Askofu Lebulu, Mghwira watoa neno mazishi ya mapadri watatu Mwanga

Askofu Mkuu wa Jimbo kuu Katoliki la Arusha, Isaac Amani, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira na Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule jana walishiriki katika ibada ya mazishi ya mapadri watatu waliofariki mfululizo kwa matukio tofauti

Mapadri hao, Ulbadius Kidavuri, Arbogast Mndeme na Michael Kiraghenja walizikwa jana katika makaburi ya mapadri, yaliyopo Chanjale, wilayani Mwanga

Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Josephat Lebulu alieleza jinsi alivyopokea kwa mshtuko taarifa za vifo hivyo vilivyotokea mfululizo

Hata hivyo, aliwaambiwa waombolezaji kuwa, “Tunajua yaliyotokea yanauma sana hivyo kuweni na matumaini.”
Aliwataka waumini kuomboleza na kulia kwa matumaini
“Nilipompigia simu ndugu yangu Askofu Rogath Kimario (wa Jimbo Katoliki Same) kumpa pole kuhusiana na kifo cha Padri Kiraghenja, aliniambia kuna msiba mwingine umetokea wa pili wa Padri Mndeme ambaye alifariki dunia April 12. Akanambia unafikiri ni vifo hivyo tu, kuna msiba mwingine tena wa Padri Kidavuri uliotokea Kurasini Dar es Salaam. Kwa kweli nilisikitika sana,” alisema akisimulia jinsi alivyopoata taarifa za vifo hivyo

Katika salamu zake za pole, Mghwira alisema vifo vya mapadri hao ni pigo kubwa kwa jimbo hilo kwani ni watumishi ambao walikuwa wakitegemewa na jamii

“Kwetu ni pigo kubwa kuwapoteza mapadri watatu kwa mpigo. Hawa ni viongozi wa kijamii ambao tunawahitaji sana katika jamii zetu,” alisema Mghwira
Kuhusu vifo vya mapadri hao
Padri Kiraghenja alikuwa Paroko wa Kanisa la Kirangare, Moshi na alifariki dunia Aprili 11 baada ya kujisikia vibaya, kisha kunywa dawa ya maumivu. Alifariki akiwa usingizini

Padri Mndeme alikuwa katika Parokia ya Lembeni, Mwanga. Alifariki dunia Aprili 13 akiwa kwenye uchunguzi wa matibabu Hospitali ya KCMC baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe wa saratani ya utumbo mpana
Padri Kidavuri alikuwa Katibu Mtendaji wa Utume wa Walei katika Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC). Alifariki dunia Aprili 13 kwa shinikizo la damu baada ya kupata taarifa za vifo vya wenzake
Askofu Lebulu, Mghwira watoa neno mazishi ya mapadri watatu Mwanga Askofu Lebulu, Mghwira watoa neno mazishi ya mapadri watatu Mwanga Reviewed by KUSAGANEWS on April 18, 2018 Rating: 5

No comments: