Chama tawala nchini Uganda, National
Resistance Movement (NRM) kinashinikiza kuwe na kura ya uamuzi ambayo itaongeza
kipindi cha utawala wa Rais Yoweri Museveni hadi mwaka 2035.
Shinikizo hili la kutaka rais awe akiongoza
kwa vipindi viwili vya miaka saba badala ya miaka mitano limepingwa na viongozi
wa upinzani ambao wamesema ni njama ya kufanya rais huyo aongoze hadi kifo
Msemaji wa NRM, Rogers Mulindwa
amesema lazima kura ya uamuzi ifanywe mwaka 2018. Desemba 2017, Bunge liliondoa
sehemu ya sheria iliyozuia watu wenye umri wa miaka 75 na zaidi kugombea urais.
Rais Museveni mwenye miaka 73 ameongoza
taifa hilo tangu mwaka 1986 na sasa amekubaliwa kugombea tena wadhifa huo mara
mbili baada ya kipindi chake kukamilika mwaka 2021
Museveni, miongoni mwa viongozi Afrika ambao
wametawala kwa muda mrefu zaidi, pia ni mmoja wa viongozi wa mataifa ya
Afrika ambao wamekuwa wakijitahidi kubakia madarakani kwa kubadilisha Katiba.
Kutokana na wabunge wa Uganda kubadili
sheria ili wawe wakiongoza kwa miaka saba badala ya mitano, chama tawala
kinasema kipindi cha uongozi wa rais pia kinafaa kuongezwa hadi miaka saba ili
kuwe na uwiano katika chaguzi zote.
Shinikizo la kuandaa kura ya uamuzi
linakabiliwa na pingamizi la kisheria kutoka kwa wanaharakati na baadhi ya
viongozi wa upinzani ambao wanasema linakiuka Katiba.
Ingawa Rais Museveni amewahi kukaririwa
akieleza anavyochukizwa na viongozi wa Afrika wanaotaka kubaki madarakani kwa
muda mrefu kupita kiasi, amekuwa akijitetea kwamba alimaanisha wale wanaotawala
bila kuchaguliwa na wananchi.
MUSEVENI ATAKA KUONGOZA MPAKA MWAKA 2035
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 01, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment