Mvua yageuka neema kwa madereva wa bodaboda, bajaji


Mvua kubwa iliyonyesha kuanzia jana na inayoendelea mpaka sasa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam,  imesababisha kufungwa kwa barabara ya Morogoro katika eneo la jangwani kutokana na daraja la mto Msimbazi kujaa maji

Hata hivyo licha ya madhara hayo, lakini hali hiyo imekuwa ni fursa kwa baadhi ya madereva bodaboda na waendesha maguta ambao wameonekana kujipatia wateja maradufu

Akizungumza katika eneo la Jangwani,  Ramadhan Juma amesema walitamani hali ya mafuriko itokee siku ya kazi kwa kuwa  leo wameingiza fedha nyingi kwa kuwavusha kwa kutumia pikipiki zao
Juma amesema wamekuwa wakivusha  kwa Sh 1000 hadi 2000 kwa mtu mmoja na kuwapeleka katika kituo cha mabasi cha Jangwani huku wengine wakichukuliwa na kupelekwa ng'ambo ya Magomeni

"Leo watu siyo wengi ingekuwa jumatatu tungeingiza fedha nyingi,mimi nimekuja hapa tangu saa 12 asubuhi hadi sasa hivi nimepata Sh15,000 na tupo wengi tunafanya biashara hii ya bodaboda,"amesema Juma

Naye mmiliki wa guta,Kamal Yasin amesema amefika saa tatu asubuhi ili kuwasaidia watu  wanaovuka eneo la jangwani hivyo mtu anayepanda kwenye guta analipia Sh 500 huku wazee wakivushwa bure

"Hadi muda huu nimeshaingiza Sh 35,000 hivyo tunaendelea kutoa huduma hii hadi hapo maji yatakapopungua”,amesema

Mvua yageuka neema kwa madereva wa bodaboda, bajaji Mvua yageuka neema kwa madereva wa bodaboda, bajaji Reviewed by KUSAGANEWS on April 15, 2018 Rating: 5

No comments: