua kituo cha msaada wa kisheria kwa ajili ya kuhudumia watu mbalimbali, wakiwamo wanaoishi vijijini wanaokabiliwa na changamoto  mbalimbali zinazohitaji ufumbuzi wa kisheria

 Akizungumza leo Mei 22, 2018 Mkuu wa Kitivo cha Sheria chuoni hapo, Profesa Cyriacus Binamungu baada ya kufanya uzinduzi wa kituo hicho cha Huduma ya Msaada wa Sheria, amesema, “Serikali imekuwa mstari wa mbele kutetea wanyonge na kusisitiza haja ya kulinda haki za wanyonge popote nchini.”

“Hivyo nasi kwa kutambua hilo tukaona kuanzisha kituo ili kuwapatia huduma ya karibu watanzania. Wananchi wamekuwa wakisimamisha misafara ya viongozi wa Serikali na kutoa malalamiko juu ya mambo kadhaa wanayoamini ni kinyume na haki zao kwa kuwa wamekosa sehemu sahihi ya kutoa malalamiko na kupata haki zao.”

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utaly amesema wanachi wengi wanashindwa kupata haki mahakamani kwa kukosa fedha, uelewa mdogo wa masuala ya kisheria, hivyo kuanzishwa kwa kituo hicho kutaleta manufaa kwa wananchi wa chini

 “Ni wakati sasa wa wanataaluma kutumia taaluma yenu kusaidia jamii inayowazunguka. Endeleeni kufanya utafiti na kujua nini hasa wananchi wanahitaji katika masula ya kisheria ndani ya wilaya ya Mvomero na Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kuweza kuwasaidia wananchi,” amesema

Makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Lugano Kusiluka amesema kuanzishwa kwa kituo hicho ni mpango mkakati wa wake wa kuhudumia jamii,  kila kitivo ndani ya chuo kinajiandaa kuhudumia jamii

Chuo Kikuu Mzumbe chazindua kituo cha msaada wa kisheria Chuo Kikuu Mzumbe chazindua kituo cha msaada wa kisheria Reviewed by KUSAGANEWS on May 22, 2018 Rating: 5

No comments: