CAG: HAKUNA MBADALA WA CCM TANZANIA.

Leo natumia fursa hii adhimu kuwaletea makala inayoeleza mustakabali wa  Vyma vya Siasa na mbadala wa Chama Cha Mapinduzi kwa kuitizamia na  kuichambua ripoti ya CAG iliyotolea hivi karibuni.

Nianze na msemo maarufu unaotumiwa na mwanasiasa mmoja hapa nchini kuwa" Chama chochote cha Siasa ni kama nyumba ya vioo, kila lifanyikalo ndani wananchi huona na kufanya tathimini, maamuzi hufanyika kwenye chumba cha kura, hivyo ni vyema Vyama vya siasa na Wanasiasa wawe na uwezo wa Kujitathimi mara kwa mara".

Tanzania tuliingia rasmi kwenye mfumo wa Demokrasia ya Vyama vingi mwaka 1992, mpaka sasa tuna jumla ya Vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu takribani ishirini na moja ikiwemo Vyama vya AFP, ADC, CHADEMA, TLP, CCM, NLD, NCCR Mageuzi, Demokrasia Makini,ACT Wazalendo, Chama Cha Kijamii na vingine vingi. Lengo kuu la kuwa na vyama vingi ni kuleta ushindani wa kiuongozi na kuwapatia wananchi uwanja mpana wa  kuchagua viongozi na vyama vyao kwa kuangalia uwajibikaji wao, ukaribu wao na namna wanavyoweza kufikika kwa wananchi, uzalendo kwa Taifa lao, namna wanavyowasemea na kuhangaika na shida zao pamoja na uadilifu wao wenyewe kama viongozi na taasisi wanazoziongoza.

Malengo yote hayo hupimwa na wananchi wenyewe kwa kusaidiana na taasisi mbalimbali ambazo zinafanya kazi kwa kutumia kodi za wananchi hivyo baada ya kazi kubwa huleta mrejesho kwa wananchi juu ya maendeleo ya Vyama hivyo ili kuwaongezea zaidi wananchi uelewa wa nini kinafanyika ndani ya taasisi hizo za siasa na viongozi wao. Mfano wa Taasisi zenye jukumu hilo la ukaguzi ni, TAKUKURU, Tasisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa  Hesabu za Serikali, Tume ya Maadili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na nyinginezo.

Tangu kuanza kwa  Vyama vingi mwaka 1992, Chama Cha Mapinduzi ( CCM ) kimekuwa kikiibuka kidedea katika Chaguzi mbalimbali hivyo kuunda Serikali. Kuanzishwa kwa mfumo wa Vyama vingi ulikuwa na maana kuwa vijitokeze Vyama vyenye mawazo na maono mbadala wa namna utendaji wa kuwaletea wananchi maendeleo inabidi ufanyike. Vyama hivyo tangu mwaka 1992 wananchi wamekuwa na matarajio ya kuwepo kwa uwazi mkubwa, uadilifu na uwajibikaji wa kiwango ambacho CCM haifikii ili waweze kuupata mbadala wa kiuongozo kutoka Chama kingine kama zilivyo nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Ghana, Nigeria Gambia nakadhalika.

Hivi karibuni Taasisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( CAG ) pamoja ukaguzi wa jumla pia imeangazia kiundani vyama vyote vya siasa na kupima uadilifu katika mapato na matumizi ya fedha za walipa kodi kwa kuzingatia vyama vya siasa hupata ruzuku kutoka serikalini ikiwa ni sehemu ya kodi za watanzania. Katika ukaguzi huo, Vyama kadhaa vya siasa vimeshindwa kuonesha ni kwa namna gani wametumia fedha walizopewa na Serikali na lakini pia kutoka katika vyanzo mbalimbali. Kwa masikitiko makubwa hali ni mbaya zaidi kwa vyama ambavyo vilitarajiwa kuwa ni vyama mbadala kwa CCM katika kushika hatamu ya uongozi.

Kutokana na ukaguzi huo upungufu uliobainika ni kuwa, vyama vya CHADEMA na CCM vimepewa hati zenye shaka huku Chama cha Wakulima (AFP), ADC, Demokrasia Makini, Chama cha Kijamii, NLD, Sauti ya Umma na TLP vikipata hati mbaya na ACT ikiwa haijaoneshwa kabisa. Watanzania wengi wameelekea kupoteza kabisa hata ile imani ndogo walioanza kuijenga juu ya Vyama hivi vilivyojinasibu kuwa vingeweza kuwa mbadala wa  CCM katika uadilifu na uwajibikaji sambamba na kuwasemea Wananchi Changamoto zao na kushiriki katika kuzitafutia majawabu kwa wakati.

Ukipima mwenendo wa vilivyokuwa vyama vya upinzani ( mawazo mbadala ) katika nchi kadhaa zikiwemo Ghana, Nigeria na Gambia ambapo wananchi wameviamini na kuvipa nafasi ya madaraka ya kuunda serikali ni tofauti kabisa na hapa kwetu Tanzania.

Mfano tukianzia nchini Nigeria Chama cha upinzani cha All Progressive Congress ( APC ) cha Bwana Muhammad Buhari kilifanikiwa kumuondoa Bwana Goodluck Jonathan wa kilichokuwa Chama tawala Cha People's Democratic Party ( PDP ) baada ya Chama Chama APC kuishi kwa vitendo uadilifu na uwajibikaji na kwa miaka yote Chama hicho hakikuwahi kukumbwa na kashfa za matumizi mabaya ya fedha wala Rushwa katika kuyaendea Madaraka. APC kilisimamia ajenda kuu mbili yaani kuisimamia kwa uadilifu Sekta ya Mafuta ambayo kwa kipindi kirefu iliandamwa na rushwa na kutokomeza Boko Haram ambapo kwa kiasi kikubwa Chama tawala cha PDP kilikiri kushindwa.

Tukiangazia nchini Ghana, ambapo mara kwa mara vyama vya Siasa hukaguliwa mapato na matumizi ya fedha, Chama cha kikuu cha upinzani wakati huo cha NPP kilijijengea umaarufu kwa kuibuka na hati safi kwa miaka mitatu mfululizo kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Desemba 2016 dhidi ya Chama cha NDC kilichokuwa tawala. Hii ilipelekea wananchi wapate mbadala wa uadilifu na uwajibikaji hivyo kupelekea Chama Cha NPP kilichokuwa pinzani cha Bwana Akuffor Addo kuibuka kidedea dhidi ya Chama tawala cha NDC cha Bwana John Mahama.

Hii ni changamoto kubwa hapa kwetu Tanzania  kwa vyama vya upinzani, kwa maana katika uanzishwaji wa vyama vingi mwaka 1992 wananchi walikuwa na matarajio makubwa na miaka inaenda bado hawajaona na kufahamu muelekeo wa vyama hivi na msimamo wao katika fedha ndogo wazipatazo kama ruzuku kutoka katika kodi za wananchi. Kutokana na ripoti ya CAG inaonesha ni kwa jinsi gani katika vyama hivi nidhamu ilivyokuwa ndogo ya matumizi ya Ruzuku. Swali dogo wananchi wanajiuliza " kama hichi kidogo wakipatacho hakina uwazi, je siku wakiunda serikali waanze kupata fedha nyingi itakuwaje? Na hapo hapo waumini wanasema kutoka katika vitabu vya dini kuwa Mtu asiyeaminika kwa kidogo kamwe asipewe kikubwa". Sasa hili nakuachia wewe msomaji uchambue.

Kwa upande mwingine tuangazie Vyama vya upinzani ambavyo vimeundwa hivi karibuni  katika Nchi za kusini mwa bara la Afrika na namna vinavyofanya kazi na kujitanabaisha kwa wananchi wake.

Kwa  ufupi tuitazame Afrika ya kusinina Chama cha Economic Freedom Fighter ( EFF ) cha kiongozi kijana na mwanaharakati aliyejitoa kutoka Chama tawala cha ANC Bwana Julius Malema. Chama hichi kichanga ni tofauti kidogo na vyama changa vya hapa kwetu Tanzania kwa kutazamia malengo ya Chama na walengwa wa Chama hicho. Chama hichi kimeundwa mwaka 2013 kwa sasa kimejizolea umaarufu mkubwa na uchaguzi uliyopita wa mwaka 2014 kimefanikiwa kupata viti vya ubunge kwa asilimia sita ( 6% ) yaani viti 25 bungeni.

Hii ni kwa sababu chama kimewalenga zaidi wanyonge kwa kupigania haki za masikini, wachimbaji wadogo wa madini Afrika ya kusini na kujitanabaisha hadharani kutetea haki za wasionacho na wengi wa wasionacho Arika ya kusini ni watu weusi. Hii inafanya Chama kufahamika dhahiri msimamo wake na wepi walengwa wa  chama na kwa maslahi ya watu gani.

EFF kwa sasa kinaheshima kubwa si kwa sababu ya harakati ila ni kutokana na msimamo wake katika matumizi ya fedha na zaidi kutoyumbishwa kwa kudandia hoja na kufanya kuwa tofauti kabisa na vyama vingi vya upinzani hapa Tanzania na imepelekea kukipa ushindani mkubwa Chama tawala cha ANC kwa sasa ingawa wananchi wengi bado wanaimani kubwa na ANC wakikumbuka kazi kubwa iliyofanywa na chama hicho mpaka kuifikisha Afrika kusini hapo ilipo sasa.

Baada ya ripoti ya CAG vyama mbalimbali vimeibuka kila chama kikichukuwa njia yake kukabiliana na ripoti hiyo.

CCM wamejifafanua kupitia kwa katibu mwenezi wa Chama hicho Bwana Humphrey Polepole kwa kutolea maelezo na ufafanuzi juu tuhuma mbalimbali zilizowekwa katika ripoti hiyo ikiwemo milioni 80 zilizohamishwa kuingia CCM kutoka Kampuni ya Jitegemee na shilingi milioni 300 zilizochukuliwa na Chama kutoka mfuko wa watumishi wastaafu wa CCM. Nukuu" CCM ina Kampuni yake ya Jitegemee na fedha hizo ziliingizwa katika chama kama gawio na hufanyika hivo mara zote, kuhusu milioni 300 CCM inamfuko wake kwa wastaafu na fedha huchukuliwa na kurudishwa, kila mwezi huwekwa 25 milioni kwa ajili ya wastaafu wetu watumishi na viongozi", alisema Polepole.

Baada ya ufafanuzi huo Polepole alihitimisha kwa kuipongeza Taasisi ya CAG kwa kufanya kazi nzuri nukuu "sisi kama Chama Cha Mapinduzi tunaipongeza taasisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa kufanya kazi nzuri na yenye tija kwa Watanzania na tumepata somo kubwa" alisema Bwana Polepole.

Kwa upande wa CHADEMA kupitia kwa msemaji wake Bwana John Mrema nao waliitisha vyombo vya habari, ila kidogo hali ilikuwa  ni tofauti kwa kuwa  kwa kiasi kikubwa waliishutumu taasisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ( CAG) mbali na fedha shilingi milioni 700 zenye utata wa matumizi yake, pia alihoji matumizi ya sh 2.3 bilioni mbazo ni makusanyo ya CHADEMA kwa mwaka 2015/ 2016 fedha ambazo zinadaiwa kutopelekwa benki na matumizi yake kushindwa kuelezeka.
Msemaji wa CHADEMA bwana John Mrema aliishutumu kwa kiasi kikbwa Ofisi ya CAG kwa madai kuwa  haitendi haki, nukuu "Ofisi ya CAG haijatutendea haki sisi CHADEMA kwa sababu fedha hizo zilipelekwa benki ila kwa kuchelewa na kwa mafungu mafungu" alisema Mrema.

Ripoti hii ya CAG inakuja kipindi ambapo Chama Cha Mapinduzi CCM  kinaendelea kujifanyia mageuzi makubwa ya kiuongozi, kimuundo na kimfumo (tofauti na vyama vya  upinzani ambavyo vinaonekana bado havijajua cha kufanya) yenye lengo la kukifanya Chama kuwa Chama cha wanachama na chenye kushughulika na shida za watu ambapo kwa mujibu wa Viongozi wakuu wa Chama hicho wakiongozwa na  Mwenyekiti ambaye ndio Rais Ndg. John Joseph Pombe Magufuli, Makamu wa Mwenyekiti Bara na Zanzibar, Katibu Mkuu , Naibu katibu Mkuu bara na Zanzibar mageuzi hayo walipitishwa mwaka 2017 katika mkutano Mkuu wa Chama hicho.

Sekretarieti yote ya Chama nayo ipo mstari wa mbele katika   kuyavumisha kwa vitendo na kupelekea wananchi kwa kiasi kikubwa kuvutiwa na mageuzi hayo yenye kuleta nidhamu ya matumizi ya fedha kama alivyo shauri CAG hivi karibuni, kuwa karibu na wananchi na kuzijua na kushiriki kuziondoa shida zao hivyo kufanya mageuzi haya makubwa kuaksi  utendaji kazi wa Mwenyekiti na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania Ndg John Joseph Pombe Magufuli na hivyo kufanya kutokuwa na mbadala wa  CCM kiuongozi hapa Tanzania kwa miaka mingi ijayo.

Mungu ibariki Tanzania,
Mungu mbariki Rais wetu,
Hapa kazi tu.

Na mwandishi wako,
Said Said Nguya.
CAG: HAKUNA MBADALA WA CCM TANZANIA. CAG: HAKUNA MBADALA WA CCM TANZANIA. Reviewed by KUSAGANEWS on April 22, 2018 Rating: 5

No comments: