Rais Magufuli azungumzia mabadiliko ofisi ya AG, DPP, awaapisha majaji 10

Rais John Magufuli amesema mabadiliko yaliyofanyika ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ni kuondoa changamoto ya Serikali kushindwa katika kesi mara nyingi

Alisema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam wakati akiwaapisha majaji 10 wa Mahakama Kuu na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka

Katika mabadiliko aliyoyafanya, Aprili 15 Rais Magufuli alimteua Dk Julius Mashamba kuwa Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi (Naibu Wakili Mkuu wa Serikali) na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Edson Makallo ambao jana aliwaapisha kuanza majukumu hayo mapya

Rais Magufuli alisema mara baada ya kuingia madarakani Novemba 5, 2015 moja ya maswali aliyokuwa akijiuliza ni kwa nini Serikali imekuwa ikishindwa kesi nyingi huku ikitumia wanasheria wa kampuni binafsi

Awali, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisema mwaka 2016 akiwa mwalimu wa chuo kikuu mwenye mkataba wa muda baada ya kuwa amestaafu, Rais Magufuli alimwita na kutaka kujua kwa nini Serikali inashindwa kesi

Alisema katika mazungumzo hayo alimweleza kwamba kunahitajika mabadiliko ya kimfumo katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ile ya Mkurugenzi wa Mashtaka jambo ambalo Rais Magufuli amefanikiwa kulitekeleza na matunda yake yataanza kuonekana

Rais Magufuli alisema tangu kufutwa kwa cheo cha Wakili Mkuu wa Serikali miaka 40 iliyopita kilichoongozwa mara ya mwisho na Jaji Mark Bomani, “tangia hapo, Serikali imekuwa ikishindwa kesi nyingi sana. 

Kesi yenye pesa, unakuta wakili wa Serikali na mtetezi wanaungana na kuwa kitu kimoja, kitu ambacho anatakiwa kukifanya hakifanyi hatimaye Serikali inashindwa. Ndio maana kuna kesi tulitumia Euro milioni saba (zaidi ya Sh18.7 bilioni), kwa nini tunashindwa,” alihoji Rais Magufuli, “Kwa nini kama tuna Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wanasheria wazuri tunatumia kampuni za nje?

Rais Magufuli alisema, “subirini wakati wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi wanasheria watajaa huko.”
Kuhusu majaji, Rais Magufuli alisema kazi ya kuwateua ni ngumu na kuwataka kumtanguliza Mungu mbele wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku
“Mtakutana na kesi za huruma za watoto maskini au wajane, kwa kuwa anayemshitaki ana pesa nyingi, kamtangulizeni Mungu mbele mnapotekeleza majukumu yenu,” alisema Rais Magufuli.
Kuhusu mabadiliko hayo DPP, Biswalo Mganga alisema, “yataleta tija kubwa sana.”
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma aliwakumbusha majaji hao dhamana waliopewa na akawataka kuwa waadilifu na kuchapa kazi kwa bidii ili kuepuka kuangukia mikononi mwa Tume ya Utumishi wa Mahakama.
“Katiba inawalinda lakini pia kumbukeni kama mtakuwa na mienendo mibaya mtaanza kufuatiliwa na tume,” alisema.
Alisema kuchaguliwa kwa majaji hao kumepunguza mzigo wa majaji kusikiliza mashauri mengi kwa mwaka. “Mzigo wa jaji mmoja kusikiliza mashauri 535 kwa mwaka sasa unashuka hadi kufikia 460,” alisema.
Alisema kwa kawaida jaji anatakiwa kusikiliza mashauri 178 kwa mwaka lakini kulingana na mazingira ya Tanzania, wastani uliowekwa ni kusikiliza mashauri 220 kwa mwaka.
Rais Magufuli azungumzia mabadiliko ofisi ya AG, DPP, awaapisha majaji 10 Rais Magufuli azungumzia mabadiliko ofisi ya AG, DPP, awaapisha majaji 10 Reviewed by KUSAGANEWS on April 20, 2018 Rating: 5

No comments: