Wanafunzi wavamia nyumba ya mwalimu na kufanya uharibifu mkubwa

Shule ya Sekondari Lyamungo  iliyoko Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imefungwa kwa muda wa wiki mbili baada ya kutokea vurugu zilizosababisha uharibifu wa nyumba ya mwalimu wa nidhamu wa shule hiyo, Safari Rasin.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo, aliyoitoa leo Machi 1, 2018 imesema  shule hiyo imefungwa kuanzia leo baada ya wanafunzi zaidi ya 400 kuvamia nyumba ya mwalimu wao wa nidhamu na kufanya uharibifu, kwa madai kuwa amekuwa akiwatukana matusi ya nguoni jambo ambalo limekuwa likiwakera.

Amesema Februari 27, 2018 wanafunzi hao walikuwa na uchaguzi wa Serikali ya wanafunzi na mmoja wao aliandika matusi kwenye karatasi ya kura, hali ambayo iliwafanya walimu kuwataka kila mmoja achukue karatasi yake ili kumbaini mhusika.

Amesema karatasi zilichukuliwa na ikabaki moja iliyoandikwa matusi,huku mwanafunzi mmoja  akikosa kataratasi yake aliyopigia kura,na katika kufuatilia walibaini ni mwandiko wa mwanafunzi huyo, ndipo taratibu za kinidhamu zikachukuliwa ikiwa ni pamoja na kusimamishwa shule.

Aidha alisema mwanafunzi aliyeandika matusi, aliadhibiwa kwa kusimamishwa kuendelea na masomo kwa muda,hali ambayo iliibua taharuki kwa wanafunzi wenzake na kutoka kwenda kuvamia nyumba ya mwalimu wa nidhamu, kwa madai kuwa yeye ndiye amekuwa akiwatolea matusi hayo.

Akizungumzia tukio hilo kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Hamisi Issah amesema tukio la uvamizi wa nyumba ya mwalimu na kufanya uharibifu wa mali, lilitokea Februari 28, 2018 saa 4:00 asubuhi katika eneo la shule hiyo.

Amesema miongoni mwa mali zilizoharibiwa ni milango, madirisha, mabati pamoja na migomba yote inayozunguka nyumba hiyo ambayo iko eneo la shule

“Wanafunzi walikuwa zaidi ya 400, na walichokifaya walipasua vyoo vyote vya nyumba kwa mawe kukata milango,kuharibu bati na kukata migomba inayozunguka nyumba hiyo,na chanzo wanadai kuwa mwalimu huyo amekuwa akiwatukana matusi ya nguoni,” amesema.



Wanafunzi wavamia nyumba ya mwalimu na kufanya uharibifu mkubwa Wanafunzi wavamia nyumba ya mwalimu na kufanya uharibifu mkubwa Reviewed by KUSAGANEWS on March 01, 2018 Rating: 5

No comments: