Wakati Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ikiendelea
kusikiliza mashauri ya wanawake na wanaume kuhusu kutelekeza watoto, kampeni
hiyo imeibua maswali kadhaa, huku baadhi ya watu wakitaka tahadhari ichukuliwe
kuepusha athari
Kwa siku tatu mfululizo sasa, wakazi wa jijini Dar es
Salaam, hasa wanawake, wamekuwa wakifurika ofisi hiyo kuwasilisha madai ya
kutelekezwa na wazazi wenzao, ikiwa ni kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa, Paul
Makonda ambaye ameeleza kuwa anataka kuwasaidia kutafuta suluhisho
Kampeni hiyo imekumbwa na matukio kadhaa, kama ya wanaume
kujitokeza wakidai kukimbiwa, wasichana wa umri mkubwa kudai pia wametelekezwa
na baba zao, huku Makonda akidai miongoni mwa waliotajwa ni wabunge na viongozi
wa dini
Katika nchi ambayo ina utamaduni wa kushughulikia masuala ya
ndoa kwa faragha, ina sheria na taasisi za kushughulikia masuala hayo nyeti,
kampeni hiyo imeibua hisia tofauti; baadhi wakisifu, wengine wakikosoa,
kushauri jinsi ya kutelekeza mradi huo na wengine kuibua maswali kuhusu ufanisi
na athari za kitendo hicho
Baadhi ya wasomaji wa Mwananchi wamekuwa wakipiga simu
kuulizia uhalali wa kampeni hiyo, huku watumiaji wa mitandao ya kijamii
wakiibua hoja za kisheria, kijamii na kiutamaduni kuhusu utekelezaji wa mradi
huo
Mwananchi imechambua maswali na hoja hizo na kuziweka katika
vipengele kumi na baadaye kuhoji wadau na pia kuchukua maoni ya watu
waliojitokeza hadharani, kama bungeni na kwenye akaunti za mitandao ya kijamii,
kuzungumzia suala hilo
Maswali hayo yanajikita katika mila na utamaduni wa
Kitanzania, sheria kama ya mtoto na ndoa, uwezekano wa mpango huo kutoa
suluhisho, utayari wa watuhumiwa kuitikia wito, athari dhidi ya watoto, hadhi
ya wahusika na mgongano unaoweza kutokea baina ya taasisi zilizopewa dhamana ya
kushughulikia masuala hayo
“Ushauri wangu kama wizara inayosimamia haki za watoto,
suala hili linapaswa kufanyika kwa faragha kwa sababu una-deal na watu,”
alisema Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustin Ndugulile, ambaye wizara yake pia
inaongoza Idara ya Ustawi wa Jamii
“Anachokifanya RC Makonda ni jambo zuri, lakini linahitaji
uangalifu na tufuate mifumo sahihi. Nitoe wito kwa wananchi wote kufuata
taasisi zinazohusika.”
Dk Ndugulile ni mmoja wa watu waliozungumzia suala hilo,
wakijibu moja ya maswali yaliyoibuka kuhusu utaratibu wa kushughulikia masuala
ya malezi na ndoa, ambayo hushughulikiwa na taasisi zinazohusika kwa njia ya
faragha
Kauli yake inatokana na hali iliyojitokeza kwenye ofisi
hiyo, ambako wanawake wengi walienda wakiwa wamebeba watoto na kuachia baadhi
ya watu kuwapiga picha na baadaye kuzisambaza mitandaoni, ikiwemo picha ya
mtoto chotara wa Kichina na Kitanzania, iliyosababisha mama yake kulalamika
Mila na desturi zinasemaje?
Moja ya maswali hayo ni kama kazi hiyo inafuata mila na
desturi za Kitanzania
“Kinachofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa kinakwenda
kinyume na mila na desturi za Mtanzania kwa sababu masuala yanayohusu mzozo wa
kifamilia na ndoa hufuata ngazi maalumu,” alisema Mwanaharakati wa haki za
binadamu na masuala ya jinsia, Gemma Akilimali
“Mara zote kunapotokea mvutano unahusisha wanandoa
kutoelewana au utata kuhusu mimba, watu wa kwanza wanaopaswa kutatua tatizo
hilo ni familia na inapoonekana suala hilo linashindikana, jamii ya eneo
hilo.”<
Kisheria ni sahihi?
Pia suala jingine ni kuhusu sheria
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, mkurugenzi wa Chama cha
Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), Tike Mwambikile alisema kitendo cha
wanawake na watoto kupigwa picha na kuonyeshwa kwenye vyombo vya habari na
mitandao ya kijamii si sawa
Hoja kama hiyo ilitolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu
aliyesema tatizo la kampeni hiyo ni kutokuwa na faragha ya watoto licha ya
kinachofanyika kuwa ndani ya sheria huku wahudumu wakitokea idara ya Ustawi wa
Jamii
Alisema ni kosa kisheria kwa chombo cha habari au mitandao
ya jamii kuonyesha picha zenye kumdhalilisha mtoto
Kuna mgongano wa kitaasisi?
Kuhusu baadhi ya mashauri kuwahi kuwasilishwa kwenye vyombo
husika na hivyo kuwepo uwezekano wa maamuzi kugongana, Akilimali alisema si
jambo la busara mkuu wa mkoa kuwakusanya watu sehemu moja na kuanza kusikiliza
shida zao na iwapo ataendelea kufanya hivyo atakuwa amezipuuza taasisi
nyingine, hivyo kuibua mvutano
Mwantum Mgonja, ambaye ni miongoni mwa wanasheria
wanaosikiliza malalamiko hayo, alisema wengi waliofika walianzia ustawi wa
jamii na baadhi walifikisha masuala yao mahakamani
Kampeni kutoa suluhisho la kudumu?
Baadhi wanaona jitihada hizo za RC zinaweza zisitoe
suluhisho lenye ufanisi na mkurugenzi wa Chama cha Wajane (Tawia), Rose Serwati
anaona kampeni hiyo inaweza ikachangia kuvunja ndoa za watu na kuweka uadui
kati ya baba, mama na mtoto
Hoja kama hiyo ilitolewa juzi na mbunge wa Ulanga (CCM),
Goodluck Mlinga alipotaka ufafanuzi wa kampeni hiyo, akisema njia inayotumika
ni ya kubomoa na si kujenga
Lakini mhadhari msaidizi, Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW),
Abigael Kiwelu alimshauri Makonda kutumia fursa hiyo kuelimisha wanawake hao
ili wafikishe matatizo yao kwa maofisa ustawi wa jamii walioko kwenye kila kata
Nini kitafanyika kwa wasioitikia wito
Wakati Makonda akitoa kauli kwamba wasioitikia wito kwenda
kusikiliza malalamiko dhidi yao watatangazwa, mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema Sheria ya Kanuni za
Adhabu sura ya 16 kifungu cha 166 inawataka wazazi kulea na kutunza watoto wao
Alisema mzazi anayekwepa kumlea mtoto au kumtunza hali ana
uwezo, wa kumuhudumia atakuwa ametenda kosa la jinai
Alisema Sheria ya Haki ya Mtoto ya mwaka 2009 inawahimiza
wazazi na walezi kulea watoto wao na kutimiza majukumu yao yote
Uhakiki wa madai yanayotolewa ukoje?
Katika kinachooneka kutaka uhakika wa madai dhidi ya wabunge
wanaotuhumiwa kutelekeza watoto, Spika wa Bunge, Job Ndugai juzi aliwataka
wazazi wenye malalamiko hayo waende kwake wakiwa na matokeo ya kipimo cha DNA
Ndugai alisema inabidi ufanyike utaratibu ili kujua namna
gani ya kushughulikia suala hilo
Kuna ajenda ya siri?
Hata kabla ya kuanza kusikiliza mashauri hayo, tayari watu
kadhaa walishatuhumu kuwa huenda mpango huo una ajenda ya siri na tayari baadhi
ya wanasiasa wamesema bayana kuwa kuna njama za kuwachafua
Tuhuma kama hizo ziliibuka pia wakati wa kampeni ya kusaka
watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya iliyotaja pia wanasiasa na viongozi wa
kidini
Maswali mengine ni pamoja na kama kampeni hiyo itatoa fursa
sawa ya kusikilizwa kati ya wanaume na wanawake na kama haki za kibinadamu
zitafuatwa
“Unapowaweka watu pale hadharani unavunja haki ya kuwa na
faragha. Mtu anaweza kushtaki kama ataona amedhalilishwa,” alisema mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Jesse James
Imeandikwa na Nasra Abdallah, Elias Msuya, Harieth Makwetta,
Kalunde Jamal, Raymond Kaminyoge, Tumaini Msowoya, George Njogopa, Sharon
Sauwa, Elizabeth Edward na Fortune Francis
Maswali 10 kampeni ya Makonda wanawake waliotelekezwa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 12, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment