Bashe ataka mabadiliko ya kanuni


Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe amemwomba Spika wa Bunge, Job Ndugai kuridhia kufanyika mabadiliko ya kanuni za Bunge ili kuruhusu hoja zinazohusu wananchi zinazojitokeza ndani ya Bunge zisifie kwenye vikao vya vyama ‘Party Caucus.’

Bashe amesema hayo bungeni leo Mei 18, 2018 wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2018/19 ambapo ameitaka Serikali kuiondoa bajeti hiyo na kwenda kujipanga upya kwani haijatoa dira ya kuwasaidia wafugaji na wafuvi.

Akichangia huku Bunge likiwa kimya, Bashe amesema atashangazwa na wabunge wa CCM kama wataipitisha bajeti hiyo na kuwataka kuzingatia mkataba baina ya wananchi na CCM ambao waliwapigia kura

Bashe amesema kabla ya kuingia bungeni mwaka 1995, alipewa kadi ya CCM; “Kwa hiyo mimi ni CCM kwanza kabla ya ubunge na muweke katika rekodi.”

Amesema katiba ya CCM inazungumzia madhumuni ya kuanzishwa chama hicho na inasisitiza kusimamia haki na maendeleo ya wakulima, wafanyakazi na wananchi wengine wawanaofanya shughuli halali za kujitegemea na kuona kila mtu ana haki ya kutaka malipo yanayotokana na kazi yake.

 “Nimelisoma dhumuni hili makusudi kabisa, ili Serikali wajiulize swali je wanatimiza wajibu wa wana CCM milioni saba nane waliokaa katika foleni ili kuiweka madarakani.

 “Mkataba uliopo kati ya wananchi na Serikali ni CCM na sisi, wananchi wameipa dhamana CCM, juzi tumepitisha bajeti (ya kilimo) na kwa masikitiko makubwa tutapitisha na hii, ndio kawaida yetu,” amesema

Amesema bajeti ya kilimo katika fedha za maendeleo ilitoa asilimia 18, katika bajeti ya mifugo na uvuvi haijapeleka fedha zozote huku akikataa kuiunga mkono

Bashe amesema hoja binafsi iliyokuwa iwasilishwe na Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ilishindikana kuwasilishwa bungeni na kuitwa katika kikao cha kamati ya uongozi, “Baada ya hapo tukaitwa  (Nape na Bashe) katika kikao cha chama na baadae ikaenda kufia huko, mheshimiwa spika tubadili kanuni ili hoja zinazowahusu wananchi zisiende kufia katika vikao vya chama.”

Bashe ataka mabadiliko ya kanuni Bashe ataka mabadiliko ya kanuni Reviewed by KUSAGANEWS on May 18, 2018 Rating: 5

No comments: