Ujenzi wa daraja la Pangani huko Kibaha kughalimu Milioni 100


UJENZI wa daraja litakalounganisha kata ya Pangani ,Wilaya ya Kibaha na Mpiji Magohe wilaya ya Ubungo umeanza ambapo hadi kukamilika kwake utatumia zaidi ya sh. milioni 100.

Akizungumza na wananchi kwenye eneo la ujenzi Diwani wa kata ya Pangani Agustino Mdachi alisema, tayari ujenzi umeanza na wameshaweka mawe ambayo yatatumika kama kitako cha daraja kwa kutumia waya ili kuzuia mmomonyoko.

Alieleza, mawe yanayotakiwa ni malori 100 na nyaya hizo kwa ajili ya kuweka kitako cha daraja upande wa Pangani na Mpiji Magohe, "Baada ya hapo vitalazwa vyuma kwa ajili ya daraja"

“Tumeanza ujenzi ambapo ujenzi wa daraja utafanywa na jeshi ambao tuliwaomba daraja na sasa wameshakubali ambapo mawe yameshawekwa wao wakija wataanza kuweka vyuma vya daraja,” alisema Mdachi.

Alisema ,gharama za ujenzi zinafanywa na wananchi ,kila kaya inatakiwa kutoa kiasi cha sh. 10,000 na kuwataka wananchi kujitolea ili kukamilisha ujenzi huo.

“Tumekubaliana kwenye vikao vya wananchi kuwa kila kaya itoe kiasi hicho lakini kama mtu anauwezo anaweza kutoa zaidi na tunawaomba wadau mbalimbali wajitokeze kutusaidia kukamilisha ujenzi huu ambao utasaidia kuondoa adha kwa wakazi wa kata ya Pangani,” alisema Mdachi.

Aidha alisema kuwa, kwa kaya ambayo itashindwa kutoa mchanago huo makubaliano watakapofikishwa kwenye ofisi za mtaa itabidi watoe kiasi cha shilingi 50,000 kama adhabu.

“Tunawaomba wale wenye maeneo yao huku na wanakaa jijini Dar es Salaam wanapaswa nao kuchangia ujenzi huo na endapo watashindwa kufanya hivyo watapaswa kulipia na faini kwani wamekuwa hawaonyeshi ushirikiano kwa kuwa hawakai maeneo hayo,” alisema Mdachi.

Alibainisha wananchi wa kata hiyo wanategemea huduma za kijamii Mpiji Magohe ambako ni jirani kuliko kufuata huduma Kibaha kwenye umbali wa zaidi ya kilometa nane.

Ujenzi wa daraja la Pangani huko Kibaha kughalimu Milioni 100 Ujenzi wa daraja la Pangani huko Kibaha kughalimu Milioni 100 Reviewed by KUSAGANEWS on April 22, 2018 Rating: 5

No comments: