MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Dodoma
imesema imejiridhisha kuwa mshitakiwa Onesmo Machibya (44), maarufu kama Nabii
Tito ana ugonjwa wa akili hivyo apelekwe taasisi za magonjwa ya akili kwa ajili
ya tiba.
Mahakama hiyo pia imemuachia huru
katika kosa la kutaka kujiua baada ya kuthibitika kuwa alifanya hivyo kutokana
na ugonjwa wa akili.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama
hiyo, James Karayemaha ametoa uamuzi huo.
Hakimu Karayemaha amesema kutokana
na taarifa ya uchunguzi wa akili wa mshitakiwa iliyopokelewa mahakamani hapo
imethibitika kuwa Nabii Tito ni mgonjwa wa akili.
"Mahakama inamuachia huru
katika kosa la kutaka kujiua na inatoa amri mshitakiwa kupelekwa hospitali ya
wagonjwa wa akili na akishapona ataachiliwa huru aendelee na maisha yake,"
amesema Hakimu Karayemaha.
Nabii Tito kabla ya kukamatwa
alikuwa akitoa mahubiri yanayoonekana kuhimiza ulevi na uasherati.
Alipandishwa kizimbani kwa mara ya
kwanza Januari 29, mwaka huu na kusomewa mashtaka ya kujaribu kujiua ambapo
alifanya jaribio la kujiua Januari 25, mwaka huu akiwa mahabusu, ambapo
inadaiwa kwamba alijikatakata na wembe kwa lengo la kuyakatisha maisha yake.
Alipotakiwa kujibu mashtaka
yanayomkabili, Nabii Tito awali alisema hakumbuki chochote kwa sababu yeye ni
mgonjwa wa akili, lakini alipobanwa kwa mara nyingine, alisema ni kweli alitaka
kujiua kwa sababu kuna sauti ndani ya kichwa chake iliyokuwa inamuelekeza
kufanya kitendo hicho.
Janauri 23, mwaka huu, Kamanda wa
Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alisema Nabii Tito alikamatwa baada ya
kurekodi vipande vifupi vya video na picha vyenye maudhui ya kukashifu dini
nyingine, na kuleta chuki dhidi ya watu wengine na kurusha mitandao ya kijamii,
kinyume na kifungu cha sheria namba 129 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 na
marekebisho yake ya 2002.
Mahakama- Nabii Tito mgonjwa wa akili
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 22, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment