TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa miezi mitatu ya
Januari hadi Machi 2018 imehudumia wagonjwa 19,371 wenye matatizo ya moyo
wakiwemo 890 waliolazwa.
Taarifa ya kitengo cha uhusiano cha taasisi hiyo, wagonjwa 105
wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua wakiwemo watu wazima 53 na
watoto 52.
Kati ya wagonjwa 105 waliofanyiwa upasuaji 66 wamefanyiwa na
madaktari bingwa Watanzania. Madaktari hao wamefanya upasuaji wa watoto 35 na
watu wazima 31.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, upasuaji wa moyo bila kufungua kifua
kwa kutumia mtambo wa Cathlab ulifanyika kwa wagonjwa 231 wakiwemo watoto 20 na
watu wazima 211. Imesema, kati ya wagonjwa 231 waliotibiwa watu wazima 211
walifanyiwa upasuaji na madaktari wa Tanzania.
“Kwa kipindi cha miezi mitatu tumekuwa na jumla ya kambi za matibabu
nane (8) ambapo tulifanya matibabu kwa kushirikiana na washirika wetu kutoka
nchi za Ujerumani, Israel, Australia, Marekani, India na Falme za Kiarabu”
imesema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kambi hizo wagonjwa 39
walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua wakiwemo watoto 17 na watu wazima 22.
Wagonjwa 72 walifanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua wakiwemo watoto 20 na
watu wazima 52.
“Tumefanya upasuaji wa kuunganisha mishipa ya damu (AVF- Arterio
Venous Fistula) kwa ajili ya kusafishia damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya
figo (Hemodialysis) 36”imesema.
Amesema, changamoto kubwa inayoikabili taasisi hiyo ni wagonjwa
wengi mioyo yao kutokuwa kwenye hali nzuri hivyo amewaomba wananchi wawe na
tabia ya kupima afya mara kwa mara ili wapate tiba kwa wakati.
JKCI yatibu wagonjwa 19,371 miezi mitatu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 19, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment