AFISA wa Polisi aliyejipatia sifa lukuki kwa kupunguza uhalifu
katika eneo la Githurai, Ruiru, kaunti ya Kiambu mwaka mitano iliyopita
amehukukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa mauaji.
Titus Ngamau Musila almaarufu Katitu alisukumiwa miaka hiyo na
Jaji James Wakiaga aliyempata na hatia ya kumuua Kennedy Kimani Mwangi kwa
kumpiga risasi Machi 4, 2013, katika steji ya Githurai 45.
Kati ya miaka hiyo 15 Katitu atatumikia mitatu kifungo cha nje.
Miaka itakayosalia 12 atakuwa gerezani.
Pia Jaji James Wakiaga aliyempata Katitu Februari 7, 2018, na
hatia ya kumuua Kimani alisema miaka minne ambayo mshtakiwa alikuwa rumande
itazingatiwa na idara ya magereza ndipo itolewe katika kifungo hicho cha miaka
12.
Hivyo basi Katitu atatumikia kifungo cha miaka minane jela ndipo
atoke atumikie kifungo cha miaka mitatu chini ya uangalizi wa Afisa wa
urekebishaji tabia.
Akipitisha hukumu, Jaji Wakiaga alisema Katitu alikosa kufuata
sheria za kulinda maisha ya binadamu alipomuua Kimani na nduguye Oscar Mwangi
Machi 2013.
“Lazima kila afisa wa polisi ajue jukumu lake la kwanza ni kulinda
maisha ya kila mmoja wahalifu wakiwamo,” alisema Jaji Wakiaga akiongeza,
“Polisi wanatakiwa kisheria kutumia kila mbinu kumtia nguvuni mshukiwa
aadhibiwe kisheria badala ya kutamatisha maisha yake.”
Mahakama ilisema ijapokuwa Katitu alikuwa anashambikiwa mno na
wakazi wa Githurai walioomba korti imwachilie mshtakiwa arudi kuwatumikia kwa
vile "aliwapiga risasi majambazi hadi uhalifu ukapungua kwa kiwango
kikubwa hapa”.
Sheria
Jaji Wakiaga alisema ingawa msimamo wa wakazi wa Githurai ni
'mzuri', sheria inasema mengine.
“Sheria inawataka maafisa wa polisi wazingatie sheria hata wakiwa
na umaarufu wa kupambana na wezi. Polisi hawapaswi kuwatoa uhai washukiwa mbali
wanatakiwa kutumia kila mbinu kuwashika na kuwafikisha kortini kuadhibiwa
kisheria.”
Mahakama ilisema mshtakiwa alimpiga Kimani risasi mara tatu
kichwani na kumuua kabisa.
“Sifa za kuogopwa kwa Katitu zilienea kote jijini Nairobi na
maeneo jirani na hata wahalifu walimtambua. Angetumia sifa hizo kuwatisha
wahalifu kwa kupiga risasi angani ama kutumia mbinu nyingine kuwashika badala
ya kuwaua,” alisema Jaji Wakiaga.
Jaji huyo alisema sheria nambari 204 ambayo washukiwa wa mauaji
huhukumiwa inatoa adhabu moja tu - ya kifo.
Hata hivyo alisema kulingana na uamuzi wa Mahakama ya Juu wa hivi
majuzi majaji wanatakiwa kutilia maanani malilio ya mshtakiwa kabla ya
kupitisha hukumu.
Jaji Wakiaga alisema ijapokuwa kumekuwa na kampeni ya vyombo vya
habari mshtakiwa aachiliwe, sheria inasema mengine.
Alisababisha kicheko aliposema upeperushaji wa baadhi ya maoni
ndio unafanya Waziri wa Usalama Fred Matiang’i atukane majaji wa mahakamani
baada ya baadhi ya vituo vya habari kuwanukuu baadhi ya watazamaji wakitoa wito
Katitu aachiliwe wakisema “wahanga walikuwa wahalifu”.
Jaji huyo alisema Katitu alivunja sheria kuwaua Kimani na Oscar na
kuamuru afungwe jela.
AFISA WA POLISI AHUKUMI WA MIAKA 15 JELA KWA KUFANYA MAUAJI
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 05, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment