Ujasiri wa mtoto Anthony Petro, sasa umezaa
matunda na kuleta mabadiliko katika familia yake
Anthony, mtoto wa miaka 10, mkazi wa Ngara
alisimama kidete kumzuia baba yake Petro Magogwa asiuze nyumba yao, iliyokuwa
mali pekee wanayoitegemea
Katika habari hiyo, Anthony alimzuia baba
yake asiuze nyumba na kutishia kumburuza polisi, akieleza kuwa anafanya hivyo
ili familia yao, wakiwamo dada zake wasikose mahali pa kuishi
Baada ya Mwananchi kuchapisha taarifa
zinazoonyesha ujasiri wa mtoto huyo, wasamaria wema wamejitokeza kuisaidia
familia hiyo na sasa watajengewa nyumba ya kisasa. Miongoni mwa waliojitokeza
kumjengea nyumba ni mtangazaji wa Redio Clouds na mmiliki wa mitandao ya
kijamii, Millard Ayo ambaye amejitolea kujenga nyumba nzima kwa gharama zake
Pia, uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara,
umeahidi kuihamisha familia hiyo kutoka Kitongoji cha Mukitano, baada ya
kubaini kuwa inaishi katika mazingira hatarishi
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,
Aidan Bahama alisema Millard Ayo ameahidi kujenga nyumba hiyo na halmashauri
itanunua kiwanja
“Kiwanja kimepatikana kwa Sh4 milioni na
tunataka kuhakikisha wanajengewa nyumba bora mzee huyu na watoto wake waishi
kiafya na kiusalama,” alisema
Mfadhili mwingine aliyejitokeza ni mmiliki
wa Shule ya Amani Humwe, (Mwanga, Kilimanjaro), Isihaka Msuya ambaye ameahidi
kumsomesha Anthony katika shule zake na kugharimia mahitaji yake yote
Bahama alisema dada zake Anthony nao
wanatafutiwa shule nyingine hivyo wanaojitokeza kusaidia familia hiyo
wawasilishe michango yao kupitia akaunti ya Benki ya CRDB ya halmashauri hiyo
au ofisi ya ustawi katika eneo hilo
“Anthony atapelekwa shule wiki ijayo kuwahi
masomo maana anaelekea sehemu ya ugenini hivyo anahitaji msaada zaidi wa
kitaaluma kwa kupewa muda wa ziada” alisema
Akizungumza kwa simu, Msuya alisema ameguswa
na maisha ya mtoto huyo baada ya kusoma taarifa zake. Aliahidi pia kumtafutia
mwalimu wa ziada kumfundisha ili aweze kwenda sambamba na wenzake
“Nawahakikishia Watanzania na wenye kuguswa
na maisha ya mtoto huyo kwamba atakuwa mazingira salama yenye kujali afya yake
na kumsaidia aweze kutimiza ndoto za maisha yake,” alisema Msuya
Baba mzazi wa Anthony, Petro Magogwa
aliwashukuru wasamaria wema waliojitokeza kumsaidia na watoto wake na kueleza
kuwa wakipata elimu itakuwa urithi wa maisha yao
Mbali ya wahisani hao, Bahama alisema
misaada mingine imeendelea kumiminika ndani na nje ya wilaya hiyo. Alisema
wafanyakazi wa sekta mbalimbali wamechanga kiasi cha Sh 2.1 milioni, kati ya
hizo, Sh 1 milioni ni ahadi
Michango mingine ya Anthony imekuwa
ikitolewa na wananchi kupitia namba ya simu inayoendeshwa na Kampuni ya
Mwananchi Communications Limited (MCL), ambayo imeahidi kutangaza kiasi
kilichopatikana kwa ajili ya mtoto huyo hivi karibuni.
Ujasiri wa mtoto Anthony wa Ngara wawaibua wadau kusaidia familia yake.
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 06, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment