Jinsi saa mbili zilivyotumika kumpeleka Sugu gerezani miezi 5

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imetumia takriban saa mbili kutoa hukumu iliyowapeleka jela miezi mitano Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite alianza kusoma hukumu saa 3:32 asubuhi hadi saa 5:20 asubuhi jana na kuwatia hatiani washtakiwa na baadaye kuwahukumu kutumikia adhabu hiyo akisema amejiridhisha pasipo shaka kwamba walitenda kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli

Washtakiwa walidaiwa kutenda kosa hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Desemba 30, 2017 katika eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Hakimu Mteite alisema mahakama ilijielekeza katika viini (hoja) vikuu kadhaa katika kesi hiyo hadi kufikia hatua ya kutoa uamuzi.

Kwanza mahakama ilijiuliza maswali kadhaa katika kesi hii, je ni kweli washtakiwa walitamka maneno hayo? Je maneno hayo yanabeba maana ya ‘abusive word’ (maneno ya fedheha

“Je, maneno hayo yalimlenga nani? Na mwisho je maneno hayo yangeweza kuleta hali ya uvunjifu wa amani? Yalimlenga nani? Lakini pia je, wana hatia au hawana hatia?” alisema Hakimu Mteite
Maelezo ya hukumu

Hakimu Mteite alianza kwa kutoa maelezo ya ushahidi uliotolewa na mshtakiwa wa pili (Masonga) kwamba katika ushahidi wake alijikita zaidi kusema siku ya mkutano hakuhudhuria.

Hakimu Mteite alisema mahakama haikuona sababu ya kuuchukulia kwa uzito ushahidi huo kwa kuwa aliutoa wakati upande wa mashtaka ukiwa umemaliza na kufunga ushahidi wake. Alisema Masonga alipaswa kuuwasilisha awali wakati wa utetezi.

Alisema, “Utetezi wa mshtakiwa wa pili uliegemea kwamba hakuwepo kwenye mkutano huo, alitoa utetezi kwamba hakuhudhuria kwa vile alipigiwa simu na mke wake Grace Mallya kuwa anaumwa, hivyo arudi nyumbani na alipofika hakutoka kwenda popote.”

“Alipaswa kutoa maelezo ya kutokuwepo eneo hilo awali kabla upande wa mashtaka haujafunga ushahidi wake. Ikumbukwe kwamba mshtakiwa huyu tangu awali alikuwa na mawakili watano, lakini mawakili wote hawa hawakuitaarifu mahakama kwamba mshtakiwa wa pili ataegemea upande fulani katika utetezi wake.

Hivyo mahakama haitaupa uzito utetezi wa mshtakiwa huyu kwamba hakuwepo eneo la tukio siku hiyo.”

Akijikita katika viini alivyovitaja awali katika utoaji hukumu hiyo, Hakimu Mteite alisema uhalisia unaonyesha washtakiwa walitamka maneno hayo kulingana na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa pili, tatu na wa tano

“Mashahidi wa pili, tatu na watano walikuwa ni wa kuona na kusikia. Hivyo, katika kesi hii hakuna ubishi kwamba mashahidi hawa walitoa ushahidi wa kuona na kusikia,” alisema.

Alisema mahakama inaamini washtakiwa walitoa maneno hayo ambayo ni ya fedheha na yalimlenga Rais kwa kuzingatia baadhi yaliyotamkwa
“Mashahidi walisema maneno yale yalimlenga Rais John Magufuli. Na hapa ni kweli unapozungumzia masuala ya kitaifa kama maneno ya kutekwa, kuuawa watu ni masuala ya kitaifa, hivyo haiwezi kuwa Rais Magufuli mwingine na hata washtakiwa wenyewe walikuwa wanatamka ‘Rais wetu Magufuli’ hii inatosha kwamba aliyelengwa katika maneno yale ni Rais Magufuli,” alisema.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mteite alisema mahakama imejiridhisha kwamba Sugu na Masonga walitamka maneno hayo, hivyo inawatia hatiani kwa vile walitenda kosa.

Walichosema mawakili

Hakimu Mteite alitoa nafasi kwa Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande aliyesema upande wa Jamhuri unaridhika kwamba washtakiwa wote wawili hawana rekodi yoyote ya kutenda makosa, lakini kwa kuwa wametiwa hatiani aliiomba mahakama kutoa adhabu kali.

“Kwa vile washtakiwa walitoa maneno ya fedheha dhidi ya Rais wa nchi, tunaomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa ili iwe funzo kwa wengine pia,” alisema.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alisimama na kuieleza mahakama iangalie adhabu ya kuwapatia wateja wake akibainisha kuwa wamekaa mahabusu kwa takriban mwezi mmoja, hivyo mahakama ione hiyo ni sehemu ya adhabu japo hawakuwa wafungwa kamili.

Kibatala aliiomba mahakama kuridhia Sugu na Masonga kupewa adhabu ya kifungo cha nje akisema hilo litasaidia mambo mengi ikiwamo suala la uvunjifu wa amani unaoweza kutokea endapo wawili hao watahukumiwa kwenda jela
“Mlengwa katika maneno yale alikuwa ni Rais Magufuli lakini hiyo haiwezi kumuondolea hadhi yake kwa kuwa ana uwezo wa kuyajibu maneno yale popote pale. Pia kwa heshima zote kwa Rais, mwisho wa siku ni mwanasiasa na waliotiwa hatiani kwa kutamka maneno yale ni wanasiasa ‘so it was a political platfrom’ (ilikuwa ni jukwaa la kisiasa) hivyo mahakama yako ijielekeze na iyachukulie hivyo hivyo kama ni maneno ya kisiasa,” alisema.

Kibatala alisema Masonga ni baba wa familia kama ilivyo kwa Sugu, lakini Sugu pia ni mbunge wa wananchi wa Mbeya Mjini, hivyo aliiomba mahakama itoe adhabu kulingana na hoja hizo kwa kuwa katika hilo kuna upande utakaoathirika na si kwa washtakiwa pekee.

Hakimu Mteite baada ya kuwasikiliza mawakili hao alisema, “Nimezingatia hoja za pande zote mbili, hivyo washtakiwa watakwenda jela miezi mitano.”

Mwanzo wa kesi

Kwa mara ya kwanza, Sugu na Masonga walifikishwa mahakamani Januari 16 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande aliyeeleza upelelezi ulikuwa umekamilika na walikuwa tayari kuendelea na usikilizaji. Pande zote zilikamilisha ushahidi Februari 9.

Jamhuri iliwasilisha mashahidi watano na kielelezo kimoja cha sauti iliyodaiwa kurekodiwa na shahidi wa tano, Inspekta Joram Magova.

Upande wa utetezi uliwasilisha mashahidi sita wakiwamo Sugu na Masonga waliokana kutamka maneno wanayoshtakiwa kuyatoa.

Washtakiwa awali walitetewa na mawakili Sabina Yongo, Boniface Mwabukusi na Hekima Mwasipu. Mawakili wengine wa Serikali walioendesha kesi hiyo ni Ofmed Mtenga na Baraka Mgaya.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili Pande uliiomba mahakama kuzuia dhamana kwa washtakiwa akitoa sababu kwamba ni kwa ajili ya usalama wao ombi lililopingwa na Wakili Yongo akisema dhamana ni haki ya kikatiba ya washtakiwa.

Hata hivyo, Hakimu Mteite alikubaliana na hoja ya upande wa mashtaka na kuzuia dhamana, hivyo Sugu na Masonga walikaa mahabusu katika Gereza Kuu la Ruanda jijini Mbeya kwa siku 24 kabla ya kuachiwa kwa dhamana Februari 9, kwa sharti la kusaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.

Kabla ya kuanza kutoa ushahidi Sugu na Masonga wakiongozwa na mawakili wao Mwabukusi, Mwasipu na Yongo walimkataa Hakimu Mteite kuendelea kusikiliza kesi wakidai ana upendeleo hivyo hawana imani naye.

Hakimu Mteite aligoma kujiondoa katika kesi hiyo akisema sababu zilizotolewa na washtakiwa hazina mashiko kisheria kwa kuwa suala la hakimu kujitoa katika kesi lipo kisheria na kwa sababu za msingi.

Aliamuru kesi kuendelea kwa Sugu na Masonga kuanza kutoa ushahidi

Baada ya Hakimu Mteite kugoma kujitoa katika shauri hilo, mawakili wa utetezi Mwabukusi, Mwasipu na Yongo walitangaza kujiondoa kuwawakilisha washtakiwa
Kutokana na mawakili hao kujitoa, Sugu na Masonga waliiomba mahakama kuwapatia muda wa siku 14 ili wajipange kutafuta mawakili wengine. Ombi hilo lilikubaliwa na mahakama.

Februari 8, Sugu na Masonga walianza kutoa ushahidi wakiwa na wakili mpya, Peter Kibatala ambaye pia alimwongoza Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Mbeya, Modestus Chambu kutoa ushahidi.

Rufaa, dhamana zaombwa

Akizungumza baada ya hukumu, Wakili Kibatala alisema hawaridhiki na hukumu iliyotolewa, hivyo wamewasilisha maombi ya kukata rufaa pamoja na kuomba dhamana kwa Sugu na Masonga.

Kibatala alisema kimsingi kulikuwa na kasoro nyingi katika mwenendo mzima wa kesi hiyo na hata namna hukumu ilivyotolewa haikuwa sahihi. “Hatujaridha na uamuzi uliotolewa hivyo tumefuata hatua za kisheria na za kimahakama. Tumekata rufaa, lakini pia tumeleta maombi ya dhamana kwa wateja wetu wote wawili. Tumeiomba mahakama kwa haraka iwezekanavyo itupe nakala ya mwenendo wa kesi husika kwa sababu nakala hiyo ni kitu muhimu katika kukataa rufaa.”

Wakili Kibatala alisema hadi leo wana imani watakuwa wamepata mwanga zaidi wa maombi ya dhamana na mchakato wa rufaa watajua unaendeleaje na itasikilizwa lini, lakini akasema kwa mazingira ya Mbeya yalivyo wanategemea watasikilizwa kwa haraka zaidi.

Kibatala alisema wanazo hoja tisa ambazo wameziwasilisha katika rufaa yao dhidi ya kesi hiyo.

Imeandikwa na Godfrey Kahango, Ipyana Samson na Hawa Mathias



Jinsi saa mbili zilivyotumika kumpeleka Sugu gerezani miezi 5 Jinsi saa mbili zilivyotumika kumpeleka Sugu gerezani miezi 5 Reviewed by KUSAGANEWS on February 26, 2018 Rating: 5

No comments: