Mwanafunzi awadakisha baba, dada


Kuna aina nyingi za ushujaa. Wapo mashujaa wa vita, ukombozi wa kisiasa na wengine ni mashujaa wa harakati za kupambana na mambo yasiyofaa katika jamii

Mwanafunzi Rehema John (siyo jina halisi), aliyehitimu darasa la saba mwaka jana katika Shule ya Msingi Kasamwa wilayani Geita na kufaulu akitakiwa kujiunga na Sekondari ya Kasamwa ni miongoni mwa walioingia kwenye orodha ya mashujaa mwaka huu.

 Ushujaa wa binti huyo mwenye miaka 13 ni kupambana na kufanikiwa kuzuia mpango wa wazazi na ndugu zake kumuoza kwa mwanaume aliyemlipia mahari ya ng’ombe watano na Sh100,000 tangu akiwa shuleni.

Hii ni baada ya kufanikiwa kumtoroka mwanaume huyo siku moja baada ya kukabidhiwa kwake na kulala naye usiku kucha kutokana na kuogopa giza nene iliyokuwa imetanda nje.

Pia, jitihada hizo zimefanikisha baba yake mzazi, Kashilimu Mashimba (60), dada yake, Kefline Mashimu na ‘mumewe’ Sayai Petro, wakazi wa Kasamwa mjini Geita kutiwa mbaroni na polisi.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo aliliambia gazeti hili kuwa watuhumiwa hao wanashikiliwa tangu Aprili 27.

Alisema bila kujua mpango wa wazazi na dada yake, Machi 14 mwananfunzi huyo alitakiwa kujiandaa kwenda kwa mume wake ambaye tayari ilikuwa amelipa mahari hayo.

“Mahari ya kumuoa yalitolewa na baba wa Sayai anaitwa Petro Masalu ambaye pia ni miongoni mwa watakaokabiliana na mkono wa sheria,” alisema.

Mwanafunzi huyo alilieleza gazeti hili: “Usiku ule sikuwa na namna ya kutoroka kwa kuogopa giza nene, kulipopambazuka nilidanganya kuwa naenda dukani nikapata upenyo wa kukimbilia kwa marafiki wa elimu waliokuwa wakifika shuleni kutuelimisha umuhimu wa shule na namna ya kukabiliana na ndoa za utotoni,” alisema Rehema.

Mwanafunzi awadakisha baba, dada Mwanafunzi awadakisha baba, dada Reviewed by KUSAGANEWS on April 30, 2018 Rating: 5

No comments: