Rais Mafuguli atangaza ajira kwa vijana 2,000 JKT walioshiriki kujenga ukuta

Rais John Magufuli amewaagiza viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuwapa ajira ya kudumu vijana 2,038 wa kujitolea wa Jeshi la Kujenga (JKT) walioshiriki katika ujenzi wa ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani, Simanjiro – Manyara

Aliagiza vijana hao wa Operesheni Jakaya Kikwete na Operesheni John Magufuli kupimwa afya zao kwanza na watakaobainika wana afya njema, wapatiwe ajira

Amiri Jeshi Mkuu alitoa agizo hilo jana wakati akizindua ukuta huo na kuagiza askari 287 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na maofisa wake 34 waliosimamia ujenzi huo kuandikiwa barua za pongezi na kuangaliwa namna ya kupongezwa kwa tukio hilo

Aliwapongeza wote kwa kujenga ukuta huo kwa muda mfupi wa miezi mitatu baada ya kuagiza ujengwe ndani ya miezi sita ili kulinda rasilimali hiyo inayopatikana Tanzania pekee

“Mkuu wa majeshi, hiki kilikuwa kipimo chako lakini nakupongeza kwa kufanikisha suala hilo na tena kwa muda mfupi hongereni sana,” alisema Rais Magufuli

Dk Magufuli alitoa ahadi ya ajira hizo, baada ya Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo katika hotuba yake, kumtaka Rais aseme neno la faraja kuhusu vijana hao

Katika hotuba yake, Jenerali Mabeyo aliwapongeza vijana hao wa JKT waliojenga ukuta huo na kumuomba Rais Magufuli awafikirie juu ya ajira ya kudumu  

Jenerali Mabeyo alisema vijana hao walianza kujenga ukuta huo Novemba mwaka jana na kumaliza Februari

Mhemishiwa Rais vijana hawa hawakupata muda kushiriki sherehe za kitaifa tangu kuanza kwa ujenzi huu Novemba mwaka jana.Muda wote walikuwa katika kazina sikuwahi kusikia wakilalamika,” alisema na kuongeza:

“Vijana hawa wanahitaji neno la faraja kutoka kwako, natumai utagusia katika hotuba yako. Nawaona wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwatamani vijana hawa.”
Kauli hiyo ilipokewa kwa shangwe na nderemo na vijana hao

Eneo jipya la Tanzanite
Katika hotuba yake, Rais Magufuli aligusia pia kuhusu kuwapo kwa eneo ambalo limegundulika kuwa na madini hayo ya Tanzanite
“Kuna eneo jingine, lakini sitalitaja hapa. Nalo lina madini ya Tanzanite, ikiwezekana nako kuzungushiwe ukuta,” alisema
“Hata kama ni Mlima Kilimanjaro, zungushia tu, na nyinyi JKT mtaendelea na suala la ulinzi hapa,” alisema
Rais Magufuli alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2015, eneo la sasa lenye Tanzanite litaendelea kutoa madini hayo kwa miaka 27 ijayo, hadi mwaka 2045
Sakata la Bombadier
Katika hotuba yake, Rais alizungumzia suala la uzalendo na kuwataka Watanzania kuwa na uzalendo kwa vitu vya kwao

“Utamkuta mtu anafurahia kwa sababu ndege imeshikwa, unafurahia nini wakati ni ndege yetu, itatusaidia sisi wenyewe,” alisema

“Hivi kwa mfano nyinyi waandishi wa habari, mmoja wenu akinyang’anywa kamera na polisi, halafu wenzako wakakaa pembeni na kuanza kushangilia, mtajisikiaje? Huu ni ushetani,”

Aliwataka Watanzania kuiga uzalendo wa vijana wa JKT.

Rais pia alimpongeza Spika Job Ndugai kwa kuunda kamati iliyochunguza uchimbaji madini ya Tanzanite.

Awali, mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alisema wachimbaji wadogo wameanza kulipa kodi ipasavyo miezi mitatu iliyopita. Alisema wachimbaji hao hawakuwa na mazoea ya kulipa kodi lakini wameanza kufanya hivyo baada ya kupewa mahesabu yao na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kuhusu ukuta
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Martin Busungu alisema gharama za ujenzi wa ukuta huo wenye urefu wa kilomita 24 ni Sh5 bilioni.
Meja Jenerali Busungu alisema awali Wizara ya Madini iliwapa tathmini kuwa ukuta huo utakuwa na urefu wa kilometa 21 hivyo wakakadiria kutumia Sh4 bilioni, lakini wamejenga wa urefu wa kilomita 24.5 na kutumia Sh5 bilioni
Kabla ya kumkaribisha Rais, Waziri wa Madini, Angela Kairuki alisema watu 6,500 kati ya 10,400 wa eneo hilo wameshasajiliwa kwa ajili ya Vitambulisho vya Taifa
Waziri Kairuki alisema watakaoruhusiwa kuingia ndani ya eneo hilo ni wale tu watakaokuwa na vitambulisho hivyo
Alisema wamefanikiwa kupata Sh700 milioni za mrabaha wa madini na wataweka vivutio vya kuongeza thamani ya madini kwenye eneo hilo
“Mheshimiwa Rais tutahakikisha fedha yetu ya madini tunayokusanya kuingiza kwenye Pato la Taifa inapanda kwa manufaa ya wananchi,” alisema Waziri Kairuki.
Rais Mafuguli atangaza ajira kwa vijana 2,000 JKT walioshiriki kujenga ukuta Rais Mafuguli atangaza ajira kwa vijana 2,000 JKT walioshiriki kujenga ukuta Reviewed by KUSAGANEWS on April 06, 2018 Rating: 5

No comments: