Walimu 260 wamefukuzwa kazi mwaka 2016/17
kutokana na makosa mbalimbali ya nidhamu, ikiwamo utoro na kujihusisha na
mapenzi na wanafunzi
Akizungumza katika mkutano wa Tume ya
Utumishi wa Walimu (TCD), katibu wake, Winfrida Rutahindurwa alisema Serikali
haiwezi kuvumilia walimu wanaokiuka sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa
umma.
Rutahindurwa ambaye aliteuliwa kushika nafasi
hiyo mwaka 2016, alisema alikuta mashauri 2,600 ya walimu mezani kwake
yaliyokuwa yakihitaji ufumbuzi, huku asilimia 90 yakihusu utoro
“Utoro upo wa aina nyingi, kuna walimu
wanadhani siku wakiwa hawana kipindi darasani wanaweza kulala nyumbani, wengine
wanadhani wanafunzi wakiwa likizo na walimu wapo likizo, hii si sawa na sheria
lazima ichukue mkondo wake,” alisema.
Katibu huyo alisema utoro mwingine ni baadhi
ya walimu kwenda masomoni bila ruhusa ya wakuu wao wa vituo na wengine
kujiongezea likizo ya masomo
Alisema sheria ya utumishi wa umma ipo wazi,
mtumishi asipoonekana katika kituo chake cha kazi kwa siku tano mfululizo bila
mwajiri wake kuwa na taarifa anapaswa kufukuzwa kazi
“Walimu ni sawa na watumishi wengine wa
kawaida wa Serikali ambao likizo yao ni siku 28 kwa mwaka, hivyo wanapaswa
kutambua kuwa likizo ya wanafunzi haiwahusu,” alisema.
Mapenzi shuleni Mkurugenzi wa Idara ya Ajira na Utumishi wa
TCD, Christina Happe alisema licha ya makosa ya utoro na mapenzi shuleni, kuna
tatizo la walimu kugomea uhamisho
“Uhamisho si uonevu bali ni taratibu za
kawaida za kazi, hivyo mtumishi akihamishwa lazima aripoti kwanza kituo kipya
cha kazi kama ana hoja za msingi za kuzuia uhamisho aziwasilishe,” alisema
Happe.
Naye mwenyekiti wa tume hiyo, Oliver Mhaiki
alisema kazi kubwa ya tume ni kusimamia maadili na nidhamu ya walimu, ikiwamo
kutoa adhabu kwa wanaokwenda kinyume na sheria za utumishi.
Walimu 260 wafukuzwa kazi kutokana na makosa ya kinidhamu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
February 27, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment