TRC yakitolea maelezo kichwa cha treni kilichopata ajali

Shirika la Reli Tanzania (TRC), limekanusha kwamba kichwa cha treni kilichopata ajali mwishoni mwa wiki ni miongoni mwa vilivyotelekezwa bandarini.

Ofisa uhusiano wa shirika hilo, Mohammed Mapondela alisema jana kwamba taarifa hizo ambazo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii hazina ukweli.

Katika ajali hiyo, watu 21 walijeruhiwa baada ya treni ya abiria iliyokuwa ikitokea Tabora kuelekea Kigoma kupata ajali eneo la Malagarasi wilayani Uvinza

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Otieno alisema kwamba ajali hiyo ilitokea Februari 27 saa nane mchana.

Katika ajali hiyo, kichwa cha treni kiliacha njia na kuanguka pamoja na mabehewa mawili.

Akifafanua kuhusu kichwa hicho Mpondela alisema, “Watu wanashindwa kuelewa kuwa kichwa kilichopata ajali ni 9001 ambavyo ni vya awamu ya kwanza, hivi vilivyopo bandarini pamoja na kwamba Serikali imeshavinunua bado havijaanza kutumika.”

Kuhusu ripoti ya ajali hiyo alisema bado haijatoka na kwamba wataalamu wanaendelea na uchunguzi. Awali, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema TRC inahitaji vichwa vya treni 47 ambavyo kama havitapatikana jitihada za kusafirisha mizigo zitashindikana.

 “Sasa tunavyo 29 na kama hatutaendelea kupata vingine, jitihada za kusafirisha mizigo kwenda nje ya nchi ikiwamo Uganda hazitafanikiwa. Tumenunua vichwa vingine kumi na moja na mchakato wa kulipia unaendelea na baada ya hapo vitaanza kutumika,” alisema.





TRC yakitolea maelezo kichwa cha treni kilichopata ajali TRC yakitolea maelezo kichwa cha treni kilichopata ajali Reviewed by KUSAGANEWS on March 04, 2018 Rating: 5

No comments: