Mahakimu wapewa somo juu ya lugha zao


Hakimu wa Mahakama ya Watoto Zanzibar, Naila Abdulbast amewataka Mahakimu kutumia lugha nyepesi ambayo haiwezi kumtisha mtoto wakati wanaposikiliza kesi hizo Mahakamani.

Akizungumza katika warsha ya uelewa wa sheria kwa Mahakimu, Polisi na Wanasheria, Hakimu huyo amesema ni vyema kesi za watoto hasa zile za udhalilishaji wa kijinsia kusikilizwa faragha na sio kila mtu kuweza kusikia anachohojiwa mtoto.

"Kitendo cha kutumia lugha ambayo sio rafiki kwa mtoto kuna pelekea watoto kushindwa kujieleza kwa ufasaha na kukosekana kwa ushahidi. Mtoto kama hawezi kujieleza vizuri ni bora Mahakimu kuhairisha kesi kwa siku hiyo na kuja kuisikiliza tena au kutumia ushahidi kwa njia ya kieletroniki", amesema Hakimu Naila.

Aidha, Hakimu Naila amesema sauti za wanaharakati wa kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia zimesaidia kufanya baadhi ya sheria kurekebishwa hali ambayo imesaidia kuongezeka kwa hukumu kwa mtu atakaebainika na kosa la udhalilishaji.

"Baadhi ya Mahakama zimeongezewa uwezo wa kuwatia hatiyni watakaobainika kufanya matendo hayo ambapo awali mahakama ya wilaya ilikuwa na uwezo wa hukumu ya miaka mitano tu na mahakama ya mkoa miaka saba lakini hivi sasa ina uwezo wa kuhukumu hadi miaka 14",amesisitiza Hakimu Naila.

Kwa upande wake, Naibu Mrajis wa Mahakama kuu Zanzibar Salum Hassan Bakar ameitaka jamii endapo ikiwa kuna Hakimu anakwenda kinyume na kazi zake ni vyema kufuata sheria ili kuweza kumripoti katika sehemu husika ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mahakimu wapewa somo juu ya lugha zao Mahakimu wapewa somo juu ya lugha zao   Reviewed by KUSAGANEWS on April 24, 2018 Rating: 5

No comments: