BAADHI WANAWAKE WAMTUHUMU AFISA MAENDELEO ARUSHA KWA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA VIKUNDI VYA AKINA MAMA MBELE YA MWENYEKITI WA UWT"


Wanawake wafanyabiashara wadogo wadogo katika kata ya Nduruma halmashauri ya Arusha waliokuwa wamejiunga na vikundi kwa ajili ya kusajiliwa katika ofisi za kata ili watambuliwe rasmi kwa ajili ya kupatiwa mikopo na Halmashauri ya  Arusha wamemtuhumu afisa maendeleo wa kata hiyo kwa kuwarubuni fedha ili wasajiliwe.

Akina mama hao wakitoa malalamiko yao mbele ya mwenyekiti wa UWT mkoa wa Arusha Yasmini Bachu katika ziara yake ya kutembelea wafanyabiashara wanawake katika Soko la Lokii lililopo kata ya Bwawani wamesema wamejiunga katika vikundi vine ambavyo ni Kutoka vitongoji vya Oldendereti,Nguuni,Nduruma kati na Samaria.

Mmoja wa akina mama hao amesema kuwa afisa huyo alikuwa amewataka wanawake hao kutoa kiasi cha shilingi elfu 65 kila kikundi ili kuwasaidia kusajili vikundi hivyo na mpaka sasa bado havijasajiliwa na afisa huyo amehamishwa hali ambayo inawafanya wasijue hatma yao.

Akitolea ufafanuzi madai hayo Bachu amesema kuwa atayafikisha kwenye mamlaka husika akiwemo mkurugenzi wa halmashauri hiyo kwa kuwa ndiye mwenye dhamana kuhusu watumishi wake.

Bachu amesema kuwa jambo hilo halikubaliki kwasababu wao kila siku wanatoa elimu kwa akinamama kuunda vikundi ili wapate mikopo lakini inashangaza kama ni kweli afisa jambo hillo linarudisha nyuma maendeleo akina mama.

“Mimi kama kiongozi wa wanawake suala hili niwahakikishie akina mama nitalifanyia kazi na tumjue vizuri afisa huyo amekula pesa zenu na atashughulikiwa mana hii serikali ya Raisi Magufuli haitaki Mchezo mchezo tena pesa ya wanyonge sasa nitawajibu hivi karibuni na nitamshirikisha mkurugenzi wenu kwasababu ni mtu msikivu atalishughulikia mana ni mtu asiyependa mchezo”Alisema Bachu

Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri hiyo Dokta Wilsoni Mahera Charles amesema kuwa hakuwahi kusikia madai hayo lakini akaniomba niwasiliane na mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii na kisha baadae Mkurugenzi huyo atalitolea maelezo zaidi baada ya mimi kupata majibu kutoka kwa afisa huyo.

Baada ya kupata maelezo ya mkurugenzi akatoa namba za simu ili kumtafuta mkuu wa idara Bi Angela Mvaa kujibu tuhuma za mtumishi wake katika idara hiyo

Kwa upande wa afisa huyo wa halmashauri ya Arusha Bi Angela amesema kuwa malalamiko hayo hayajawahi kufika kwake na kata hiyo ina mtaalamu na huenda kuna jambo zaidi ya hivyo wanawake hao walivyotoa tuhuma.

“Ndiyo maana nasemaje wewe mwandishi uzuri ni mtaalamu pia kwenye fani yako mpaka mtu afike kwa mkurugenzi wako ina maana kuna boss zaidi namaana anatakiwa apewe taarifa sasa kama mtendaji amejua hawa wamama wanatakiwa waje kwangu kwahiyo ukichunguza kuna jambo zaidi ya hilo Mimi siwezi kukataa kweli labda malalamiko hayo  yapo sitaki kuprove inawezekana hela yao imechukuliwa lakini saa ingine wanazungumza tu hivyo labda hiyo mikopo hawajawahi kuomba au hawajakidhi vigezo au wanaona kwasababu kama mikopo ni ya akina mama kwasababu inawataja wanadhani labda watapelekewa nyumbani kwao “Amesema Mratibu Angela

Afisa huyo amesema kuwa licha ya kuwa afisa huyo amekula pesa ama hajala lakini ameshangazwa wanawake hao kulalamika katika ziara ya kiongozi ile hali yeye yupo ambaye ni msimamizi wa idara.

“Kwasababu watu wasitumie hiyo kuchafua majina ya watu na siwezi kutetea mtu na kwanini wasije ofisini wasubiri ziara nduruma ni kubwa sasa mimi nitalifuatilia kwa nani wamama ni wengi aah si lazima nijue ni kikundi gani kilicholiwa fedha zao nitamfuatilia mtendaji mpaka na kwanini umekiri kwa muandishi na viongozi yeye pia hatoshi kwasababu mtendaji akipelekewa malalamiko si anatakiwa ayapeleke kwenye ngazi husika yani hapo mtendaji ana kosa na hao waliolalamika mwenyewe wana makosa”Alisema afisa maendeleo

BAADHI WANAWAKE WAMTUHUMU AFISA MAENDELEO ARUSHA KWA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA VIKUNDI VYA AKINA MAMA MBELE YA MWENYEKITI WA UWT" BAADHI WANAWAKE WAMTUHUMU AFISA MAENDELEO ARUSHA KWA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA VIKUNDI VYA AKINA MAMA MBELE YA MWENYEKITI WA UWT" Reviewed by KUSAGANEWS on March 03, 2018 Rating: 5

No comments: