Watu wanane wamefariki dunia katika
mazingira tofauti kuanzia Jumatatu hadi juzi wilayani Kiteto mkoani Manyara,
huku chanzo cha vifo hivyo kikiwa bado hakijajulikana.
Wakati wakazi hao wakiripotiwa kufariki dunia, zaidi ya ng’ombe 6,000 wilayani humo wamekufa.
Akizungumza juzi, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto,
Tumaini Magessa alisema mpaka sasa hawajajua chanzo cha vifo hivyo.
Alisema wataalamu wa Wizara ya Mifugo na
Uvuvi na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) wanaendelea na uchunguzi.
Magessa alisema wataalamu hao kwa
kushirikiana na wengine wa Wizara ya Afya wameshachukua sampuli kutoka kwa watu
waliokufa, ng’ombe na uyoga kwa ajili ya kufanya uchunguzi.
“Uchunguzi wa awali haujabaini chanzo cha
vifo vya watu hawa na mifugo. Bado tunaendelea ili kujua sababu kwa kuwa vifo
hivi vimetokea siku tofauti wiki hii,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya alisema, “Watu wamekuwa
wakizungumza mambo mengi kuhusu chanzo cha vifo, ikiwamo kula nyama ya ng’ombe
na wengine wakidai kuwa walikula uyoga.”
Alisema baadhi ya wafugaji wilayani humo
wanadai chanzo cha ng’ombe kufa ni kula majani baada ya mvua kubwa kunyesha na
kusababisha mafuriko. “Majina ya waliofariki dunia bado hatujayapata ila wawili
walifariki katika Kata ya Kiperesa, wanne katika Kijiji cha Emat, Kata ya
Magungu na wengine wawili bado hatujajua walikuwa wakazi wa kijiji kipi.”
Alisema, “Baada ya ukame, mvua kubwa
ilinyesha na majani mapya kuota, sasa wanasema ng’ombe walipokula nyasi hizo
ndipo wakafa ila bado tunafanya uchunguzi.”
Alisema mizoga ya ng’ombe hao imekutwa
maeneo tofauti, mingine ikiwa barabarani na porini.
Mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi wa
eneo hilo kuwa watulivu akisema Serikali inafanya uchunguzi kubaini sababu ya
vifo vya watu hao na mifugo.
Mkazi wa Kata ya Kiperesa, Shabani Khamis
alisema vifo hivyo vimewashangaza kwa kuwa chanzo chake hakijafahamika.
“Hata hatujui tatizo ni nini, pengine
tuiachie Serikali kufanya uchunguzi na kubaini chanzo. Hayo mambo ya uyoga au
kula mboga zenye sumu si ya kuyasema kwa sasa,” alisema.
Watu 4 wafariki dunia wakihofiwa kula chakula chenye sumu Kiteto
Reviewed by KUSAGANEWS
on
January 28, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment