Dodoma, April 13, 2018:
Serikali imefafanua hatua
zilizochukuliwa kuhakikisha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linafaidika na
kampuni ya ubia ya StarMedia, huku ikisisitiza kuwa uongozi wa sasa chini ya
Rais John Pombe Magufuli umefanya mageuzi makubwa na ya kihistoria katika
kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati.
Wakizungumza mjini hapa jana katika
mfululizo wa mawaziri kufafanua utekelezaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG), Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, wamesisitiza ripoti ya CAG ni nyenzo muhimu kwao.
Dkt. Mwakyembe: TBC Sasa Kufaidika na StarMedia
Akizungumzia hoja ya CAG kuhusu
mkataba wa StarMedia, Waziri Mwakyembe amewaambia waandishi wa habari kuwa
changamoto kubwa iliyosababisha kampuni hiyo kutozalisha faida kwa miaka saba
sasa ni udhaifu katika uendeshaji wa kampuni na baadhi ya watendaji wa zamani
wa TBC waliotarajiwa kusimamia maslahi ya Taifa kususa, kujiuzulu na kuuacha
uendeshaji chini ya wabia kutoka China.
Hata hivyo Waziri Mwakyembe
ameongeza kuwa baada ya Serikali kumwagiza CAG kufanya ukaguzi ikiwemo pia yeye
binafsi Kuunda Kamati Maalum ya Waziri kuchunguza mkataba wa StarMedia, sasa
makubaliano yamefikiwa ili kuondoa dosari zote.
“Baada ya majadiliano ya muda mrefu
na wenzetu wa StarTimes Group (kampuni mama yenye hisa nyingi katika ubia wa
StarMedia), wenzetu hatimaye wamekubali taarifa ya CAG na mapendekezo yake
yote,” alisema Waziri Mwakyembe.
Aliyataja baadhi ya makubaliano
yaliyosainiwa ili kuigeuza StarMedia kujiendesha kwa ufanisi zaidi kuwa ni
pamoja na: kufanyiakazi hoja zote za CAG, kuongeza wafanyakazi zaidi wa
Kitanzania katika menejimenti, uwazi zaidi katika uendeshaji wa kampuni na
kuanzia sasa Bodi ya ubia inayoongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBC kuwa ndio
chombo cha juu cha uamuzi badala ya kusubiriwa maelekezo kutoka Beijing, China.
Aidha, Waziri Mwakyembe ameeleza
kuwa, kwa kuwa kampuni hiyo haikuwa kutoa gawio kwa wanahisa wake, kuanzia
mwaka huu, wakati kasoro zote zilizobainishwa na CAG na Kamati ya Waziri
zikifanyiwakazi, StarMedia itatoa ruzuku ya Shilingi Bilioni tatu (3) kwa TBC.
“Kwa niaba ya Serikali, Wizara yangu
itafuatilia kwa karibu utekelezaji na haitasita kuchukua hatua kali za kisheria
na kinidhamu kwa mtendaji wa upande wowote atakayekuwa kikwazo katika
uendeshaji wa kampuni,” alisema.
Waziri Mwijage: Tumeongeza Bajeti Kuinua
Wajasiriamali
Kwa upande wake, Waziri Mwijage,
akifafanua hoja mbalimbali zilizoelekezwa katika Wizara yake alisema
ameshaagiza hatua za haraka zichukuliwe kwa taasisi zote zilizo chini ya wizara
yake kutekeleza hoja mahsusi za CAG.
Kwa upande wa hoja ya mchango mdogo
wa Sekta ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati nchini, Waziri Mwijage amefafanua
kuwa wakati lengo kuu ni ifikapo 2025 sekta hiyo kuchangia Pato la Taifa kwa
asilimia 40, tayari kwa ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi, inachangia asilimia
35, ambazo ni kubwa ikilinganishwa na nchi jirani.
“Kwa kulinganisha mchango wa sekta
hii kwa Tanzania katika pato la taifa na nchi nyingine bado nchi yetu inafanya
vizuri. Kwa Kenya sekta hiyo inachangia takribani asilimia 25; Uganda asilimia
20; Afrika ya Kusini asilimia 36; India asilimia 40 na Malaysia 40,” alisema.
Aidha, Waziri Mwijage amesisitiza
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mageuzi makubwa katika utoaji wa mtaji
kwa Mfuko wa Kuendeleza Wajasiriamali (NEDF) na Shirika la Kuendeleza Viwanda
Vidogo (SIDO) ambapo mwaka jana Mfuko huo ulipewa Bajeti ya Shilingi bilioni
tano (5), mwaka huu Bajeti iliongezwa hadi shilingi bilioni saba (7.8).
Bajeti ya SIDO imeongezeka mpaka
shilingi bilioni 26.8; kiasi ambacho ni cha kihistoria kwani hakijapata
kutolewa na Serikali kabla ya kuingia Awamu ya Tano.
“Kama CAG alivyobaini, sekta hii ni
uti wa mgongo wa Taifa kulingana na uchangiaji wake katika pato la Taifa na
ajira. Kutokana na nafasi ya sekta hii katika kujenga taifa la uchumi wa kati,
ni mpango wa Wizara kuendelea kuiongezea rasilimali zaidi,” alisema.
Katika mfululizo wa Mawaziri wa
Serikali ya Awamu ya Tano kufafanua utekelezaji wa hoja mbalimbali za CAG,
Jumatatu ijayo itakuwa zamu ya Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo.
Serikali Yafafanua Mkataba Starmedia, Ruzuku Viwanda Vidogo
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 14, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment