Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi na Usalama (JWTZ), Jenerali Venance Mabeyo amewataka Watanzania
kujiepusha na vitendo vinavyoweza kutishia usalama wa nchi na kuharibu tunu ya
amani iliyopo.
Ameeleza kuwa hivi
sasa vipo viashiria vinavyotishia usalama wa nchi, na kwamba hatua
zinachukuliwa ili kudhibiti hali hiyo.
Jenerali Mabeyo
amewaomba Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli
dhidi ya wizi, ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi za umma, kwa kuwataja
hadharani watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Ametoa kauli hiyo jana
wakati akifunga Maadhimisho ya Tamasha la Mashujaa wa Vita ya Majimaji katika
Viwanja vya Makumbusho ya Mashujaa wa Vita ya Majimaji mjini Songea.
Mabeyo amesema vita
dhidi ya wizi na ufisadi, iliyoanzishwa na Rais Magufuli, si ya mtu mmoja, bali
kila Mtanzania anapaswa kushiriki, kwani mali zinazoibwa na baadhi ya Watanzania,
zinapaswa kuwanufaisha watu wote.
Mabeyo alisema badala
ya kushughulika na uvunjifu wa amani, ipo haja ya Watanzania kuunga mkono
juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo imedhamiria
kuwatumikia wananchi kwa kuboresha huduma za kijamii ili kutoa fursa kwa
wananchi kutumia muda wao kufanya kazi za kujiletea maendeleo.
Ametaja baadhi ya
mambo yanayotishia usalama wa nchi kuwa ni matumizi mabaya ya utandawazi ambayo
mbali na ya kuharibu utamaduni wa nchi, baadhi ya watu wanaitumia vibaya kwa
kuhamasisha wananchi kufanya na kushiriki katika matukio ambayo yanaashiria
uvunjifu wa amani na utulivu uliopo nchini kwa muda mrefu.
Jenerali Mabeyo
alitaka shule za msingi, sekondari na vyuo nchini, kufundisha wanafunzi umuhimu
wa kulinda, kutunza amani na wananchi kuishi kwa kupendana, badala ya kutumia
muda wao kutafuta sababu za kutengana, jambo ambalo halina tija kwa taifa.
Wakati huo huo,
Jenerali Mabeyo aliitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuboresha Makumbusho ya
Mashujaa wa Vita ya Majimaji ili yatumike kwa ajili ya utalii na kuliingizia
taifa fedha nyingi.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma, Chiristina Mndeme alisema Serikali ya Mkoa wa Ruvuma, itaongeza nguvu
katika kulinda mipaka yake ili wananchi wa mkoa huo waweze kuendelea na kazi za
uzalishaji mali.
Mkuu wa Majeshi "Kuna Viashiria vinavyotishia Usalama wa Nchi,
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 01, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment