Wanaotaka kuuza figo Muhimbili waongezeka


IDADI ya watu wanaotaka kuuza figo yao kwa ajili ya kupandikizwa kwa wagonjwa wenye matatizo ya kiungo hicho imekuwa ikiongezeka siku hadi siku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Onesmo Kisanga alisema hayo alipozungumza na gazeti hili kuhusu idadi ya watu hao baada ya hospitali hiyo kuanza huduma hiyo ya kupandikiza figo Novemba mwaka jana.

Kwa mujibu wa Dk Kisanga, mpaka juzi tayari walikuwa wamefikia watu 10, na mwishoni wa wiki iliyoisha, watu wawili walimtumia na kumpigia simu kuwa wanataka kuuza figo zao ili kujikimu na maisha.
Alisema siyo hao tu, bali tokea huduma hiyo ilipoanza, kuna mafaili ya watu hao ambao wanataka kuuza figo zao, hali ambayo amekuwa akizungumza nao na kuwaelewesha kuwa kufanya hivyo ni jambo lisilokubalika kimataifa.

“Mpaka jana (juzi) wameshafika watu 10 kwa mwaka huu wanaotaka kuuza figo zao,” alisema Dk Kisanga na kutaja sababu kubwa inayowafanya watu hao wauze figo zao ni ili wapate fedha za kuwawezesha kumudu maisha.
"Tunawashauri watu hao na kuwaelimisha kuwa haturuhusu kuuza figo. Hapa tunamlinda mtoa figo asirubuniwe kwa kuwa tatizo la figo ni kubwa kwa watu wengi," alisema Dk Kisanga.
Alisema kwa mtu mwenye tatizo la figo, anashauriwa ndugu yake wa karibu ndiyo anapaswa kumtolea figo akiwepo mtoto wake, dada au kaka, baba au mama na si wa pembeni kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa figo ya mtu wa pembeni isiendane na mgonjwa husika.
Amesema kuna azimio la mwaka 2004 la kuzuia kuuza viungo hasa figo kwa kuwa tatizo hili ni la ulimwengu mzima.

Amesema hospitalini hapo kuna wagonjwa zaidi ya 200 na wanazidi kuongezeka, na hapa nchini hivi sasa kuna wagonjwa 800 ambao wanasafisha damu.

Kwa maelezo ya daktari huyo, wagonjwa 60 tayari wamefanyiwa vipimo na wapo tayari kupandikizwa figo, hivyo alitoa mwito kwa jamii kuzuia figo zao zisipate shida kwa kubadilisha tabia na pale wanapozidiwa waende hospitali.

Wiki iliyopita, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilipandikiza figo wagonjwa wanne kati ya watano walioandaliwa, ikiwa ni awamu ya pili kufanyika nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Profesa Lawrence Museru aliwaambia waandishi wa habari kuwa mgonjwa wa tano aliyekuwa ameandaliwa, alikutwa na tatizo la kitaalamu hivyo wataalamu walikubaliana aendelee na uchunguzi zaidi ili wasisababishe matatizo mengine.

“Sasa ni awamu ya pili. Tulitayarisha wagonjwa watano wafanyiwe upandikizaji wa figo wamefanyiwa wanne. Upandikizaji wa figo nchini tulianza Novemba mwaka jana kwa mara ya kwanza. Ulifanikiwa vizuri na mgonjwa anaendelea vizuri,” alisema Profesa Museru.

Alisema kutokana na kuboreshwa kwa miundombinu watajitahidi kupandikiza figo kwa wagonjwa watano kila mwezi.

Alisema kutokana na idadi hiyo, kwa mwaka watakuwa wamepandikiza figo kwa wagonjwa 60. Alisema baada ya upandikizaji huo kukamilika, wameanza mazungumzo na wataalamu kutoka India ambao wamekuwa wakishirikiana nao, ili waje mwezi ujao kuendelea na wagonjwa wengine watano walioandaliwa.

“Naamini baada ya miezi mitatu ijayo wataalamu wetu watakuwa wanafanya wenyewe upandikizaji huo bila kuhitaji wataalamu kutoka nje kusaidia,” alieleza Profesa Museru.

Alisisitiza kuwa mipango ya muda mrefu ni kuwa na sehemu maalumu kwa ajili ya upandikizaji wa figo. Kabla ya huduma hiyo kutolewa nchini, kati ya Sh milioni 80 hadi 100 zilitumika kwa mgonjwa mmoja kwenda nje ya nchi, tangu kuanza kwa huduma hiyo nchini gharama ni Sh milioni 21.

Mbali ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mwishoni mwa mwezi uliopita ilikuwa hospitali ya pili nchini kupandikiza figo, baada ya kufanikiwa kumpandikiza figo mkazi mmoja wa Mvumi mkoani Dodoma.

Wanaotaka kuuza figo Muhimbili waongezeka Wanaotaka kuuza figo  Muhimbili waongezeka Reviewed by KUSAGANEWS on April 22, 2018 Rating: 5

No comments: