Baba yake Nondo afunguka sakata la uraia wa mwanaye

Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu uraia wake, baba yake Omar Nondo amefunguka kuhusu uraia wa mtoto wake

Nondo ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amejikuta kwenye misukosuko na vyombo vya dola tangu alipotoweka katika kile kilichoelezwa kuwa ni katika mazingira ya kutatanisha Machi 6 na kuonekana Machi 7 wilayani Mufindi, Iringa

Baada ya Nondo kuripoti polisi mjini Mafinga alishikiliwa na jeshi hilo Mkoa wa Iringa na na baadaye kukabidhiwa kwa Polisi Kanda 

Maalumu ya Dar es Salaam ambako kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema kupitia uchunguzi wa kisayansi, wamebaini kuwa hakuwa ametekwa, bali alijiteka na tayari suala lake lipo mahakamani, Iringa

Jana mzazi wa mwanafunzi huyo alijitokeza kuzungumzia suala la uraia wa mtoto wake na kueleza kwamba, baba yake (yaani babu wa Nondo) alizaliwa mwaka 1919 huko Ujiji, Kigoma na kuwa ni miongoni mwa waasisi wa chama cha Tanu
Mzee Omar, alisema baba yake huyo aliyemtaja kwa jina la Omar Kagobe alipata watoto 30, mmoja akiwa yeye
“Nashangaa hao wanaomkamata na kumhoji mtoto wangu kuwa sio raia, wananichekesha sana kwa kuwa najua mwisho wa siku watajua ukweli wake

‘Ukweli ni kwamba wazazi wangu ndio waasisi wa Tanu na walishiriki kikamilifu katika kupigania uhuru wa nchi hii, hivyo suala hilo halinipi wasiwasi wala hofu na hivyo vyeti wanavyovitaka mbona vipo tu, ila waelewe kuwa sisi ni Wamanyema halisi na ni raia halali wa nchi hii,” alisema

Pia alisema babu yake Nondo, alishawahi kuwa Polisi kwa miaka 18 kuanzia mwaka 1940 hadi 1958 na alishafanya kazi huko Mabatini mkoani Mwanza na sehemu nyingine za nchi

Alisema babu yake Nondo akiwa polisi, ndipo zilipoanzishwa Kota za Msimbazi, Dar es Salaam na jina lake lilikuwa maarufu, akijulikana kama Mzee Kagobe

Kama haitoshi alisema bibi yake Nondo alikwenda kuhiji, mnamo 1970 na alipewa hati ya kusafiria ya Tanzania, huku akihoji, “Kama angekuwa sio raia wa Tanzania angepewaje hati hiyo?”

Hata hivyo, alibainisha kuwa anachopitia mtoto wake kwa sasa ikiwamo kuitwa na Idara ya Uhamiaji, ni jambo linalotengezwa na mtu binafsi

Juzi, Mwenyekiti wa ACT - Wazalendo, Mkoa wa Kigoma, Sendwe Mbaruku, alitoa taarifa kuhusu suala la Nondo kuhojiwa na uhamiaji na kusema; “Kijana Abdul ni mtoto wetu hapa Kigoma, wazazi wake ni wakazi na wapiga kura wa hapa Ujiji, zaidi ni Watanzania wenzetu.”
Hivi karibuni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alituma taarifa kwenye mitandao ya kijamii akisema kwamba atawashtaki kwa wazee wa Ujiji wale wote wanaohoji uraia wa kijana huyo.
Taarifa za kuhojiwa kwa Nondo zilitolewa Machi 4 na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kupitia ofisa wake wa utetezi na ushwishi, Leopald Mosha

Mosha alisema kwamba Nondo aliitwa katika ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam zilizopo kwenye ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani na kuhojiwa kwa saa mbili kuhusu taarifa zake za uraia
Pamoja na kuwasilisha taarifa za wazazi wake, alisema kijana huyo ametakiwa pia kuwasilisha vyeti vya kuzaliwa vya babu na bibi yake wa pande zote mbili ifikapo Aprili 20 mwaka huu.
Baba yake Nondo afunguka sakata la uraia wa mwanaye Baba yake Nondo afunguka sakata la uraia wa mwanaye Reviewed by KUSAGANEWS on April 07, 2018 Rating: 5

No comments: