Mtoto wa miezi sita, Halfani Lema, mkazi wa
Mtaa wa Ibanda Kata ya Nyegezi amefariki dunia saa chache baada ya mama yake
kuachiwa kutoka Kituo cha Polisi Igogo, Nyegezi jambo ambalo limeibua utata
Mama wa mtoto huyo, Ashura Theonest (26)
alikamatwa na polisi Aprili 2, akidaiwa kuiba simu ya jirani yake hivyo
kupelekwa mahabusu akiwa na mtoto wake
Mwenyekiti wa mtaa huo, Vedastus Mushola
alisema jana kwamba mama huyo alipofikishwa kituoni hapo aliwaomba askari
waliokuwa zamu ajidhamini ili arudi nyumbani kwani hakuwa na maziwa ya
kumnyonyesha mwanaye usiku kucha lakini hakuruhusiwa
“Pamoja na mwanamke huyo kueleza sababu
hiyo, hakuna askari aliyemruhusu, lakini baadaye usiku hali ya mtoto
ilibadilika na Aprili 3 mchana ndipo walimruhusu kwenda hospitali ya Wilaya
Butimba kwa ajili ya matibabu,” alidai Mushola
Mwenyekiti huyo alisema mtoto huyo alifariki
dunia baada ya kufikishwa hospitali wakati akitibiwa jambo lililozua hasira kwa
wakazi wa eneo hilo wakisema polisi ndiyo waliosababisha kifo hicho
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Ahmed Msangi alisema si kweli kwamba polisi ndio waliosababisha kifo
cha mtoto huyo akisema mama wa mtoto alijidhamini na kuruhusiwa kwenda
nyumbani, “Yule mama alipofika nyumbani mtoto wake, aliumwa akampeleka
hospitalini na alifia hospitali. Hizi taarifa za kwamba mtoto alifia kituoni si
za kweli, kwanza kituo cha Igogo hakina mahabusu ya wanawake kuna mahabusu ya
wanaume tu, kwa hiyo ukweli ndio huo.”
Mushola alilitaka jeshi la polisi
kuwashirikisha wenyeviti wa mitaa husika pindi yanapotokea matukio kwenye mitaa
yao ili kuepusha adha kama hizo, “Matukio madogomadogo yawe yanasuluhishwa
kwenye uongozi wa mtaa, kwanza mimi nilikuwa sijui tukio hilo hatujashirikishwa
mpaka linafika polisi.”
Mtaa wasusia msiba
Ashura hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa
sasa akieleza kuwa ana maumivu makali ya kupoteza mtoto wake lakini wananchi
wenzake wa Mtaa wa Ibanda walisusia msiba huo wakitaka maelezo ya kina kutoka
polisi
Hali hiyo ililazimu maiti kukaa mochwari kwa
siku tatu hadi pale uongozi wa polisi ulipotolea ufafanuzi suala hilo ndipo
wananchi walipokubali kumzika mtoto huyo jana katika makaburi ya mtaa huo
Ofisa utumishi wa Hospitali ya Nyamagana
Andrew Chinduo alisema hakuwa na taarifa kuhusu tukio hilo lakini alitaka
atafutwe Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba
kwani ndiye msemaji mkuu
Hata hivyo, Kibamba alipotafutwa simu yake
iliita bila kupokewa
Imeandikwa na Ngollo John, Jesse Mikofu na
Sada Amir, (Mwanza)
Utata waibuka mtoto kufariki saa chache baada ya mama yake kutoka mahabusu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 06, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment