Watu 720,181 wameripotiwa kuugua ugonjwa wa malaria
katika vituo mbalimbali vya afya kwa miaka mitatu iliyopita mkoani Pwani
Idadi hiyo ni takriban asilimia 15 zaidi ya kiwango cha
maambukizo ya kitaifa, ambayo ni asilimia 14
Takwimu za idara ya afya mkoani Pwani, zinabainisha
wilaya na kiwango cha maambukizi yake kwenye mabano ni Halmashauri ya Chalinze
(131,197); Mkuranga (127,740); Kibiti (114,584); Kisarawe (90,079); Rufiji
(80,910); Kibaha vijijini (60,286); Mafia (53,461); Kibaha mjini (36,963); na
Bagamoyo (24,958).
Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Mkuranga
inakadiriwa kuwa na watu 243,062 kwa maana hiyo nusu yao waliugua ugonjwa huo;
Kisarawe yenye watu 110,777 takriban asilimia 87 walipata malaria; na Kibiti
yenye 133,727 wote waliugua malaria
Takwimu hizo zilimshtua mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist
Ndikilo na kulazimika kuandaa kampeni maalumu ya uhamasishaji matumizi ya dawa
za kuulia viluwiluwi vya mbu, ambayo aliizindua jana katika viwanja vya
Mailimoja na kuhudhuriwa na wadau wa afya.
Ndikilo alisema mwaka 2016 wagonjwa walioripotiwa ni
211,810 na mwaka 2017 waliongezeka hadi 268,394 na kwamba, anashindwa kujua
kiini cha tatizo hilo ilhali kiwanda cha dawa za mbu kipo mkoani hapa. Pwani
inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 1,197,933
“Dawa za kuulia viluwiluwi vya mbu zinatengenezwa hapa
Kibaha napata shida kuelewa sababu za idadi kuwa hivi, ukiangalia Rais (John
Magufuli) alishaagiza halmashauri zinunue kwa ajili ya watu wao, nikiuliza
naambiwa wananunua,” alisema Ndikilo na kuhoji:
“Je, tatizo lipo wapi wanafungia stoo? Sasa nafuatilia
hili jambo kwa umakini zaidi.”
Ndikilo alibainisha kuwa amedhamiria kuongeza matumizi
ya viuatilifu hivyo ili kudhibiti mbu na kwamba, siku ya kwanza ya kampeni ya
uhamasishaji matumizi ya dawa hizo watatoa bure dawa za thamani ya Sh1,056,000
kwa baadhi ya wananchi na watatoa elimu kwa vitendo
Pia, aliagiza wakurugenzi wote kuhakikisha wananunua
dawa hizo na kuwafikishia wananchi siyo kuziweka stoo na kwamba, ili
kuhakikisha utekelezaji unafanyika kama alivyoagiza Rais Magufuli mwaka jana
atatumia vyombo vyake mbalimbali
“Mkurugenzi atakayekwenda kinyume na agizo hili atakuwa
amekwenda kinyume na agizo la rais. sheria ipo wazi mtumishi yeyote anayekwenda
kinyume na maagizo ya rais ina maana hatoshi atabidi atupishe tu, hatutaki hizi
takwimu tena,” alisema
Awali, mganga mkuu Mkoa wa Pwani, Dk Yudas Ndungile
alisema mwaka jana malaria ilikuwa ugonjwa wa pili kati ya magonjwa makuu
matano yanayoogoza kwa vifo na iliua watu 57
Naye mkazi wa Mailimoja Kibaha, Gustaph Elius alipongeza
hatua ya mkuu wa mkoa kwa kuanzisha kampeni ya malaria inawakutanisha wananchi
wa ngazi zote pamoja na kuelimishwa matumizi sahihi ya dawa za viuatilifu vya
malaria, kwa kuwa bila elimu hata wakipewa bure inaweza ikawa kazi bure.
Wilaya hatari kwa malaria zatajwa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 14, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment