Rais Cyril Ramaphosa pamoja na watangulizi wake Jacob Zuma
na Thabo Mbeki walikuwa miongoni mwa maelfu ya wananchi waliohudhuria mazishi
ya mpigania uhuru, Winnie Madikizela Mandela yaliyofanyika kitaifa Jumamosi
katika Uwanja wa Orlando, Soweto.
Mwili wa Winnie Mandela ulitarajiwa kupelekwa kwa maziko
kwenye makaburi yaliyopo kitongoji cha Fourway umbali wa kilomita 40 Kaskazini
mwa Soweto
Waombolezaji waliimba sifa za Winnie wakati jeneza lenye
mwili wa mwanamama huyo shujaa lilipokuwa likiingizwa kwenye uwanja huo umbali
wa chini ya kilomita mbili kutoka nyumbani kwake
Jeneza lake lilifunikwa kwa bendera ya Afrika Kusini na
baada ya kuingizwa liliwekwa katikati ya uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua
watu 37,500 wote wakiwa wamekaa
Waombolezaji walikuwa wamevaa mavazi ya rangi za chama
tawala cha African National Congress (ANC), na za chama cha upinzani chenye
siasa kali cha Economic Freedom Fighters (EFF), huku wakiimba “hakuna, hakuna
kama Winnie”, wimbo maarufu kutoka enzi za harakati za ukombozi
Mazishi hayo yamehitimisha siku 10 za maombolezo ya kitaifa
kipindi ambacho maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini walitoa heshima zao kwa
“Mama wa Taifa” nyumbani kwake Soweto na kwingineko
Winnie Mandela, aliyefariki dunia katika hospitali jijini
Johannesburg akiwa na umri wa miaka 81, Aprili 2 baada ya kuugua muda mrefu,
amepongezwa kwa kusaidia kuweka hai ndoto ya Nelson Mandela ya Afrika Kusini
kuwa nchi isiyo ya ubaguzi wa rangi wakati yeye akiwa gerezani kwa miaka 27
“Alikuwa mmoja wa viongozi jasiri katika chama cha ANC,”
alisema mwombolezaji Brian Magqaza, 53. “Alipambana kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Nenda Mama yetu nenda.”
Mfuasi wa EFF Mufunwa Muhadi, 31, alisema “Mama alipigania
uhuru wetu. Ni muhimu sana kumpa heshima na tundeleze mapambano”.
Rais Cyril Ramaphosa, aliyeingia madarakani miezi miwili
iliyopita, aliongoza waombolezaji katika misa iliyofanyika kwenye uwanja huo wa
Orlando.
Marais wa zamani Jacob Zuma na Thabo Mbeki pia walishiriki.
Lakini waombolezaji bila kujali huzuni zao walimzomea Zuma alipotangazwa
kutambua uwepo wake
Watu kadhaa mashuhuri kutoka nje walihudhuria wakiwemo
viongozi wa Namibia, Swaziland na Jamhuri ya Congo, pamoja na mwanaharakati wa
haki za binadamu Jesse Jackson wa Marekani. “Huyu ni mama halisi wa Afrika
Kusini,” Jackson aliwaambia wanahabari.
Rais Ramaphosa aongoza mazishi ya Winnie Mandela
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 14, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment