Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu imemsomea maelezo ya awali mkurugenzi mkuu wa zamani wa
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando anayekabiliwa
na mashtaka matano likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka.
Kabla ya
kusomewa maelezo leo Februari 28,2018 mbele ya Hakimu Mfawidhi, Victoria
Nongwa, Wakili wa Serikali Dismas Mganyizi, alimkumbusha mashtaka yanayomkabili
Tido anayetetewa na wakili Ramadhani Maleta.
Baada ya
kusomewa, Tido ambaye yuko nje kwa dhamana amekubali maelezo binafsi na kwamba
alikuwa mkurugenzi mkuu wa TBC mwaka 2006 hadi 2010.
Amekubali kuwa
alikuwa msimamizi wa shughuli za TBC lakini si zote.
Pia amekubali
kutoa maelezo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kuwa
alifikishwa mahakamani Januari 26,2018.
Tido amekana
mashtaka yanayomkabili na upande wa mashtaka katika kesi hiyo utaanza kutoa
ushahidi Machi 28,2018.
Anakabiliwa na
mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali
hasara ya Sh887.1 milioni.
Tido anadaiwa
Juni 16,2008 akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), akiwa mkurugenzi
mkuu wa TBC kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa
kuendesha na kutangaza vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group
Corporation (BV1) bila kupitisha zabuni kinyume cha sheria ya ununuzi, hivyo
kuinufaisha BVl.
Katika shtaka
la pili anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake ikielezwa Juni 20,2008 alisaini
makubaliano ya utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.
Tido katika
shtaka la tatu anadaiwa Agosti 11,2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai alitumia
vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano ya ununuzi, usambazaji,
kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na
kuifaidisha BVI.
Shtaka la nne,
anadaiwa Novemba 16,2008 akiwa Dubai alitumia vibaya madaraka yake kusaini
mkataba wa makubaliano ya kuendesha miundombinu ya utangazaji kati ya TBC na
BVI na kuinufaisha BVI.
Tido katika
shtaka la tano anadaiwa kati ya Juni 16 na Novemba 16,2008 akiwa Dubai
aliisababishia TBC hasara ya Sh887.1 milioni.
Tido Mhando asomewa maelezo ya awali
Reviewed by KUSAGANEWS
on
February 28, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment