ACT WAZALENDO NGOME YA WANAWAKE WASHTUSHWA WATAKA KUUNDWA TUME HURU

Kufuatia mfululizo wa matukio ya kupotea, utekaji na mauaji ya watu Ngome ya Wanawake wa chama cha ACT Wazalendo imetaka kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi wa matukio hayo.

Pia, imetaka kurejewa kwa mchakato wa Katiba mpya ambayo wanadhani itakuwa ni jawabu kwa changamoto nyingi zinazojitokeza nchini.

Akitoa tamko la wanawake wa chama hicho leo Machi 1, 2018, Mwenyekiti wa ngome hiyo, Chiku Abwao amesema wamesikitishwa na hali ya kisiasa nchini ambayo inawafanya wananchi waishi kwa hofu kubwa.

Abwao amesema matukio hayo yanaashiria kupotea kwa utu na usawa wa binadamu, tishio kwa vyama vya upinzani, uhuru wa maoni pamoja na amani na usalama wa nchi

"Matukio ya watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha, kutekwa na kuteswa sasa yamekuwa sehemu ya maisha ya watanzania. Hali hii haikubaliki, tumejitokeza kukemea ili kulinusuru taifa na hatari inayoendelea," amesema Abwao.

Kiongozi huyo amebainisha kwamba mchakato wa uchaguzi nao umekuwa kama mchezo wa kuigiza.

Amesema wanaikumbusha Serikali kwamba mfumo wa vyama vingi ni takwa la kikatiba na kisheria na haliwezi kuondolewa kwa matakwa binafsi ya kiongozi yoyote

"Tunataka serikali ihuishe mchakato wa katiba mpya kutoka pale ilipoishia Tume ya Jaji Warioba. Wadau na wananchi wote tuungane pamoja kudai katiba mpya ili kulinusuru taifa letu," amesema Abwao.

Mwenyekiti huyo aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu (Chadema) katika Bunge lililopita, amesisitiza kwamba mfumo wa vyama vingi uachwe ufanye kazi yake kwa mujibu wa Katiba na kitendo cha vyombo vya dola kuingilia hakikubaliki  
ACT WAZALENDO NGOME YA WANAWAKE WASHTUSHWA WATAKA KUUNDWA TUME HURU ACT WAZALENDO NGOME YA WANAWAKE WASHTUSHWA WATAKA KUUNDWA TUME HURU Reviewed by KUSAGANEWS on March 01, 2018 Rating: 5

No comments: