SOMA HAPA HOTUBA YA WAZIRI WA TAMISEMI SELEMANI SAIDI JAFO , ALIYOWASILISHA BUNGENI MAPITIO, MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019
HOTUBA
YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA,
MHESHIMIWA SELEMANI SAIDI JAFO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPITIO, MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA
FEDHA YA OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA KWA MWAKA WA FEDHA
2018/19
I.
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa
hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi
wa Rehema kwa kunijalia
afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Kwa heshima kubwa namshukuru Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Rais
kwa kuongoza nchi yetu kwa falsafa ya uchumi wa viwanda na utekelezaji makini
wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2015. Vilevile,
nawapongeza Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (MB) kwa uongozi wao
mahiri na miongozo ambayo imetoa dira katika kuboresha utendaji Serikalini.
2.
Mheshimiwa
Spika, napenda kukupongeza wewe mwenyewe na Naibu Spika
kwa uongozi wenu imara
na madhubuti katika uendeshaji wa shughuli za Bunge. Nawaombea kwa Mwenyezi
Mungu azidi kuwajalia afya njema na
hekima katika kuuongoza
Mhimili huu muhimu kwa ustawi na maendeleo
ya Taifa letu. Aidha, napenda kuwapongeza
Mheshimiwa Damas Daniel Ndumbaro Mbunge wa Songea Mjini, Mheshimiwa Justine
Joseph Monko Mbunge wa Singida Kaskazini, Mheshimiwa Maulid Said Mtulia Mbunge
wa Kinondoni na Mheshimiwa Dkt. Godwin Mollel Mbunge wa Siha kwa kuchaguliwa na
kisha kuapishwa na Bunge lako tukufu ili wawatumikie wananchi waliowachagua. Vilevile
nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi kwa kuteuliwa
na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge. Waheshimiwa
Wabunge hongereni sana.
3.
Mheshimiwa Spika, mnamo Novemba 2017, Bunge lako Tukufu liliondokewa na Mheshimiwa
Leonidas Tutubert Gama aliyekuwa Mbunge wa Songea Mjini. Kwa masikitiko makubwa
napenda kutumia fursa hii kukupa pole wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika,
Wenyeviti na Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge lako Tukufu kwa kuondokewa na
Mbunge mwenzetu mahiri. Aidha, natoa pole kwa ndugu,
jamaa na marafiki wote
waliofiwa na wapendwa wao katika ajali za magari, pikipiki na nyinginezo.
Mwenyezi Mungu azilaze
Roho za
marehemu mahali pema peponi Amina.
4.
Mheshimiwa
Spika, kwa namna ya pekee naomba kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Jasson Samson
Rweikiza Mbunge wa Bukoba Vijijini, Mwenyekiti wa Kamati na Mheshimiwa Mwanne
Mchemba Mbunge wa Viti Maalum, Makamu Mwenyekiti wa Kamati kwa kuchaguliwa tena
kuiongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa. Kuchaguliwa
kwao kwa mara nyingine kuiongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa kunadhihirisha kukubalika kwao na umahiri wao wa uongozi
katika Kamati hii. OR-TAMISEMI inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Kamati hii
katika kuboresha utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi. Kamati
imepokea,
kuchambua kwa kina na hatimaye kupitisha makadirio ya Bajeti ya OR-TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2018/19.
5.
Mheshimiwa
Spika,
kutokana na taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako
Tukufu likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya OR-TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2017/18. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha
Mpango na Bajeti ya OR - TAMISEMI Fungu 56, Tume ya Utumishi wa Walimu Fungu Na. 02 pamoja
na mafungu 26 ya Mikoa kwa Mwaka wa Fedha 2018/19.
II.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18
6.
Mheshimiwa
Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18,
OR-TAMISEMI, Tume ya Utumishi wa Walimu, Mikoa na Halmashauri iliidhinishiwa shilingi Trilioni 6.57 kwa ajili ya Mishahara,
Matumizi Mengineyo na Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi Trilioni 4.27 ni Mishahara, shilingi bilioni 519.45 ni Matumizi Mengineyo na shilingi Trilioni 1.78 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha
hizo, shilingi Trilioni 1.31 ni
fedha za ndani na shilingi bilioni
467.67 ni fedha za nje. Hadi Februari, 2018 fedha zilizopokelewa ni
shilingi Trilioni 3.33 sawa
na asilimia 50.68 ya
bajeti yote.
Maduhuli
ya OR-TAMISEMI na Mikoa
7.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, OR-TAMISEMI iliidhinishiwa kukusanya Maduhuli
ya shilingi milioni 14.0. Hadi Februari,
2018, makusanyo halisi yalikuwa shilingi milioni 10.3 sawa na asilimia 74 ya lengo. Taasisi zilizo chini ya OR-TAMISEMI
zimekusanya maduhuli ya shilingi bilioni
9.0 kati ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 22.8 sawa na asilimia
44. Aidha, Maduhuli yaliyokusanywa na Mikoa yalikuwa shilingi bilioni 3.3 sawa na asilimia 96 ya makadirio ya kukusanya
shilingi bilioni 3.51 katika kipindi
hicho. Kuimarika kwa makusanyo ya maduhuli ya Mikoa kumetokana na ufanisi wa matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa GoT-HOMIS unaotumika katika Hospitali za Mikoa, matumizi ya Tiba
kwa Kadi (TIKA) katika kufanya malipo na kuimarika kwa usimamizi.
Mapato
ya Ndani ya Halmashauri
8.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Halmashauri
ziliidhinishiwa kukusanya shilingi bilioni
687.30 kutoka vyanzo vya mapato ya
ndani. Hadi Februari, 2018 shilingi bilioni
343.82 zimekusanywa sawa na asilimia 50.0
ya makadirio (kama inavyooneshwa katika jedwali Na. 1). Kiasi
kilichokusanywa ni ongezeko la shilingi bilioni
90.68 ikilinganishwa na kiasi cha shilingi bilioni 253.12 zilizokusanywa hadi Februari,
2017. Ongezeko la makusanyo limechangiwa na kuimarishwa kwa usimamizi, elimu na
uhamasishaji kwa walipa kodi, ushuru mbalimbali pamoja na matumizi ya mifumo ya
kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato.
9.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu
ya Mwaka wa Fedha 2017/18, nililifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Halmashauri
zote zitakamilisha kufunga mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato ifikapo
tarehe 30 Juni, 2017. Nafurahi kuliarifu Bunge lako kuwa Halmashauri zote 185
zimeunganishwa na zinatumia Mfumo wa Kukusanya Mapato unaojulikana kama Local Government Revenue Collection
Information System (LGRCIS).
Matumizi
10. Mheshimiwa Spika, hadi
kufikia Februari 2018, OR-TAMISEMI pamoja na Taasisi zake imepokea jumla ya shilingi
bilioni 245.17 sawa na asilimia 53 ya bajeti ya shilingi bilioni 459.41 iliyoidhinishwa na Bunge
lako Tukufu kwa Mwaka wa Fedha 2017/18. Aidha,
katika kipindi hicho, Tume ya Utumishi wa Walimu imepokea jumla ya shilingi bilioni 6.92 kati ya shilingi bilioni 12.42 zilizoidhinishwa na Bunge
sawa na 56. Kwa upande wa Mikoa,
fedha zilizoidhinishwa na Bunge ni shilingi bilioni 285.13 ambapo kiasi kilichopokelewa ni shilingi bilioni 156.18 sawa na asilimia 55. Vilevile, Halmashauri
ziliidhinishiwa shilingi Trilioni 5.83
ambapo tayari jumla ya shilingi Trilioni
3.17 zimepokelewa hadi Februari, 2018 ikiwa ni sawa na asilimia 54.
11. Mheshimiwa Spika,
fedha zilizopokelewa na kukusanywa zimetumika kutekeleza majukumu ya msingi ya
OR-TAMISEMI, Taasisi zilizo chini ya OR-TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri kwa
ajili ya kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi kwa kuzingatia misingi ya
utawala bora.
Utawala
Bora
12.
Mheshimiwa Spika, mafunzo ya kuwajengea
uwezo na utawala bora Wakuu wa Mikoa yote 26 yametolewa Tanzania Bara. Aidha, Makatibu Tawala wa Mikoa 26, Wakuu wa Wilaya 139,
Wakurugenzi wa Halmashauri 185,
Maafisa Utumishi 185 na Maafisa Mipango
185 wamepata mafunzo kuhusu majukumu na mipaka ya kazi zao,
maadili ya uongozi, utawala bora, usimamizi wa Sheria, Kanuni na Miongozo
mbalimbali. Mafunzo hayo yamesaidia kuboresha utendaji na kuondoa mwingiliano
wa majukumu baina ya Viongozi na Watendaji. Aidha, Viongozi na Watendaji hao wamekumbushwa
wajibu wa kusimamia maendeleo na kutatua kero mbalimbali za wananchi katika
maeneo yao ya utawala.
Usimamizi
wa Fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa
13.
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 27 (2) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inaelekeza kuwa ni
wajibu wa kila Mtanzania kulinda mali za umma na kuhakikisha zinatumika kwa
maslahi ya Watanzania wote. OR-TAMISEMI imeendelea kusimamia
matumizi ya fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia Katiba ya
Nchi, Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290, Sheria ya Bajeti ya Mwaka
2015, Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya
Mwaka 2011, Kanuni zake za Mwaka 2013 na marekebisho yake ya Mwaka 2016.
14. Mheshimiwa Spika, usimamizi wa fedha katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa umeendelea kuimarika. Kwa mujibu wa Hati za
Ukaguzi zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kati ya
Halmashauri 185 zilizokaguliwa Mwaka wa Fedha 2016/17, Halmashauri 166
sawa na asilimia 90 zimepata hati safi, Halmashauri 16 zimepata hati
zenye mashaka na Halmashauri 3 tu ndizo zimepata hati chafu ikilinganishwa na
ukaguzi wa Mwaka wa Fedha 2015/16 ambapo kati ya Halmashauri 171
zilizokaguliwa, Halmashauri 138 sawa na asilimia 81 zilipata hati
safi, Halmashauri 32 zilizopata hati zenye mashaka na Halmashauri 1 ilipata
hati chafu.
15. Mheshimiwa Spika, OR-TAMISEMI imeimarisha shughuli za ufuatiliaji na tathmini ili
kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa na thamani ya fedha zilizotumika
katika miradi ya maendeleo. Katika Mwaka wa Fedha 2017/18, ufuatiliaji
umefanyika katika Mikoa yote 26 na Halmashauri 182 ambao
ulihusisha kukagua miradi na shughuli mbalimbali za utawala bora. Vilevile, ukaguzi maalum kuhusu
tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma umefanyika katika Halmashauri za
Wilaya za Hanang’, Kilindi, Mbulu, Tunduru, Morogoro, Nkasi, Same, Chalinze,
Bumbuli, Halmashauri ya Mji wa Mbinga na Halmashauri za Manispaa za Ilala,
Ubungo, Temeke na Kinondoni na Mpanda.
16. Mheshimiwa Spika, hatua mbalimbali za kudhibiti ubadhirifu na
ukiukwaji wa Sheria zimechukuliwa ambapo watumishi 434 waliobainika kwa
ubadhirifu na ukiukwaji wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma wamechukuliwa
hatua za kinidhamu na wengine 28 michakato ya nidhamu inaendelea ili waweze
kufikishwa Mahakamani.
17. Mheshimiwa Spika,
OR-TAMISEMI imeendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti kupitia mfumo Funganishi wa
Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Fedha (Epicor) ambapo Halmashauri zilizounganishwa
kwenye mfumo huo zimeongezeka kutoka 168 katika Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi
Halmashauri zote 185 katika Mwaka wa Fedha 2017/18.
Mfumo
umeongeza uwazi na uwajibikaji katika mchakato mzima wa malipo. Aidha, Serikali
imeanzisha mfumo wa Tanzania
Interbank Settlement System – TISS ambapo malipo yote ya Serikali
yanafanyika kutoka akaunti zilizofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania kwenda moja
kwa moja kwa mlipwaji. Mfumo wa TISS umeunganishwa
katika Mikoa 11 ya Arusha, Dodoma, Dar
es Salaam, Mbeya, Morogoro, Lindi, Mtwara, Mwanza, Songwe, Pwani na Tanga yenye
jumla ya Halmashauri 77. Mikoa 15
iliyobaki na Halmashauri zake itaunganishwa kwenye mfumo katika Mwaka wa Fedha
2018/19.
Uwekezaji katika Mamlaka za
Serikali za Mitaa.
18. Mheshimiwa Spika, OR-TAMISEMI inaratibu
uanzishaji, utunzaji na uendelezaji wa maeneo ya uwekezaji katika kila Mkoa na
Halmashauri. Halmashauri zinaendelea kutenga maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya
viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya kujenga
uchumi wa viwanda. Hadi Februari, 2018 Halmashauri 184 zimetenga maeneo yenye ukubwa wa hekta 196,710 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vidogo, viwanda vya kati
na viwanda vikubwa. Aidha, katika utekelezaji wa agizo la ujenzi wa viwanda
vidogo na vya kati 100 kwa kila
Mkoa, jumla ya viwanda vipya 1,285
vimejengwa kati ya Mwezi Novemba, 2017 hadi Machi, 2018 ambapo ni sawa na asilimia 49.4 ya utekelezaji.
Matumizi ya Mifumo ya TEHAMA
19.
Mheshimiwa Spika, OR-TAMISEMI imeendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA iliyopo
kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utendaji na uwajibikaji. Mfumo mpya wa Facility Financial Accounting and Reporting
System (FFARS) umeandaliwa ili kuwezesha upelekaji wa fedha na utoaji wa
taarifa katika vituo vya kutolea huduma katika ngazi za msingi za Serikali za
Mitaa. Aidha, Mfumo wa kuandaa Mipango na Bajeti za Halmashauri (PlanRep-Web
based) umeboreshwa na kutumika kuandaa bajeti za Halmashauri zote 185 kwa Mwaka
wa Fedha 2018/19. Mifumo hii ya
kielektroniki imeongeza ufanisi katika utendaji kazi, imepunguza gharama, imeongeza
udhibiti wa rasilimali, uwajibikaji, upatikanaji wa taarifa na hivyo kuwezesha Viongozi
kufanya maamuzi kwa wakati.
20. Mheshimiwa Spika,
ili kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika Mikoa na Mamlaka za Serikali
za Mitaa, mafunzo ya kujenga uwezo yametolewa kwa watumishi 262 wa Mikoa na 1,507 wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mafunzo hayo yametolewa kuhusu matumizi ya mifumo
ya PlanRep, FFARS, Basic Education Management Information
System (BEMIS), Government of Tanzania
Hospital Management Information System (GoT-HOMIS) na Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS). Matumizi
ya TEHAMA yamesaidia katika upatikanaji wa takwimu za msingi kwa ajili ya kusaidia
kufanya maamuzi mbalimbali ya Serikali, uwazi na uwajibikaji. OR-TAMISEMI itaendelea kubuni, kuratibu, kujenga,
kuboresha na kusimamia mifumo na miundombinu ya TEHAMA kwa ajili ya ukusanyaji
wa takwimu, uchakataji, uchambuzi, utunzaji na utoaji wa taarifa zilizo sahihi
kutumika katika mipango kwenye Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili
kuimarisha uwajibikaji na uadilifu.
Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi
21. Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Mfuko wa Maendeleo
ya Vijana na Wanawake umetengewa shilingi bilioni
61.6 ikiwa ni asilimia 10 ya
mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya mikopo ya vikundi 18,233. Hadi
Februari, 2018 kiasi cha shilingi bilioni 15.6 zimetolewa
kwa vikundi 8,672 vya Wanawake na
Vijana.
22. Mheshimiwa
Spika, OR-TAMISEMI kupitia programu ya LocaL Investment Climate (LIC)
inawawezesha wananchi kiuchumi kwenye Sekta za Kilimo, Biashara na Uvuvi katika
Mikoa ya Kigoma na Dodoma. Maeneo yanayopewa kipaumbele ni uzalishaji na
uchakataji wa mazao ya Mchikichi, Zabibu, mbogamboga, muhogo, mpunga, Alizeti
na ufugaji wa samaki. Hadi Februari, 2018 jumla ya shilingi bilioni 2.89 zimetumika katika kuendesha shughuli za programu
hiyo. Aidha, jumla ya wananchi 1,000 wamewezeshwa
kuandaa maandiko ya kibiashara.
Utoaji
wa Huduma za Afya
23. Mheshimiwa Spika,
katika sekta ya afya, OR-TAMISEMI inahusika na uratibu pamoja na usimamizi wa
Hospitali za Halmashauri, Vituo vya Afya na Zahanati ili kuhakikisha zinatoa
huduma bora za afya kwa wananchi. Hospitali za Halmashauri zilizopo ni 120 kati ya Hospitali 184 zinazohitajika sawa na asilimia 65 ya lengo. Kati ya Hospitali
hizo, 77 zinamilikiwa na Serikali na
43 zinamilikiwa na Mashirika Binafsi
ambazo ni Hospitali Teule zilizoingia mkataba wa utoaji huduma na Halmashauri.
24. Mheshimiwa Spika,
Vituo vya Afya vilivyopo ni 696 sawa
na asilimia 15.7 ya lengo la kuwa na
Vituo vya Afya 4,420. Kati ya hivyo,
vituo 513 vinamilikiwa na Serikali
na vituo 183 vinamilikiwa na Sekta
Binafsi na Mashirika ya Dini. Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa Vituo
vya Afya 208 ili kuviwezesha kutoa huduma
za dharura za upasuaji kwa ajili ya kuboresha huduma zote za Vituo vya Afya.
Kati ya Vituo hivyo 15 ni vipya na 14 ni zahanati zilizopandishwa hadhi,
vituo vitatu (3) ni maboma ambayo
yalikuwa hayajakamilika. Ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya 44 umekamilika, vituo 139 vitakamilika kabla ya tarehe 30
Juni, 2018 (kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 2) na vituo 25 vitaanza
ujenzi Aprili, 2018. Vituo hivyo vitagharimu shilingi bilioni 93.5 hadi kukamilika. Sambamba na ujenzi, vituo hivyo
vimetengewa shilingi bilioni 50.2
kwa ajili ya kununulia vifaa tiba pamoja na samani ili kuviwezesha kuanza kutoa
huduma. Aidha, shilingi bilioni 13.0
zimetumika kwa ajili ya kuboresha mifumo ya kupeleka fedha vituoni ikiwemo
mishahara ya Wasaidizi wa Hesabu 535
kwenye vituo vya Afya na Zahanati zenye wagonjwa wengi.
25. Mheshimiwa Spika,
mpango uliopo ni kukamilisha ukarabati na ujenzi wa vituo vyote ili kuboresha
huduma za Afya na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Kazi hiyo inatekelezwa
kwa uratibu na usimamizi wa OR-TAMISEMI ikishirikiana na Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wadau wa maendeleo wa Mfuko wa
Pamoja wa Afya. Vigezo vilivyotumika kuchagua vituo hivyo ni pamoja na idadi ya
watu katika Kata, umbali kutoka kituo cha kutolea huduma kilichopo na hali ya
kijiografia ya eneo husika.
26. Mheshimiwa Spika,
idadi ya Zahanati zilizopo nchini ni 6,640
sawa na asilimia 53 ya lengo la kuwa
na Zahanati 12,545 zinazohitajika.
Kati ya hizo, zahanati 4,554 sawa na
asilimia 47.9 zinamilikiwa na Serikali
na Zahanati 2,086 zinamilikiwa na
Sekta Binafsi. Katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Serikali iliidhinishiwa na Bunge
lako Tukufu jumla ya shilingi bilioni 35.5 kwa ajili ya kuendelea na
ujenzi wa Zahanati, kipaumbele kikiwa ni kukamilisha ujenzi wa maboma
yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.
27. Mheshimiwa Spika,
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imekamilisha ujenzi
wa nyumba 578 za watumishi wa afya
katika vituo vya afya 268 kwenye
Halmashauri 51. Nyumba nyingine 262 zinaendelea kujengwa na imepangwa
ziwe zimekamilika kabla ya tarehe 30 Juni, 2018. Lengo la Serikali ni
kuhakikisha kila kituo cha kutolea huduma za Afya kinakuwa na nyumba angalau
mbili ifikapo Mwaka 2020 ili kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.
Upatikanaji
wa Dawa na Vifaa Tiba
28. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeongeza bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba, chanjo na vitendanishi
kutoka shilingi bilioni 31
zilizotengwa Mwaka wa Fedha 2015/16 hadi shilingi bilioni 269 zilizotengwa katika Mwaka wa Fedha 2017/18. Kati ya
fedha hizo, shilingi bilioni 98.08
zimetengwa kwa ajili ya huduma ya afya ya msingi kwenye Hospitali za Wilaya,
Vituo vya Afya na Zahanati.
29. Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka wa Fedha 2016/17, kiasi cha shilingi bilioni 17.3 zilizoidhinishwa kwa ajili ya dawa na vifaa tiba
katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zilibaki Bohari ya Taifa ya Dawa (MSD)
kutokana na kukosekana kwa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi. Hadi Desemba,
2017 vituo vya kutolea huduma za Afya katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa vimetumia shilingi bilioni 35.3
zikijumuisha bakaa iliyobaki MSD katika Mwaka wa Fedha 2016/17 kwa ajili ya
dawa na vifaa tiba. Upatikanaji wa dawa muhimu umeongezeka kufikia asilimia 92 ikilinganishwa na asilimia 81 katika kipindi kama hicho Mwaka
2016.
30. Mheshimiwa Spika,
OR-TAMISEMI imeanza matumizi ya mfumo wa jazia kwa kutumia Washitiri (Prime
Vendor) katika Mikoa ya Dodoma, Morogoro na Shinyanga ambao lengo ni kuhakikisha
dawa zinakuwepo katika vituo vya kutolea huduma za Afya endapo zimekosekana
MSD. Azma ya Serikali ni kuhakikisha mfumo huu unatumika katika Mikoa yote 26
nchini.
Huduma za Ustawi wa Jamii
31. Mheshimiwa Spika,
Usimamizi wa huduma za Ustawi wa Jamii unatekelezwa kwa kuzingatia Sheria ya
Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2010. Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria hiyo
Mwaka 2017, OR-TAMISEMI ilitoa Waraka kwenda Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuwakumbusha na kuwataka Wadau wote katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa kutekeleza maelekezo ya Sheria hiyo ili kuimarisha ustawi wa
makundi yote ya jamii hususan Watu Wenye Ulemavu. Watu Wenye Ulemavu wapatao 221,090
wakiwemo wanawake 110,290 na wanaume
110,800 wametambuliwa na kupatiwa huduma zikiwemo vifaa vya shule, kofia za kuzuia jua na
mafuta ya ngozi kwa Watoto Wenye Ualbino
1,836.
32. Mheshimiwa
Spika, Serikali imewajengea
uwezo Maafisa Ustawi wa Jamii 35
kuhusu utoaji wa huduma ya ulinzi na usalama wa mtoto na msaada wa kisaikolojia
na kijamii kwa watoto 4,536 wakiwemo
wanawake 2,211 na wanaume 2,325
katika makambi ya Ntuta, Nyarugusu
na Mtendeli yaliyoko Mkoani Kigoma. Mkakati
huu unakusudia kuboresha ustawi wa jamii kwa makundi yote.
33. Mheshimiwa Spika,
huduma za matunzo ya Watu Wenye Ulemavu zinatolewa katika makazi maalum 17 yanayomilikiwa na Serikali na makazi
24 yanayohudumiwa na Mawakala wa
hiari. Huduma hizo ziko kwenye Mikoa ya Mara, Mwanza, Tanga, Dar es Salaam,
Morogoro, Dodoma, Kigoma, Kagera, Arusha, Kilimanajaro na Rukwa. Watu 100,000 Wenye Ulemavu wanahudumiwa
katika makazi hayo. Aidha, huduma za ushauri nasihi na huduma za mazoezi tiba
na unasihi zimetolewa kwa Watu 1,150
Wenye Ulemavu kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii.
Mfuko wa Afya ya Jamii
34. Mheshimiwa
Spika, jumla ya wanachama 12,278,406 wamejiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) katika Mwaka
2017. Wananchi katika Halmashauri 154
kati ya 185, wanatumia kadi za CHF
na TIKA katika maeneo ya miji. Hadi Machi, 2018 jumla ya shilingi bilioni 22.5 zilikuwa zimekusanywa na
Halmashauri. Halmashauri zimetunga Sheria Ndogo ambazo zimeweka viwango vya
kuchangia kati ya shilingi 5,000
hadi 30,000 kwa kila mwanachama. Halmashauri zote zimeelekezwa kuhakikisha
fedha hizo zinatumika katika ununuzi wa dawa na vifaa tiba ili kuboresha huduma
za Afya kwa wananchi.
35. Mheshimiwa Spika,
Wazee 1,652,206 wasiokuwa na uwezo
wametambuliwa katika Mikoa 22 ambapo
kati yao 462,513 wamepatiwa kadi za
CHF kwa ajili ya matibabu bila malipo. Halmashauri 117 zinaendelea na utambuzi wa Wazee ili kuwapatia kadi za CHF.
Mpango uliopo ni kuhakikisha Halmashauri zote 184 zinawatambua Wazee wasiokuwa na uwezo ili kuwapa matibabu bila
malipo.
Usimamizi wa Elimu ya Msingi na Sekondari
Nchini
Elimu ya Awali na Msingi
36. Mheshimiwa Spika,
OR-TAMISEMI inaendelea kuboresha utoaji wa elimu katika ngazi zote za elimu ya
Awali, Msingi hadi Sekondari. Hadi Machi, 2018 shule za msingi zilizopo ni 16,140 ambapo kati ya hizo shule 16,004 zina madarasa ya elimu ya awali ikilinganishwa
na shule 14,946 zilizokuwepo Mwaka
wa Fedha 2016/17. Kwa ujumla shule zenye madarasa ya awali ni asilimia 99.2 ya lengo. Wanafunzi wa
elimu ya Awali walioandikishwa hadi Machi, 2018 ni 1,283,790 (Wavulana 647,467 na Wasichana 636,323) sawa na asilimia 85.7 ya lengo la kuandikisha
wanafunzi 1,498,043 (Wavulana
746,102 na Wasichana 751,941) hadi tarehe 31 Machi, 2018 (kama inavyooneshwa katika
Jedwali Na. 3).
37. Mheshimiwa Spika,
uandikishaji wa Wanafunzi wa Darasa la Kwanza hadi kufikia Machi, 2018 umefikia
wanafunzi 1,751,221 (Wavulana
880,391 na Wasichana 870,830) ikilinganishwa na lengo la kuandikisha wanafunzi 1,732,303 (Wavulana 871,918 na
Wasichana 860,385) sawa na asilimia
100.1 ya lengo (kama
inavyooneshwa katika Jedwali Na. 4). Wito
unatolewa kwa Wazazi/Walezi na jamii
kwamba wanao wajibu wa kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule
anaandikishwa na kuanza masomo.
38. Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018, Serikali kwa kushirikisha
wadau mbalimbali wa elimu na wananchi, imekamilisha ujenzi wa vyumba vya
madarasa 2,278 kwa shule za msingi.
Ujenzi huo umeongeza idadi ya vyumba vya madarasa kutoka 120,766 vilivyokuwepo Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi vyumba vya
madarasa 123,044 kufikia Machi 2018 sawa
na ongezeko la asilimia 1.8. Hivyo,
mahitaji ya vyumba vya madarasa yamepungua hadi 264,594 ikilinganishwa na
266,872 Mwaka 2017. Aidha, nyumba
za walimu zimeongezeka kutoka nyumba 43,075
zilizokuwepo Mwaka 2017 hadi 43,365 sawa na ongezeko la nyumba 290 zilizojengwa hadi Machi, 2018.
39. Mheshimiwa Spika, matundu
ya vyoo yameongezeka kutoka 167,496
hadi 173,770 sawa na ongezeko la matundu
ya vyoo 6,274 yaliyojengwa kufikia
Machi, 2018. Ongezeko hilo limepunguza upungufu uliokuwepo kutoka matundu ya
vyoo 350,110 Mwaka 2017 hadi 343,832 kufikia Machi, 2018. Vilevile,
katika Mwaka wa Fedha 2017/18, jumla ya Ofisi za Walimu 316 na maktaba 165
zimejengwa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
40. Mheshimiwa Spika, walimu
wa shule za msingi waliokuwepo nchini Mwaka wa Fedha 2016/17 ni 175,946 ambapo mahitaji yalikuwa ni
walimu 273,463 hivyo upungufu ulikuwa
ni walimu 97,517. Katika Mwaka wa Fedha
2017/18, Serikali imefanikiwa kuajiri walimu wapya 2,767. Aidha, Serikali imewahamisha walimu wa ziada 8,834 wa masomo ya Sanaa na Lugha
kutoka shule za sekondari kwenda katika shule za msingi na kufanya upungufu wa
walimu kuwa 85,916 ikilinganishwa na
upungufu wa walimu 97,517 katika
Mwaka 2017.
41. Mheshimiwa Spika,
jumla ya wanafunzi 1,192,655
walisajiliwa kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Upimaji wa Darasa la Nne (SFNA)
katika Mwaka 2017 wakiwemo Wavulana 590,380
na Wasichana 602,275. Wanafunzi
waliofanya Mtihani huo walikuwa 1,158,499
(Wavulana 569,718 na Wasichana 588,781) sawa na asilimia 97.1 ya lengo. Kati ya Wanafunzi waliofanya Mtihani huo,
jumla ya wanafunzi 1,086,156
(wavulana 513,916 na wasichana 554,240) sawa na asilimia 93.76 walifaulu na kujiunga na Darasa la Tano. Hivyo,
ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 93.36
Mwaka 2016 hadi asilimia 93.76 Mwaka
2017.
42. Mheshimiwa Spika, wanafunzi
waliohitimu Darasa la Saba Mwaka 2017 walikuwa 909,950, wakiwemo wasichana 480,784
na wavulana 429,166. Kati ya hao,
wanafunzi 662,035 wakiwemo wasichana
341,020 na wavulana 321,015 walifaulu mtihani huo sawa na asilimia 72.75. Ufaulu umeongezeka
kutoka asilimia 70.84 Mwaka 2016
hadi asilimia 72.75 Mwaka 2017 kutokana
na kuboreshwa kwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia na kuimarishwa kwa
usimamizi wa shule.
43. Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka wa Fedha 2017/18, OR-TAMISEMI kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu
Kata 17,518 kuhusu mbinu za kufundisha Kusoma, Kuandika na
Kuhesabu. Aidha, mafunzo ya uongozi yametolewa kwa Walimu Wakuu 5,333
na mafunzo ya uandaaji mipango ya elimu yametolewa kwa Maafisa Elimu na Maafisa
Mipango katika Halmashauri 51. Vilevile, walimu 4,452 na Maafisa Elimu Kata 998 kutoka katika Mikoa saba wamepatiwa
vifaa vya TEHAMA (tablets) 5,450 kwa
ajili ya kuimarisha mfumo wa kukusanya takwimu. Katika kuimarisha
ufuatiliaji na usimamizi wa Elimu ngazi za Kata, Maafisa Elimu Kata 2,025
wamepatiwa Pikipiki ili kurahisisha utendaji wa majukumu yao. Aidha, Wataalam 314 wamepatiwa mafunzo kwa ajili ya kuwatambua na kuwa hudumia
watoto wenye mahitaji maalum.
Elimu
ya Sekondari
44. Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka 2018 wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza
walikuwa 661,059 (wavulana 320,849
na wasichana 340,210) ikinganishwa
na wanafunzi 555,291 (wavulana
283,751 na wasichana 271,540) waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza
katika Mwaka 2017 sawa na ongezeko la wanafunzi 105,768 ambao ni asilimia
19.05. Hadi Machi, 2018 wanafunzi 586,830
(wavulana 285,847 na wasichana 300,983) wameripoti katika shule
walizopangiwa sawa na asilimia 88.8 (kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 5) na wanafunzi 74,229 bado hawajaripoti katika shule walizopangiwa. OR-TAMISEMI imetoa
maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanafunzi wote
waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza wanafuatiliwa ili kuhakikisha wanajiunga
na shule walizochaguliwa.
45. Mheshimiwa Spika,
nyumba za walimu zimeongezeka kutoka 12,922
zilizokuwepo Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi
nyumba za walimu 13,196 sawa na
ongezeko la nyumba za walimu 274 zilizojengwa hadi Februari, 2018. Vyumba
vya madarasa vimeongezeka kutoka 39,490
kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi vyumba 40,278
kufikia Februari, 2018 ikiwa ni ongezeko la vyumba 788. Aidha, matundu ya vyoo yameongezeka kutoka 51,327 kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi
kufikia matundu 53,398 hadi
Februari, 2018 ikiwa ni ongezeko la matundu ya vyoo 2,071. Katika kipindi hicho, miundombinu mingine iliyojengwa ni
maktaba 176, mabweni 543, majengo ya utawala 36 na maabara 165. Utekelezaji umefanyika kupitia fedha za Programu ya Elimu ya
Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) pamoja na fedha za ndani za Halmashauri. Serikali inaendelea na ukarabati wa shule kongwe 89 ambapo shule 43
ukarabati wake umekamilika. Ukarabati unahusisha kuondoa miundombinu
iliyochakaa ikiwemo paa, kupiga rangi, kuboresha mifumo ya maji safi na maji
taka, umeme na kujenga miundombinu mipya kulingana na mahitaji.
46. Mheshimiwa Spika,
walimu waliopo katika shule za sekondari nchini ni 88,865. Walimu wa masomo ya Sanaa waliopo ni 69,395 ikilinganishwa na mahitaji ya walimu 48,245 sawa na ziada ya walimu 20,712.
Kwa upande wa masomo ya sayansi na hisabati, walimu wanaohitajika ni 35,136 na walimu waliopo ni 19,459 sawa na upungufu wa walimu 15,677.
47. Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea kutoa fedha za Elimumsingi
Bila Malipo kila Mwezi tangu mpango huu uanze kutekelezwa Desemba, 2015. Katika
kipindi cha kuanzia Julai 2017 hadi Februari, 2018 Serikali imefanikiwa kutoa jumla
ya shilingi bilioni 172.4 kugharamia
Mpango wa Elimumsingi bila Malipo ambapo kati ya hizo shilingi bilioni 77.2 zimetolewa kwa shule za
msingi na shilingi bilioni 89.2
zilitolewa kwa shule za sekondari nchini. Utoaji wa Elimumsingi Bila Malipo
umesaidia watoto wenye umri wa kwenda shule kupata fursa ya kusoma. Wazazi
wamebaki na jukumu la kumwezesha Mwanafunzi kupata madaftari, kalamu, sare za
shule, chakula na nauli kwa wanafunzi wa shule za kutwa.
48.
Mheshimiwa Spika, kati ya wanafunzi
521,759 (wasichana 270,174 na wavulana 251,585) waliosajiliwa kufanya
Mtihani wa Taifa wa Upimaji wa Kidato cha Pili, wanafunzi 486,742 (wasichana 254,538 na wavulana 232,204) walifanya mtihani huo. Wanafunzi
waliofaulu ni 433,453 (wasichana 224,736
na wavulana 208,717) sawa na asilimia 89.05 na
kufanikiwa kuendelea na Kidato cha Tatu. Kwa upande wa Mtihani wa Taifa wa
Kidato cha Nne, jumla ya wanafunzi
287,713 (wasichana 143,728 na wavulana 143,985) walifaulu mtihani huo
katika Mwaka 2017 sawa na asilimia 77.09
ikilinganishwa na wanafunzi 374,950 (wasichana
191,956 na wavulana 182,994) waliofanya Mtihani huo. Ufaulu katika Mtihani wa
Kidato cha Nne umeongezeka kutoka asilimia
75.99 Mwaka 2016 hadi asilimia 77.09
kwa Mwaka 2017. Kati ya wanafunzi 62,725
waliofanya mtihani wa Kidato cha Sita Mwaka 2017, wanafunzi 61,308 walifaulu sawa na asilimia 97.74 ikilinganishwa na
wanafunzi 63,525 waliofaulu Mwaka
2016.
Usimamizi
na Uendelezaji Vijiji na Miji
49. Mheshimiwa Spika, ukuaji
wa miji ni fursa ya maendeleo kijamii, kiuchumi na kimazingira. Mipango ya
matumizi bora ya ardhi imeandaliwa katika Vijiji 1,764 ikilinganisha na Vijiji 12,545
nchini sawa na asilimia 14. Aidha,
upimaji wa mipaka ya Vijiji umefanyika katika Vijiji 11,256 kati ya Vijiji 12,545
sawa na asilimia 90. Vilevile,
Halmashauri 161 kati ya 184 zipo katika hatua mbalimbali za maandalizi
ya Mipango ya Jumla ya uendelezaji miji ili kuhakikisha kunakuwa na ukuaji
endelevu wa miji kuepuka uwepo wa miji ambayo haijapangwa vizuri. Aidha, Miji
Midogo 800 inayochipukia
imebainishwa ili iweze kuendelezwa kabla haijavurugika.
50. Mheshimiwa Spika,
OR-TAMISEMI imekamilisha uandaaji wa mwongozo wa utoaji wa vibali vya ujenzi na
usimamizi wa ukaguzi wa majengo ambao umesambazwa kwenye Mikoa na Halmashauri zote.
Mwongozo huo utapunguza muda wa utoaji wa vibali vya ujenzi ambapo kibali
kitatolewa kati ya siku 7 hadi 30 kutegemeana na aina ya jengo
ikilinganishwa na siku 60 hadi 309 hapo awali. Mwongozo umesisitiza
wadau wote wanaohusika na utoaji wa idhini ya vibali kuwa katika eneo moja ili
kuondoa urasimu. Utekelezaji wa mwongozo huo utaiwezesha Tanzania kuboresha
mazingira ya kufanyia biashara kwa kupunguza muda wa upatikanaji wa huduma
hiyo.
Uendelezaji
wa Sekta ya Kilimo
51. Mheshimiwa Spika, ukuaji
wa uchumi na maendeleo ya Wananchi wa Tanzania unategemea kwa kiasi kikubwa
sekta ya kilimo. Sekta hii ni muhimili wa uchumi wa Viwanda na kuchangia
kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati, kupunguza umaskini na kuongeza
uhakika wa chakula. Kwa sasa asilimia 65.5
ya Wananchi wa Tanzania wanategemea sekta ya kilimo kwa maendeleo yao ya
Kiuchumi na Kijamii.
52. Mheshimiwa Spika, Sekta
ya Kilimo inachangia sehemu kubwa ya mapato ya uendeshaji wa Mamlaka za
Serikali za Mitaa kupitia ushuru wa mazao ya kilimo na ushuru wa huduma katika
sekta ya Mifugo na Uvuvi. Mikoa na Halmashauri imeitikia mwito wa kusimamia
kilimo cha mazao makuu matano ya biashara katika maeneo yao. Mazao hayo ni
Pamba, Korosho, Kahawa, Chai na Tumbaku. Usimamizi huu utachangia ongezeko la
mavuno ya mazao hayo katika msimu wa mavuno ujao.
53. Mheshimiwa Spika, maelekezo
yametolewa kwa Wakuu wa Mikoa na
Wilaya kushirikiana pamoja na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha
wanawatafuta na kuwafikisha mbele ya vyombo vya Sheria wale wote wanaochafua
ubora wa mazao, iwe ni kuweka mawe, maji, mchanga na uchafu wowote katika
pamba, korosho au zao lingine lolote. Aidha, ni jukumu la Vyama vya Ushirika na
kila mkulima kuhakikisha mazao hayahujumiwi.
Ruzuku ya Maendeleo katika
Mamlaka za Serikali
za Mitaa
54. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeongeza fedha za ruzuku ya maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za
Mitaa kutoka shilingi bilioni 156
zilizoidhinishwa na Bunge lako Tukufu katika Mwaka wa Fedha 2016/17 hadi
shilingi bilioni 251.0 kwa Mwaka wa
Fedha 2017/18. Halmashauri zimeboresha miradi iliyopangwa kutekelezwa katika
Mwaka wa Fedha 2017/18 kwa kuchagua miradi michache yenye tija ambayo
itatekelezwa na kukamilika ili ianze kutoa huduma. Mkakati huu umesaidia
kuondoa changamoto ya kuwa na miradi viporo kila Mwaka. Asilimia 95 ya fedha
hizo zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za
afya, elimu ya msingi, elimu ya sekondari, ujenzi wa majengo ya utawala, vitega
uchumi vya kibiashara, sekta ya maji, sekta ya kilimo, mifugo na sekta ya ardhi
na maliasili. Utekelezaji wa miradi hiyo umepangwa kukamilika ifikapo Juni,
2018 ili ianze kutoa huduma. Fedha zinazobaki sawa na Asilimia 5 zimetengwa kwa ajili ya shughuli za ufuatiliaji na
tathmini ya miradi iliyopangwa.
Mradi
wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati Tanzania
55. Mheshimiwa Spika, Awamu
ya Kwanza ya utekelezaji wa Mpango wa kuboresha Miji nane (8) ya Kimkakati
ulikamilika katika Mwaka wa Fedha 2015/16. Mpango huu umeongezewa muda wa
utekelezaji kwa miaka miwili (2) kwa gharama ya shilingi bilioni 291.2. Programu itatekelezwa kwenye Majiji ya Arusha,
Mbeya, Mwanza na Tanga na Halmashauri za Manispaa za Dodoma, Kigoma Ujiji,
Ilemela na Mtwara Mikindani ili kuchochea ukuaji wa fursa mbalimbali za
kiuchumi katika Miji nchini. Hadi kufikia Januari, 2018 shilingi bilioni 21.17 zimetolewa kati ya
shilingi bilioni 81.5 zilizopangwa
katika Mwaka wa Fedha 2017/18 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Jumla ya kilometa 12.74 za barabara
zimejengwa kwa kiwango cha lami katika Halmashauri nane zinazotekeleza mradi.
Aidha, ujenzi wa nyongeza ya mashimo 6
(6 Cells) katika madampo matano ya kisasa katika Miji mitano ya Dodoma, Arusha,
Mbeya, Mtwara Mikindani na Kigoma unakamilika. Vilevile, ujenzi wa mitaro ya
maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 7.25
pamoja na uwekaji wa taa za barabarani katika barabara zilizojengwa nao pia
umekamilika.
Programu
ya Kuzijengea Uwezo Halmashauri za Miji
56. Mheshimiwa Spika,
Programu ya Kuzijengea Uwezo Halmashauri za Miji inaendelea kutekelezwa katika
Miji 18 ambayo ni Halmashauri za Manispaa za Morogoro, Tabora, Moshi,
Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Singida, Musoma, Iringa, Bukoba, Kibaha, Mpanda
na Lindi na Halmashauri za Miji ya Njombe, Babati, Geita, Korogwe na Bariadi. Kupitia
programu hii, jumla ya kilometa 64.38
za barabara zimejengwa kati ya kilometa 220
za barabara zilizopangwa kujengwa. Aidha, barabara zenye urefu wa kilometa 67.03 ziko katika hatua mbalimbali za
ujenzi.
57. Mheshimiwa Spika, Serikali
inatekeleza Programu ya Kuendeleza Miji 18 ambao unagharimu shilingi bilioni 571.2 kwa kipindi cha Miaka
mitano (5). Katika kuboresha na
kupanga Miji, uandaaji wa Mipango Kabambe ya uendelezaji wa Miji katika Miji 18
unaendelea. Hadi kufikia Januari, 2018 Mipango Kabambe ya Miji mitatu (3)
imezinduliwa, Mipango Kabambe ya Miji mitano (5) imewasilishwa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuidhinishwa na Mipango Kabambe ya
Miji saba ipo katika maandalizi. Hadi kufikia Desemba, 2017 kiasi cha shilingi bilioni 91.9 zimetolewa na kutumika kutekeleza miradi ya
ujenzi wa barabara za lami, mifereji, uwekaji wa taa za barabarani, madampo na
ununuzi wa magari ya taka ngumu.
Mradi
wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam
58. Mheshimiwa Spika, mradi
wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam umepangwa kutekelezwa kwa miaka mitano kwa
gharama ya shilingi bilioni 660. Serikali
inaendelea kutekeleza malengo ya Programu ya Kuendeleza Miundombinu katika Jiji
la Dar es Salaam ambapo jumla ya barabara zenye urefu wa kilometa 15 zimejengwa likiwemo tuta la kilometa 1.5 lenye daraja la meta
16 na makalvati kwenye bonde la mto Mzinga linalounganisha maeneo ya
Kijichi na Tuangoma. Aidha, usanifu wa miradi ya barabara zenye urefu wa kilometa 110 umekamilika. Jumla ya
shilingi bilioni 17.7 zimetumika
kutekeleza miradi hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2017/18.
59. Mheshimiwa Spika,
kupitia Programu ya Kuendeleza Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam, Serikali
inaendelea na usanifu wa mradi wa Bonde la Mto Msimbazi unaofanywa na Kampuni
mbili za COWI Tanzania Ltd na ECORYS ya nchini Netherland ili kumpata Mkandarasi wa kujenga na kuboresha
miundombinu ya bonde hilo. Kazi ya usanifu imepangwa kukamilika ifikapo Juni,
2018. Mradi huu utatekelezwa kwa mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 20 kutoka Department
for International Development (DfID) ikiwa ni mkakati wa kupunguza athari
za mazingira na mafuriko katika Bonde la Mto Msimbazi.
Mradi wa
Kuondoa Vikwazo vya Upitikaji (Improving Rural Access in Tanzania).
60. Mheshimiwa Spika, katika
Mwaka wa Fedha 2017/18, mradi wa kuondoa vikwazo uliidhinishiwa jumla ya
shilingi bilioni 10.95 kwa ajili ya
matengenezo maalum ya kilometa 122.2
kwenye Halmashauri 9 ambazo ni
Halmashauri za Wilaya za Kyerwa, Kishapu, Babati, Kondoa, Magu, Mpwapwa,
Bariadi, Kibiti na Songwe. Hadi Februari, 2018 jumla ya shilingi bilioni 4.36 zimetumika kufanya
matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa
24. Aidha, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Uingereza (DfID),
imetumia shilingi bilioni 15.74
kujenga kilometa 11.45 za barabara
na kilometa 78 zinaendelea kujengwa.
Programu ya Maboresho
ya Fedha za Umma (PFMRP V)
61.
Mheshimiwa
Spika, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa
Maendeleo imekuwa ikitekeleza Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za
Umma (PFMRP) kwa vipindi tofauti tangu mwaka 1998 ambapo PFMRP Awamu ya IV ya
utekelezaji ilikamilika Juni, 2017. Katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Programu
imefanikiwa kutekeleza mambo yafuatayo:- kuimarisha Mfumo Funganishi wa
Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Fedha (IFMS – EPICOR 9.05) ambao umefungwa
katika Halmashauri zote 185, kufanya mapitio ya Sheria Ndogo za Mamlaka za
Serikali za Mitaa ili kuzihuisha Sheria ndogo kulingana na wakati na Sheria
mama, kuandaa Mwongozo wa namna bora ya kuwatambua wafanya biashara wadogo
wadogo (Wamachinga) katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuimarisha Mfumo wa
ukusanyaji mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wa Mfumo (LGRCIS) pamoja
na ununuzi wa Mashine za Kieletroniki za kukusanya mapato (POS) kwa ajili ya
Halmashauri zenye uwezo mdogo katika ukusanyaji wa mapato.
62.
Mheshimiwa
Spika, kazi nyingine zilizotekelezwa ni pamoja na kuandaa
Mwongozo kwa lugha ya Kiswahili wa Usimamizi wa Fedha katika Mamlaka za
Serikali za Mitaa, kuanzishwa kwa mfumo wa utoaji taarifa za Fedha
zinazopekelekwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa (Fiscal Transfer Web
Portal) ambayo imeunganishwa kwenye Tovuti ya OR-TAMISEMI ili kuweka uwazi wa
taarifa hizo na kuandaa na kusambazwa kwa Miongozo ya Maeneo muhimu sita (6) ya
Usimamizi wa fedha itakayotumika kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ya Ukaguzi
wa ndani na nje, ununuzi, Mikopo na Uwekezaji, Ukusanyaji wa mapato, Mipango na
Bajeti na Taarifa za Kihasibu na za Fedha.
Huduma ya Maji na
Usafi wa Mazingira Vijijini
63.
Mheshimiwa
Spika,
OR-TAMISEMI
inaendelea kusimamia utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya
Sekta ya Maji inayotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Mwaka wa
Fedha 2015/16 hadi Mwaka 2020/21. Programu hii imelenga kuboresha huduma ya maji
na usafi wa mazingira kwa maeneo ya mijini na vijijini kwa kuboresha miundombinu,
usimamizi na uendelezaji endelevu wa rasilimali za maji.
64.
Mheshimiwa
Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Halmashauri ziliidhinishiwa
shilingi bilioni 267.3 kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maji 366.
Hadi Februari 2018, shilingi bilioni
91.08 zilipokelewa kwenye Halmashauri kwa ajili ya kutekeleza miradi
hiyo. Katika kipindi hicho miradi 71 imetekelezwa na kukamilika kwa
gharama ya shilingi bilioni 14.0. Miradi
iliyokamilika inajumuisha miradi ya mserereko 6 na miradi 43
inayoendeshwa kwa Nishati. Miradi hiyo ina jumla ya vituo 990 vya kuchotea maji ambavyo vinahudumia wananchi 247,500.
65.
Mheshimiwa
Spika, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeendelea
kuimarisha na kuunda vyombo huru vya watumiaji maji kwa ajili ya usimamizi na
uendeshaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira vijijini. Hadi Februari,
2018, jumla ya Jumuiya za Watumiaji Maji 565
zimeundwa na kufanya idadi ya Jumuiya zilizopo kuwa 2,796. Lengo la kuundwa kwa Jumuiya hizo ni kuwa na mifumo thabiti
ya kusimamia uendelevu wa miradi ya maji na usafi wa mazingira vijijini.
66.
Mheshimiwa
Spika, OR-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na
Umwagiliaji na Shirika la Maendeleo la Uingereza inatekeleza mfumo wa malipo
kwa matokeo (Payment by Results -PbR) uliozinduliwa
katika mwaka wa fedha 2016/17. Mfumo huo unahusisha utoaji wa fedha kwa
Halmashauri kulingana na ufanisi, usimamizi na uendeshaji wa vituo vya kuchotea
maji. Kwa Mwaka wa Fedha 2016/17, jumla
ya Halmashauri 74 zilikidhi vigezo
vya usimamizi wa miradi ya maji na kupata fedha shilingi bilioni 1.7. Hadi Februari, 2018 jumla ya Halmashauri 95 zimekidhi vigezo na kupewa jumla ya
shilingi bilioni 8.55 kwa ajili ya
ujenzi na ukabarati wa miundombinu ya maji katika mwaka huu wa fedha wa
2017/18. Aidha, Halmashauri zingine zilizobaki zitaendelea kujengewa uwezo ili
nazo ziweze kukidhi vigezo.
Mradi
wa Kukabiliana na Changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi
67. Mheshimiwa Spika,
Serikali kwa kushirikiana na Shirika la
Misaada la Uingereza (UKAID) kupitia Shirika lake la Maendeleo (Department for International
Development-DfID) na Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo
(International Institute for Environment and Development-IIED) na Shirika la Hakikazi Catalyst la
Arusha inatekeleza mradi wa kukabiliana
na kujenga ustahimilivu wa athari za mabadiliko ya Tabianchi. Lengo kubwa la
mradi huu ni kuhakikisha mipango ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali inafungamanishwa
na masuala ya mabadiliko ya Tabianchi ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu
ifikapo Mwaka 2030.
68. Mheshimiwa Spika, Awamu ya Kwanza ilianza kutekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2012/13 na
kuhusisha Halmashauri tatu (3) za Mkoa wa Arusha ambazo ni Halmashauri za
Wilaya za Monduli, Ngorongoro na Longido. Kupitia mradi huu
Halmashauri zinajengewa uwezo na ujenzi wa miundombinu ili kuhakikisha
ustahimilivu wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi. Jumla ya
miradi 34 imetekelezwa ambapo baadhi
ya miradi hiyo ni ujenzi wa skimu ya maji mserereko, ujenzi wa mifereji ya
kudhibiti mafuriko, ujenzi na ukarabati wa malambo na mabirika ya kunyweshea
mifugo, ujenzi wa masoko ya mifugo na ukarabati na uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Kazi nyingine zilizofanyika ni ujenzi wa maabara za mifugo, ujenzi wa maghala ya
kuhifadhia mazao na ujenzi wa matanki ya kuhifadhia maji. Miradi hiyo ambayo
inanufaisha wananchi 436,569
imegharimu shilingi bilioni 2.0 hadi
kukamilika.
IV.
TAASISI
ZILIZO CHINI YA OFISI YA RAIS-TAMISEMI
Tume
ya Utumishi wa Walimu
69. Mheshimiwa Spika,
hadi kufikia Desemba, 2017, walimu 4,054
walisajiliwa, walimu 2,173 walithibitishwa
kazini na walimu 1,084 wamewezeshwa
kukamilisha taratibu za kustaafu. Aidha, mashauri ya nidhamu 250 yalipokelewa na mashauri 156 yamefanyiwa kazi na kutolewa uamuzi
sawa na asilimia 60.2.
70. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2017 walimu 869 wamefunguliwa mashtaka ya nidhamu. Mashauri
401 yapo kwenye hatua mbalimbali ya
uamuzi kwa mujibu wa Sheria.
Wakala wa Barabara
Mijini na Vijijini (TARURA)
71.
Mheshimiwa
Spika, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tanzania Rural and Urban Roads
Agency–TARURA) umeanzishwa rasmi kwa Sheria ya Wakala
za Serikali Sura 245 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 211 la tarehe
12/05/2017. Wakala ulianza kutekeleza majukumu yake Julai, 2017. Wakala unasimamia ujenzi wa barabara na madaraja, ukarabati
na matengenezo ya mtandao wa barabara za Halmashauri zenye urefu wa kilometa 108,946.2 vijijini na mijini. Kati ya
barabara hizo, kilometa 56,000
zinafanyiwa mchakato wa kuzihakiki ili hatimaye ziweze kutangazwa kwenye Gazeti
la Serikali ili zitambulike ki-sheria na kilometa 52,946.2 tayari zinatambulika na zimeshatangazwa kwenye Gazeti la
Serikali. Lengo la Serikali kuanzisha TARURA ni kuleta
ufanisi katika ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara ambazo awali
zilikuwa zinasimamiwa na Halmashauri.
72.
Mheshimiwa Spika, TARURA inatekeleza majukumu yake kupitia Fedha za
Mfuko wa Barabara ambapo
katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Wakala umeidhinishiwa shilingi bilioni 230.8 kwa ajili ya matengenezo ya
barabara kilomita 34,024. Hadi Februari, 2018, TARURA
imepokea shilingi bilioni 98.5 ambazo zimetumika kutengeneza barabara
zenye urefu wa kilometa 4,183.31, ujenzi wa madaraja 35,
Makalavati makubwa 43, Drift
4, na Makalavati madogo 364. Wakala unategemea kuongeza
mtandao wa barabara za lami katika Halmashauri kutoka kilometa 1,585.51 zilizopo sasa hadi kilometa 2,059.83 ifikapo Mwaka 2020.
Shirika
la Elimu Kibaha
73. Mheshimiwa Spika, Shirika
la Elimu Kibaha linaendelea kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwake ambayo ni
kupambana na maadui watatu wa maendeleo yaani Ujinga, Umaskini na Maradhi. Hadi Februari, 2018, Shirika limetoa huduma kwa wagonjwa 33,652 wakiwemo wagonjwa 2,806
waliolazwa. Pia Hospitali ilihudumia majeruhi wa ajali za barabarani 352, na majeruhi wasio wa ajali za
barabarani wapatao 129. Shirika limeanzisha
huduma ya matibabu ya Mdomo Sungura “Cleft
Lip and Palate” ambapo wagonjwa 22
wameshanufaika na huduma hii. Huduma hii inagharamiwa na Shirika lisilokuwa la
kiserikali lijulikanalo kama SmileTrain
la nchini Marekani.
Vilevile, kupitia Chuo cha Afya na Sayansi
Shirikishi Kibaha na Hospitali ya Tumbi,
Shirika liliendelea kutoa mafunzo kwa kada za maafisa tabibu, Afya ya Jamii, uuguzi
na ukunga kwa ngazi ya stashahada, na wauguzi wasaidizi kwa ngazi ya cheti
ambapo kwa sasa Chuo kinao wanafunzi 265
wanaoendelea na masomo.
74. Mheshimiwa Spika, Shirika limefanikiwa kutoa elimu na malezi kwa
wanafunzi 2,614. Wanafunzi 904 walipata elimu ya msingi na
wanafunzi 1,710 walipata elimu ya
sekondari. Kwa upande wa maktaba, wanafunzi pamoja na wadau wengine 20,499 walipata huduma za kujisomea
vitabu na majarida mbalimbali. Aidha, mafunzo ya vitendo
yanaendelea kutolewa na Shirika kupitia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi chenye wanachuo 279.
Mafunzo yanayotolewa ni Kilimo, Mifugo, Uashi, Ufundi Bomba, Useremala,
Ushonaji, Upishi, Ufundi wa Magari, Uundaji na Ufuaji vyuma
na Umeme wa majumbani.
Chuo
cha Serikali za Mitaa - Hombolo
75.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2017/18, Chuo
kimedahili jumla ya wanafunzi 3,485 ambapo
wanafunzi wa kike ni 2,067 na wa kiume
1,178. Aidha, Chuo kiliendesha
mafunzo mbalimbali ya muda mfupi katika Tawala za Mikoa, Halmashauri pamoja na
Taasisi na Mashirika ya Umma. Vilevile, Chuo kimetoa ushauri wa kitaalam kwenye
maeneo mbalimbali ya kujenga uwezo hususan utoaji taarifa, tathmini na upimaji.
Bodi ya Mikopo ya
Serikali za Mitaa
76.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18,
Bodi ilikadiria kukusanya mapato ya ndani ya shilingi bilioni 5.71. Hadi Februari, 2018 Bodi imefanikiwa kukusanya
shilingi bilioni 1.11 sawa na asilimia 20 ya lengo. Aidha, Bodi
imefanikiwa kutoa mkopo wa shilingi milioni
450.00 katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo.
Mfuko wa Pensheni wa
Serikali za Mitaa
77. Mheshimiwa
Spika, katika Mwaka wa Fedha
2017/18, Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa ulipanga kukusanya mapato ya
kiasi cha shilingi bilioni 611.67.
Hata hivyo, makisio hayo yalifanyiwa marekebisho baada ya miezi sita na kuwa
shilingi bilioni 543.34 kutokana na
kuondolewa wafanyakazi wasio na sifa katika utumishi wa umma. Kiasi kilichopungua
ni shilingi bilioni 68.33. Hadi
Desemba, 2017 makusanyo halisi yamefikia shilingi bilioni 254.65 sawa na asilimia
41.6 ya lengo. Thamani ya Mfuko
inatarajiwa kukua kwa asilimia 16
kutoka shilingi trilioni 1.75 ya
Mwaka wa Fedha 2017/18 hadi shilingi
trilioni 2.4 ifikapo Juni, 2019.
Shirika
la Masoko Kariakoo
78. Mheshimiwa Spika, Shirika la Masoko
Kariakoo lilianzishwa kwa ajili ya kusimamia na kuendesha masoko ya mazao ya
chakula, zana za kilimo na pembejeo za kilimo katika Jiji la Dar es Salaam. Katika
Mwaka wa Fedha 2017/18, Shirika lilikadiria kukusanya mapato ya ndani kiasi cha
shilingi bilioni 3.6 kutokana na
ushuru wa mazao, kodi ya pango na ada ya kutumia soko. Hadi Februari, 2018
Shirika limekusanya shilingi bilioni 1.7
sawa na asilimia 47 ya lengo.
79. Mheshimiwa Spika, fedha hizo zimetumika kulipa mishahara ya watumishi wa Shirika,
uendeshaji wa biashara, kulipa kodi ya mapato, ujenzi wa maduka 94, utatuzi wa mgogoro wa viwanja vya
Shirika Mbezi Beach, ukarabati wa nyumba za Shirika na barabara kuzunguka
Shirika, kumaliza mashauri 16
yaliyokuwa Mahakamani, kufunga mitambo ya CCTV na kulipa madeni ya Shirika
kiasi cha shilingi milioni 176.7.
Wakala wa
Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam
80.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Wakala umefanikiwa kufanya
maandalizi ya Awamu ya Pili na Tatu ya ujenzi wa miundombinu ya DART ambapo
taratibu za ununuzi zimefanyika ili kuwapata Wakandarasi wa kujenga miundombinu
hiyo. Wakala umeendelea kuimarisha usimamizi na usalama wa miundombinu ya mradi
katika vituo vikuu (5), vituo vidogo ishirini na saba (27),
madaraja ya watembea kwa miguu matatu (3) pamoja na karakana. Aidha, umesimikwa
mfumo wa kielektroniki wa masjala pamoja na mfumo wa usimamizi na udhibiti wa
fedha – Epicor 10.1 kwa lengo la kuboresha utendaji, ufanisi na uwajibikaji.
81.
Mheshimiwa
Spika, kazi nyingine zilizofanyika ni kuendelea na ukamilishaji wa taratibu za ununuzi wa
kumpata mtoa Huduma wa pili (SP2), mafunzo ya viwango vya ubora wa Kimataifa
kwa watumishi wa Wakala; ujenzi wa uzio kuzunguka vituo vikuu vitatu (3) vya
Ubungo, Kivukoni na Morocco ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya
nauli na usalama wa abiria ambao umepangwa kukamilika Juni 2018. Aidha, Wakala
umefunga Kituo cha Mawasiliano cha muda ili kuboresha ufuatiliaji na tathmini
ya mwenendo wa mabasi katika mfumo wa DART.
82.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi wa DART umeliwezesha Jiji la Dar
es Salaam kupewa tuzo ya Usafiri
Endelevu na kuwa Jiji Bora duniani (Sustainable Transport Award) kwa Mwaka
2018. Vigezo vilivyotumika kupata
tuzo hiyo ni pamoja na kupanga mradi kwa ufanisi mkubwa, kujenga miundombinu
mizuri, kuzingatiwa kwa mahitaji ya watumiaji mbalimbali na kutoa elimu ya mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka kwa
watumiaji kupitia Mpango Mkakati wa Wakala. Kutokana na ufanisi wa utekelezaji
wa mradi wa DART, Nchi mbali mbali zimekuja Tanzania kujifunza mafanikio na changamoto za
mradi huu zikiwemo nchi za Zambia, Zimbabwe, Uganda, Kenya, Ethiopia, Senegal
na Rwanda. Aidha, tuzo hiyo
imeipa Tanzania heshima ya kuandaa Mkutano wa Kimataifa wa Masuala ya
Usafirishaji mijini utakaofanyika Juni 2018 hivyo kufungua fursa za kiuchumi,
uwekezaji na utalii.
83.
Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuongezeka kwa
idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa DART kutoka wastani wa abiria 76,000 kwa siku Mei, 2016 mradi
ulipoanza kutekelezwa hadi abiria 209,000
kwa siku Machi, 2018. Ongezeko
la watumiaji wa DART limeongeza mapato kutoka wastani wa shilingi milioni 8.13 Mei, 2016 hadi wastani wa shilingi
bilioni 3.6 kwa Mwezi Agosti, 2017.
Vilevile, muda wa safari kutoka Kimara hadi Kivukoni kwa usafiri wa mabasi ya kawaida umepungua kutoka saa 2 za awali hadi wastani wa dakika 40 baada ya mabasi ya DART kuanza kufanya kazi na
gharama za nauli zimepungua kutoka takriban shilingi 20,000 kwa gari binafsi hadi shilingi 1,300 kwa siku. Aidha, msongamano wa magari barabarani umepungua
hususan katika barabara ya Morogoro.
84.
Mheshimiwa Spika, mradi umetoa fursa za ajira kwa zaidi ya watu 1,000 pamoja na watoa huduma wakiwemo watumishi wa UDA-RT, Maxcom,
kampuni ya ulinzi, usafi na maegesho ya magari katika eneo la Kimara. Aidha,
matumizi ya teknolojia yakiwemo matumizi ya kadi badala ya fedha taslimu
yamerahisisha abiria kuingia na kutoka kwenye vituo na kudhibiti upotevu wa
mapato.
V.
MPANGO
NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA KAWAIDA NA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2018/19
85. Mheshimiwa
Spika, maandalizi ya Mpango na Bajeti ya OR-TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha
2018/19 yamezingatia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19, azma ya kufikia
Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka
2015, Agenda ya Dunia ya Malengo ya
Maendeleo Endelevu 2030, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano
2016/17-2020/21, Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha
2018/19, maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kuzindua Bunge Novemba, 2015 na
maagizo mbalimbali ya Viongozi.
86.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19, OR -TAMISEMI,
itaendelea kutekeleza vipaumbele mbalimbali, kama ifuatavyo:-
i)
Kuimarisha amani na utulivu nchini,
kusimamia shughuli za utawala bora, kukuza demokrasia, ushirikishwaji wa
wananchi na Ugatuaji wa Madaraka kwa
Umma (D by D);
ii)
Kusimamia matumizi ya rasilimali katika
ngazi zote za Ofisi ya Rais – TAMISEMI;
iii)
Kusimamia utekelezaji wa majukumu ya
msingi (Core Business) ya kila Taasisi yaliyoainishwa kwenye Mipango Mikakati
yao;
iv)
Kuchochea na kuhimiza ukuaji wa uchumi
kwa maendeleo ya Wananchi na Taifa kwa ujumla kwa kuiwezesha Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa kuweka mazingira mazuri ya Biashara na Uwekezaji hasa
katika kilimo na viwanda;
v)
Kusimamia utekelezaji wa majukumu ya
msingi ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI ikiwa ni pamoja na kufanya ufuatiliaji wa
utekelezaji wa shughuli za Serikali, programu na miradi katika ngazi ya Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
vi)
Kuratibu shughuli za usimamizi na
uendeshaji wa elimu, afya, maji, kilimo, mifugo, uvuvi na sekta nyingine;
vii)
Kuratibu shughuli za kuboresha
mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na kuendeleza rasilimali watu kwa
kuwaongezea ujuzi na vitendea kazi;
viii)
Kusimamia, kuratibu na kuwezesha
utekelezaji wa Taasisi, programu na miradi iliyo chini ya Ofisi ya Rais –
TAMISEMI; na;
ix)
Kusimamia maandalizi ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa.
Tawala za Mikoa
87. Mheshimiwa
Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19, Tawala za Mikoa
zitatekeleza majukumu yafuatayo:-
i)
Kudumisha amani, utulivu na usalama;
ii)
Kuendeleza ujenzi, ukarabati na
ukamilishaji wa Ofisi na Makazi ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa,
Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Wilaya
na Maafisa Tarafa;
iii)
Kuendesha mikutano ya Kisheria ya
Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC) ili kuimarisha utawala bora na
uwajibikaji katika ngazi zote;
iv)
Kuratibu maandalizi ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa utakaofanyika Mwaka 2019;
v)
Kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji
wa Sera ya Ugatuaji wa Madaraka kwa Wananchi na Sera nyingine za kisekta ili
kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi;
vi)
Kuratibu masuala mtambuka
yanayotekelezwa kwenye Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
vii)
Kushughulikia migogoro inayotokana na matumizi ya ardhi na
mipaka kwenye Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
viii)
Kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi
katika sekta mbalimbali za uchumi katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
ix)
Kuandaa Mipango Mikakati ya Mikoa na
Serikali za Mitaa kwa Kuzingatia Mpango wa Pili wa Maendeleo na Ilani ya
Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya
Mwaka 2015;
x)
Kuanzisha na kurasimisha utengaji wa
maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya viwanda, kilimo, ufugaji, makazi, hifadhi za
wanyamapori, misitu na vyanzo vya maji;
xi)
Kusimamia rasilimali watu, fedha na
vifaa katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na
xii)
Kuanzisha na kusimamia madawati ya
kuratibu malalamiko kuhusu huduma zinazotolewa kwenye Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa.
Mamlaka za Serikali za Mitaa
88. Mheshimiwa
Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19, Mamlaka za Serikali
za Mitaa nchini zitatekeleza majukumu yafuatayo:-
i)
Kujenga na
kukarabati miundombinu ya kijamii na kiuchumi hususan katika sekta za elimu,
maji, afya, kilimo, mifugo, uvuvi, barabara na sekta nyingine kwa kushirikisha
nguvu ya wananchi;
ii)
Kuendesha Mikutano
ya Kisheria ngazi ya Halmashauri, Kata, Vijiji na Mitaa ili kuimarisha masuala
ya utawala bora na uwajibikaji;
iii)
Kuimarisha
matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato;
iv)
Kubuni na kusimamia utekelezaji wa miradi ya
kimkakati itakayosaidia kuongeza mapato ya Halmashauri;
v)
Kuwezesha
Vikundi vya Vijana na Wanawake kupata mikopo kupitia Mifuko ya Maendeleo ya
Vijana na Wanawake;
vi)
Ukamilishaji wa
miradi viporo, majengo ya Ofisi na makazi ya Viongozi na watumishi hasa katika
maeneo mapya ya utawala;
vii) Kuanza maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
utakaofanyika Mwaka 2019;
viii) Kusimamia mpango wa utoaji
wa elimumsingi bila malipo katika shule za Msingi na Sekondari;
ix)
Kutenga maeneo ya
uwekezaji kwa ajili ya uwekezaji na maendeleo ya viwanda vidogo, vya kati na
viwanda vikubwa;
x)
Utunzaji wa mazingira
na hifadhi ya vyanzo vya maji; na
xi)
Kuimarisha
uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara pamoja na kuanzisha mazao mbadala
ili kupunguza hasara pamoja na kuwezesha viwanda vya usindikaji.
VI.
MALENGO
YA TAASISI ZILIZO CHINI YA OR - TAMISEMI
KWA MWAKA WA FEDHA 2018/19
Wakala wa Mabasi
Yaendayo Haraka (DART)
89. Mheshimiwa
Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19 Wakala wa Mabasi
Yaendayo Haraka-Dar es Salaam umepanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-
i)
Kuanza Awamu ya Pili ya ujenzi wa
miundombinu ya DART utakaohusisha barabara za Kilwa,
Kawawa, Sokoine, Gerezani, Bandari na Chang’ombe zenye urefu wa kilometa 20.3. Ujenzi umepangwa kuanza
Desemba, 2018 baada ya kumpata Mkandarasi. Mradi huu utatekelezwa kupitia mkopo
wa Dola za Marekani milioni 141.71
kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika;
ii)
Kuanza Awamu ya Tatu ya
ujenzi wa miundombinu ya DART utakaohusisha barabara za Nyerere, Uhuru, Bibi
Titi, Azikiwe, Shaurimoyo, Lindi na Maktaba zenye urefu wa kilometa 23.6 kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 148.2 kutoka Benki ya Dunia. Kazi ya ujenzi imepangwa
kuanza Desemba, 2018;
iii)
Kuanza usanifu wa Awamu ya Nne ya
ujenzi wa miundombinu ya DART kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 97.9 kutoka Benki ya Dunia. Usanifu
utahusisha barabara za Sam Nujoma, Bagamoyo, Bibi Titi na Ali Hassan Mwinyi
zenye urefu wa kilometa 25.9;
iv)
Ujenzi wa Maegesho katika maeneo ya
mfumo wa Wakala;
v)
Kukamilisha taratibu za upatikanaji wa
Mtoa Huduma wa Pili (SP2), Mkusanyaji Nauli, Msimamizi wa Fedha pamoja Mshauri
Mwelekezi’’ Transaction Advisor’’ kwa
ajili ya awamu ya tatu;
vi)
Kuhakikisha upatikanaji wa Mfumo wa ´´Intelligent
Transport System (ITS)`` wa Serikali na kuwajengea uwezo watumiaji wake;
vii)
Kutekeleza Mpango Kazi wa Fidia ya
Makazi kwa waathirika wa mradi wa awamu ya
pili na tatu ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa ajili ya mradi wa awamu ya 2,
3 na 4;
viii)
Uboreshaji na ujenzi wa vituo mlisho (bus stops); maeneo ya kugeuzia mabasi (bus turning facilities) pamoja na kuweka
mipaka karakana ya Jangwani; na
ix)
Kuimarisha mfumo wa TEHAMA wa Mabasi
Yaendayo Haraka Dar es Salaam.
Tume
ya Utumishi wa Walimu
90. Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka wa Fedha 2018/19, Tume ya Utumishi wa Walimu imepanga kutekeleza
kazi zifuatazo:-
i)
Kuwezesha Makao Makuu
na Wilaya 139 kufanya vikao vya
Kisheria vya kusikiliza mashauri ya nidhamu na kuthibitisha
walimu kazini;
ii)
Kuandaa mfumo wa kielektroniki wa utunzaji
wa taarifa
za Walimu;
iii)
Kuwajengea uwezo
Watumishi wa Tume ili kutekeleza Majukumu yao ipasavyo;
iv)
Kuratibu na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa
majukumu ya Tume katika Wilaya 139; na
v)
Kuhakikisha kunakuwa na uwiano sawa wa Walimu kwenye
Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Shirika la Elimu
Kibaha
91. Mheshimiwa
Spika,
katika
Mwaka wa Fedha 2018/19, Shirika la Elimu Kibaha limepanga
kutekeleza majukumu yafuatayo:-
i)
Kuendelea kutoa huduma za afya za
kinga na tiba katika hospitali ya Tumbi;
ii)
Kuendelea kutoa elimu ya Afya ya
mazingira, uuguzi na utabibu kwa wanafunzi 265
katika Chuo cha Sayansi na Tiba Shirikishi Kibaha;
iii)
Kuendelea kutoa elimu na malezi bora
kwa wanafunzi 1,710 wa Sekondari na
Wanafunzi 904 wa shule za msingi;
iv)
Kuendelea kutoa huduma za maendeleo ya
jamii ili kuiwezesha Taasisi kuondokana na umaskini kwa kutoa mafunzo ya
ufundi, ujasiriamali, kilimo na mifugo
kupitia Chuo cha Maendeleo ya wananchi Kibaha na shamba darasa la mifugo
na mazao;
v)
Kuongeza uzalishaji wa maji tiba kwa
ajili ya matumizi ya hospitali;
vi)
Kuboresha miundombinu ya Chuo cha
Maendeleo ya Wananchi na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi ili viweze kutoa
huduma bora zaidi kwa jamii kulingana na uhitaji uliopo;
vii)
Kujenga miundombinu ya shule ikiwemo
maabara katika shule ya sekondari ya wasichana ya Kibaha na vyoo vya nje katika
shule ya sekondari Kibaha; na
viii)
Kukarabati mabanda ya mifugo kwa ajili
ya kuongeza uzalishaji na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa vitendo katika
shamba darasa la mifugo na mazao.
Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA)
92. Mheshimiwa Spika, katika
Mwaka wa Fedha 2018/19, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) umepanga
kufanya kazi zifuatazo:-
i)
Matengenezo ya kawaida ya barabara za changarawe na udongo kilometa 13,163.89;
ii)
Matengenezo ya sehemu korofi kilometa 6,201.22;
iii)
Matengenezo maalum ya barabara kilometa 3,925.94;
iv)
Ukarabati wa madaraja 117, mifereji urefu wa meta 67,844 na makalvati 1,881;
v)
Matengenezo ya kawaida kwenye barabara
za lami kilometa 54.72 na ujenzi wa
kilometa 34.2 kwa kiwango cha lami;
vi)
Kujenga uwezo wa Wahandisi katika
maeneo ya usanifu na usimamizi wa Mikataba; na
vii)
Kuimarisha maabara iliyopo pamoja na kununua
vifaa vya upimaji wa kazi za barabara.
Chuo cha Serikali za
Mitaa - Hombolo
93. Mheshimiwa
Spika,
katika
Mwaka wa Fedha 2018/19, Chuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo kimepanga kutekeleza
majukumu yafuatayo:-
i)
Kudahili wanafunzi wapya 2,500;
ii)
Kufanya shughuli za utafiti katika maeneo ya mifumo,
uongozi na usimamizi wa rasilimali fedha na watu katika Mamlaka za Serikali za
Mitaa;
iii)
Ununuzi wa vitabu nakala 500 na kompyuta 25 kwa
ajili ya Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA);
iv)
Kuajiri watumishi wapya 72; na
v)
Kukusanya mapato ya ndani kupitia vyanzo vilivyopo.
Bodi
ya Mikopo ya Serikali za Mitaa
94.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19,
Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa itatekeleza majukumu yafuatayo:-
i)
Kutoa mikopo kwenye Halmashauri;
ii)
Kufanya
ufuatiliaji wa uwasilishaji wa marejesho ya mikopo na michango kutoka kwenye
Halmashauri zinazodaiwa kwa lengo la kuongeza mtaji wa Bodi;
iii)
Kubuni vyanzo vipya vya mapato;
iv)
Kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ili waweze
kufahamu majukumu ya Bodi na huduma zinazotolewa;
v)
Kuboresha muundo wa Bodi ili iweze kutekeleza
majukumu yake ya kutoa mikopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ufanisi
zaidi; na
vi)
Kuandaa mwongozo wa kuboresha utoaji wa mikopo kwa
vikundi mbalimbali kupitia Mfuko wa Wanawake na Vijana.
Mfuko wa Pensheni wa
Serikali za Mitaa
95. Mheshimiwa
Spika, katika Mwaka wa Fedha 2018/19, Mfuko wa Pensheni wa Serikali za
Mitaa umepanga kufanya shughuli
zifuatazo:-
(i)
Kuandikisha wanachama wapya 21,128;
(ii)
Kuendelea kukusanya michango ya
wanachama;
(iii)
Kukusanya mapato kutokana na uwekezaji;
(iv)
Kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu ya Mfuko;
(v)
Kufanya uwekezaji katika kiwanda cha Nyama cha Nguru Hills Ranch;
(vi)
Kuanzisha Ofisi Ndogo za uratibu katika Mikoa ya Tabora na Kagera;
(vii)
Kiwanda cha kuchakata Tangawizi Same; na
(viii)
Kiwanda cha maturubai Morogoro, sekta ya mafuta na gesi na viwanda
vingine kwa kushirikiana na Mifuko mingine ya Hifadhi ya Jamii.
Shirika la Masoko Kariakoo
96. Mheshimiwa
Spika, katika Mwaka wa Fedha
2018/19, Shirika la Masoko Kariakoo litatekeleza majukumu yafuatayo:-
i)
Kufanya marekebisho
ya Sheria Na. 36 ya Mwaka 1974 iliyoanzisha Shirika;
ii)
Kufanya
shughuli za uwekezaji katika viwanja vinavyomilikiwa na Shirika ambavyo viko
Mbezi Beach, Tabata Bima, Mbezi Makonde na soko dogo lililopo katikati ya Jiji
la Dar es Salaam; na
iii)
Kufunga
mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato (Local Government Revenue Collection
Information System – LGRCIS) ili kuongeza mapato ya Shirika.
MALENGO MAHSUSI KWA MWAKA WA FEDHA 2018/19
97. Mheshimiwa
Spika, katika Mwaka wa Fedha
2018/19, OR-TAMISEMI itatekeleza kazi maalum zifuatazo:-
i)
Ujenzi wa Hospitali 67 za Halmashauri
katika Halmashauri 67 ambazo hazina
Hospitali hizo (kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 6);
ii)
Maandalizi
ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Mwaka 2019;
iii)
Kutekeleza
miradi ya kimkakati katika Halmashauri 21
zilizokidhi vigezo kwa ajili ya kuongeza mapato ya Halmashauri;
iv)
Ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Halmashauri 22 ambazo hazina Ofisi (kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 6);
v)
Ununuzi wa
boti saba (7) kwa ajili ya kutatua
changamoto za usafiri majini katika Halmashauri za Wilaya za Ludewa, Kibiti,
Rufiji, Mafia, Ukerewe, Kigoma na Nyasa (kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 6);
vi)
Ujenzi wa
barabara zenye urefu wa kilometa 85
kwa kiwango cha lami kupitia Mradi wa Kuendeleza Miundombinu katika Jiji la Dar
es Salaam ili kupunguza msongamano wa magari;
vii)
Ujenzi wa kilometa 80.96 za lami pamoja na ujenzi
wa mitaro mikubwa ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 16.47, ujenzi wa stendi ya mabasi Mkoani Dodoma na ununuzi
wa vifaa vya kukusanyia taka katika Halmashauri saba za Manispaa kupitia Mradi
wa Miji ya Kimkakati (TSCP);
viii)
Ujenzi wa
barabara zenye urefu wa kilometa 220
kupitia Programu ya Kuimarisha Miji katika Halmashauri za Manispaa na Miji 18 pamoja na kuweka taa za barabarani kwenye
barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami;
ix)
Kuratibu
ujenzi wa viwanda 100 kwa kila Mkoa katika
Mikoa yote 26;
x)
Kutenga ekari 228,543 kwa kila Mkoa katika
Mikoa yote 26 kwa ajili ya uwekezaji
wa viwanda vidogo, kati na vikubwa; na
xi)
Kuondoa
riba kwenye mikopo kwa vikundi vya Vijana na Wanawake kwa fedha inayotokana na
asilimia 10 ya mapato ya ndani katika Halmashauri.
Shukrani
98. Mheshimiwa Spika, naomba
kuhitimisha hotuba yangu kwa kukushukuru tena wewe Mheshimiwa Spika, Naibu
Spika, Wenyeviti na Waheshimiwa Wabunge wote. Kipekee niishukuru tena Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa. Nichukue fursa hii kuwashukuru
wadau wetu wa maendeleo wakiwemo Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB), Shirika la Maendeleo la Uingereza (DfID), Jumuiya ya Nchi za
Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Shirika la Maendeleo la
Canada (CIDA), UNFPA, UN-Habitat, Shirika la Maendeleo ya Ubelgiji (BTC),
Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Shirika la Maendeleo la Marekani
(USAID), Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA), UNICEF, UNDP, pamoja na nchi
zote zinazochangia kupitia Mfuko wa Pamoja wa Kusaidia Bajeti ya Serikali.
Mafanikio katika utekelezaji wa
majukumu ya OR-TAMISEMI yamepatikana kutokana na ushirikiano mzuri wa Wadau wa
Maendeleo ambao waliendelea kushirikiana katika utekelezaji wa Programu na
Miradi mbalimbali katika Sekta za afya, elimu, maji, barabara, fedha, kilimo na
maboresho ya mfumo wa Serikali za Mitaa. OR-TAMISEMI itaendelea kushirikiana na
Wadau wote wa maendeleo wa ndani na nje ili kutimiza azma ya kutoa huduma bora
kwa wananchi kupitia miradi inayotekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele vya
wananchi wenyewe.
99. Mheshimiwa Spika,
naomba kutambua kazi kubwa inayofanywa na Viongozi wenzangu katika OR-TAMISEMI nikianzia
na Mheshimiwa Joseph George Kakunda (Mb.), Naibu Waziri Ofisi ya Rais –TAMISEMI
anayeshughulikia masuala ya huduma za elimu, maji na utawala, Mheshimiwa Josephat
Sinkamba Kandege (Mb.), Naibu Waziri anayeshughulikia huduma za afya,
miundombinu na uwekezaji, Mhandisi Mussa I. Iyombe, Katibu Mkuu, Bw. Tixon T.
Nzunda, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Elimu, na Dkt. Zainab A.S. Chaula, Naibu
Katibu Mkuu anayesimamia Afya, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu
wa Wilaya, Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri na Wakurugenzi wa Halmashauri kwa
ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, ninawashukuru Viongozi
wa Taasisi zilizo chini ya OR-TAMISEMI na watumishi wa OR-TAMISEMI katika ngazi
zote kwa utekelezaji makini wa majukumu yao katika kuboresha huduma kwa
wananchi.
100. Mheshimiwa Spika, kipekee
napenda kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe kwa kuendelea kuwa
wavumilivu mara zote nilipokuwa mbali nao kwa majukumu ya Kitaifa. Naahidi
kuendelea kuwatumikia kwa moyo wangu wote.
Aidha, naishukuru familia yangu kwa kuendelea kunitia moyo katika
utekelezaji wa majukumu haya ya kuwatumikia wananchi.
VII.
MAOMBI YA FEDHA KWA KAZI ZILIZOPANGWA KUFANYIKA KATIKA
MWAKA WA FEDHA 2018/19
Maduhuli
na Makusanyo ya Mapato ya Ndani
101. Mheshimiwa Spika, katika
Mwaka wa Fedha 2018/19, OR - TAMISEMI, Taasisi zilizo chini yake, Mikoa 26 na Halmashauri
185 inaomba idhini ya kukusanya maduhuli na mapato ya ndani jumla ya shilingi
Bilioni Mia Saba Hamsini na Nane,
Milioni Mia Tatu Sitini na Mbili, Mia Saba Kumi na Moja Elfu, Mia Saba Tisini na
Tisa (shilingi 758,362,711,799.00). Makusanyo hayo yatatokana na mauzo ya
vifaa chakavu, nyaraka za zabuni, faini mbalimbali, ada za wanafunzi, marejesho
ya masurufu na mishahara na kodi na ushuru mbalimbali unaotozwa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa kulingana na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290.
Mchanganuo wa makusanyo ya mapato hayo ni kama ifuatavyo:-
Mchanganuo
wa Maduhuli na Makusanyo kwa Mwaka wa Fedha 2018/19
Na.
|
OFISI/TAASISI
|
MAKADIRIO
|
1.
|
OR – TAMISEMI
|
20,000,000.00
|
2.
|
Taasisi
|
22,623,519,091.00
|
3.
|
Mikoa
|
130,563,708.00
|
4.
|
Halmashauri
|
735,588,629,000.00
|
JUMLA
|
758,362,711,799.00
|
102. Mheshimiwa
Spika, sasa naomba Bunge lako
Tukufu likubali kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha
2018/19 jumla ya shilingi Trilioni Sita,
Bilioni Mia Tano Themanini na Sita, Milioni Mia Tisa Kumi na tano, Mia Saba
Hamsini na tatu Elfu, Mia Saba Thelathini na Tatu (Shilingi 6,586,915,753,733.00)
kwa ajili ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI fungu Na. 56, Tume ya Utumishi wa Walimu
fungu Na. 02 na mafungu 26 ya Mikoa yanayojumuisha Halmashauri 185. Mchanganuo wa fedha zinazoombwa kwa Mwaka wa
Fedha 2018/19 ni kama ifuatavyo:-
Muhtasari
wa Fedha zinazoombwa kwa Mwaka wa Fedha 2018/19
AINA YA MATUMIZI
|
FEDHA ZINAZOOMBWA
|
OR-TAMISEMI
|
|
A) Mishahara
|
|
Makao Makuu
|
8,736,397,905
|
Taasisi
|
14,916,444,000
|
Jumla Ndogo Mishahara
|
23,652,841,905
|
B) Matumizi Mengineyo
|
|
Makao Makuu
|
17,896,530,002
|
Taasisi
|
1,318,870,806
|
Jumla Ndogo Matumizi Mengineyo
|
19,215,400,808
|
Jumla ya Matumizi ya Kawaida (A+B)
|
42,868,242,713
|
TUME YA UTUMISHI WA WALIMU
|
|
Mishahara
|
7,893,115,025
|
Matumizi Mengineyo
|
4,622,145,495
|
Jumla ya Matumizi ya Kawaida (TSC)
|
12,515,260,520
|
MIKOA NA HALMASHAURI
|
|
MIKOA:
|
|
Mishahara
|
159,941,766,000
|
Matumizi Mengineyo
|
45,219,821,000
|
Jumla Matumizi ya Kawaida
|
205,161,587,000
|
HALMASHAURI:
|
|
Mishahara
|
3,942,713,089,000
|
Matumizi Mengineyo (Ruzuku SK)
|
190,390,615,000
|
Matumizi Mengineyo (Own source)
|
389,862,000,000
|
Jumla ya Matumizi ya Kawaida
|
4,522,965,704,000
|
MIRADI YA MAENDELEO
|
|
OR-TAMISEMI
|
|
Fedha za Ndani
|
283,642,430,000
|
Fedha za Nje
|
61,471,111,000
|
Jumla OR-TAMISEMI
|
345,113,541,000
|
MIKOA
|
|
Fedha za Ndani
|
80,120,000,000
|
Fedha za Nje
|
13,064,414,000
|
Jumla Mikoa
|
93,184,414,000
|
HALMASHAURI
|
|
Fedha za Ndani (SK)
|
566,773,370,500
|
Fedha za Ndani (MH)
|
345,726,629,000
|
Jumla Ndogo
|
912,499,999,500
|
Fedha za Nje
|
452,607,005,000
|
Jumla Maendeleo Halmashauri
|
1,365,107,004,500
|
Jumla Maendeleo Mikoa na Halmashauri
|
1,458,291,418,500
|
Jumla Miradi ya Maendeleo
|
1,803,404,959,500
|
JUMLA KUU
|
6,586,915,753,733
|
103. Mheshimiwa Spika, pamoja
na hotuba hii yapo majedwali ambayo yanafafanua kwa kina makadirio ya mapato na
matumizi ya fedha ya OR-TAMISEMI, Taasisi, Mikoa na Halmashauri.
104. Mheshimiwa Spika, hotuba
hii inapatikana pia kwenye Tovuti ya OR-TAMISEMI ambayo ni www.tamisemi.go.tz
105. Mheshimiwa Spika, naomba
kutoa hoja.
SOMA HAPA HOTUBA YA WAZIRI WA TAMISEMI SELEMANI SAIDI JAFO , ALIYOWASILISHA BUNGENI MAPITIO, MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 11, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment