Zenani, mtoto wa mwanamapinduzi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela
na Julius Malema ambaye ni kiongozi wa chama cha EFF jana, walifanya tukio
lisilo la kawaida baada ya kuamua kuwapa vidonge vyao wasaliti na wabaya wa
Winnie Mandela mbele ya umati uliofurika kuaga mwili wake kwenye Uwanja wa
Orlando
“Mama‚ wale waliokusaliti kwa watawala (enzi za ubaguzi wa rangi)
wako hapa,” alisema Malema mbele ya maelfu ya waombolezaji waliofurika kuaga
mwili wa Winnie, mke wa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela
Zenani pia aliwaliza waombolezaji aliposema mama yake aliporwa
haki yake wakati wa maisha yake. Zenani pia alivicharukia vyombo vya habari
akisema vilitumika kumchafua mama huyo
“Kwanini waliukalia ukweli na kusubiri hadi mama yangu afe ndipo
wauseme? Wamepora urithi wa haki wa mama yangu wakati wa uhai wake,” alisema
Zenani huku dada yake Zindzi akiwa pembeni yake
Alionyesha kukasirishwa na kauli ya kamishna wa zamani wa polisi
nchini humo, George Fivaz ambaye wiki iliyopita baada ya kifo cha Winnie
alisema hakuna kinachomhusisha Winnie na kifo cha Stompie Seipei. Zenani
alisema wote waliomfanyia mabaya mama yake wasifikiri hata mara moja familia
itayasahau mambo hayo
“Kumsifia sasa hivi kunaonyesha wazi jinsi ulivyo mnafiki,”
alisema Zenani akimtaja Fivaz na akaongeza: “Maumivu aliyoyapata maishani mwake
yapo kwetu.”
Malema alisema pamoja na huzuni aliyonayo kwa kumpoteza Winnie anafurahia namna alivyofariki dunia, akiongeza kwamba hakuwasaliti watu wake
“Mama wale waliokusaliti kwa watawala wako hapa. Wanalia kwa sauti kubwa kuliko sisi sote tuliokuheshimu‚” alisema katika hotuba yake
Malema aliwataja watu waliomshambulia mama huyo wakati wa uhai wake, kwanza akiwashutumu viongozi wa zamani wa chama cha United Democratic Front (UDF) ambao waliitisha mkutano wa waandishi wa habari wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi ili kutangaza kujitenga na mwanamama huyo
Pia, aliwashambulia viongozi wa ANC ambao walimwita mama huyo kuwa
mhalifu na baadaye walimzuia kuzungumza katika msiba wa mwanaharakati kijana,
Peter Mokaba
“Wasaliti‚ tunawaona. Maisha hayana usawa‚” alisema Malema.
Aidha kiongozi huyo wa EFF aliwapongeza watu waliosimama kidete na
Winnie Madikizela-Mandela wakati alipodhalilishwa
“Winnie Mandela ni mama yetu. Tunamfahamu. Hatumhitaji Fivaz kutuambia chochote kuhusu Winnie Mandela‚” alisema Malema
Alitoa wito kwa wakazi wa Soweto ambako alikuwa akiishi hadi alipofariki dunia, wasimsahau kamwe Winnie Mandela
Pia Malema alipendekeza uwanja wa ndege wa Cape Town upewe jina la
Winnie.
Malema, Zenani wachafua hali ya hewa msiba wa Winnie Mandela
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 15, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment