NAIBU Rais William Ruto
amesema serikali imeanzisha mpango wa kuifanya elimu ya kiufundi
(Technical Vocational Education and Training-TVET) kuwa ya kuvutia kote nchini.
Alisema elimu ya
kiufundi sio ya wale waliogura shule lakini ni ya wanafunzi waliokirimiwa
talanta ambazo zinaweza kuwawezesha kufaulu maishani.
Akiongea afisini mwake,
jumba la Harambee Annex, alipokutana na maafia wakuu wa Wizara ya Elimu na
Fedha, Naibu Rais alisema mikakati imewekwa kuondoa dhana kuwa mafunzo ya
kiufundi yametengewa wanafunzi ambao hawakupata alama za juu mitihani ya
kitaifa.
"Tunafanya kila
tuwezalo kutoa nafasi kwa wanafunzi kupata elimu bora. Tunafanya hivi kwa
kuboresha vyuo vya kutoa mafunzo hayo ili vifikie viwango vya kimataifa.
Tumetenga fedha za
kununua vifaa vya kisasa vya mafunzo ili wanafunzi waweze kupata ujuzi mwafaka
wanapohitimu," akasema Bw Ruto bila kufafanua zaidi.
Bw Ruto alisema elimu ya
kiufundi inaweza kuimarisha uchumi wa nchini kwa kutoa nafasi kuimarisha ujuzi
wao ili wapate ajira katika sekta za kiufundi kama viwandani.
"Waliohitimu kwa
mafunzo ya kiufundi wanaweza kusaidia kustawisha sekta ya utengenezaji bidhaa,
ambayo ni mojawapo ya ajenda nne za maendeleo ya serikali ya Jubilee. Tunapaswa
kuwa na nguvu kazi ya kutosha yenye ujuzi ili kutosheleza mahitaji ya
kiteknolojia katika taifa leo," Naibu Rais akasema.
Mipango kukamilika
Ruto alisema Wizara ya
Elimu imekamilisha mipango ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaosomea masomo ya
kiufundi wanapata mikopo kutoka kwa serikali.
"Ama kwa hakika
wanafunzi 27,000 kutoka vyuo mbalimbal vya kiufundi sasa wanapaswa kupata
mikopo hiyo," akaongeza, kauli yake ikithibitishwa na Katibu katika Wizara
ya Elimu Belio Kipsang'.
Mkutano huo pia
ulihudhuriwa na Mawaziri wa Elimu Amina Mohammed na mwenzake wa Fedha Henry
Rotich.
SERIKALI YA KENYA YAWEKA MIKAKATI KUIMARISHA SEKTA YA ELIMU YA KIUFUNDI
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 05, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment