Maaskofu watatu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) ‘wametengwa’ na kanisa hilo kwa tuhuma za usaliti
unaohusishwa na masuala ya kisiasa
Mbali ya Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na
Pwani, Dk Alex Malasusa aliyeripotiwa jana na vyombo vya habari kwamba
ametengwa, wengine ni Dk Solomon Massangwa wa Dayosisi ya Kaskazini Kati na Dk
Lucas Mbedule wa Dayosisi ya Kusini Mashariki
Hatua ya kuwatenga maaskofu hao ilifikiwa
katika mkutano wa Baraza la Maaskofu wa KKKT uliofanyika Aprili 24 na 25 jijini
Arusha kujadili masuala mbalimbali ikiwamo kufanya tathmini ya waraka wake wa
Sikukuu ya Pasaka lililoutoa Machi 24
Habari za uhakika kutoka ndani ya Baraza
hilo zinasema kwamba pia limewapa maaskofu hao watatu muda wa hadi Septemba
kuandika barua kueleza kama wanaukubali au kuukataa waraka huo ambao limesema
walishiriki kuuandaa na ikiwa hawatafanya hivyo hatua zaidi dhidi yao
zitachukuliwa
Kwa hatua hiyo, waumini wa dayosisi zao
hawatakuwa na uwakilishi kwenye Baraza la Maaskofu hivyo kupoteza fursa ya
kujadiliwa kwa masuala yanayowahusu
Pia, maaskofu waliotengwa hawataruhusiwa
kufanya shughuli za kiroho nje ya dayosisi zao wala maaskofu wengine 24
waliobaki hawatashiriki masuala yoyote ya kiimani katika dayosisi hizo tatu na
uamuzi wa mwisho kuhusu nafasi zao umeachwa kwa waumini wao
Waraka huo walioutoa baada ya kikao
kilichofanyika Arusha Machi 15, mbali ya kuzungumzia masuala ya kiroho, umetaja
changamoto tatu na kuzifikisha kwa waumini wake “ili ziongeze mzigo wa
kuliombea taifa letu na viongozi wake.”
Changamoto zilizotajwa katika waraka huo
uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ na kusainiwa na maaskofu wote 27 wa
kanisa hilo nchini ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa na masuala
mtambuka likiwamo la Katiba Mpya
Baraza hilo liliagiza maaskofu wote
kuusimamia ili usomwe katika sharika zote nchin
Hata hivyo, imeelezwa kuwa maaskofu 25 kati
ya 27 waliokutana mkoani Arusha, katika tathimini, walibaini wenzao hao
kuwasaliti ikielezwa kuwa baada ya kuupokea hawakusimamia kuhakikisha unasomwa
kama walivyokubaliana Machi 15 wakiuhusisha na siasa
“Unajua ule waraka walioutoa maaskofu
ulikuwa mzito na kishindo chake mlikiona, sasa kabla ya kusomwa kuna watu
waliwafuata baadhi ya maaskofu na kuwatisha wasiusome na wao wakakubali bila
kujua wanachokifanya ni makosa,” kilidokeza chanzo na kuongeza
“Ndiyo maana kama unakumbuka, Askofu Mkuu wa
KKKT, Frederick Shoo alitoa kauli ya kuwaonya wanaoupinga.”
Waliotengwa
Alipoulizwa jana kwa simu kuhusu kutengwa,
Askofu Mpedule alisema, “aaa, sio kweli, muulize huyo aliyekupa taarifa atakuwa
na majibu mazuri.”
Alipoulizwa kama alisimamia waraka huo
kusomwa kama walivyokubaliana, alijibu kwa kifupi, “Hapana sina jibu.”
Askofu Masangwa kwa upande wake alisema,
“Sina barua inayosema nimetengwa.” Alipoulizwa kama alisimamia waraka huo kusomwa
alijibu, “Ulisomwa katika makanisa mengi.”
Hata hivyo, mawasiliano ya simu yalikatika
katikati ya mazungumzo na alipopigiwa tena hakupokea na kutuma ujumbe mfupi wa
maandishi akisema yupo kikaoni
Jitihada za kumpata Dk Malasusa ziligonga
mwamba kutokana na simu yake ya kiganjani kutokupatikana
Hata hivyo, juzi jioni alipopigiwa
kuzungumzia suala hilo hakuwa tayari kuzungumza kwani baada ya mwandishi
kumweleza kuhusu hatua hiyo aliomba apigiwe kwa simu ya ofisi na alipofanya
hivyo hakuipokea
Jana, Dk Shoo ambaye pia ni Askofu wa
Dayosisi ya Kaskazini hakupatikana kuzungumzia suala hilo
Machi 25, Askofu Shoo akiwa katika Usharika
wa Masama Kati, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro baada ya Mchungaji Kiongozi wa
usharika huo, Pray Usiri kuusoma waraka huo, aliwaomba Wakristo na Watanzania
kuutafakari kwa makini huku akiwaonya wanasiasa kuepuka kuwagawa Watanzania
akisema hawatakaa kimya
Waraka huo uliokuwa na kurasa nane
ulipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika ukusanyaji kodi huku
ukitaka kuwapo kwa jitihada za mara kwa mara baina ya sekta binafsi na Serikali
za kuimarisha uhusiano mwema.
Huo ni waraka wa pili kutoka kwa viongozi wa dini baada ya Februari mwaka huu, Baraza laMaaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kutoa ujumbe wa Kwaresma uliosaniwa na maaskofu wake 35 uliozungumzia masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Maaskofu watatu KKKT ‘watengwa’
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 29, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 29, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment