Ujenzi wa reli ya Tanzania Rwanda kuanza Mwezi wa kumi mwaka huu

Serikali ya Tanzania na Rwanda kupitia mawaziri wanaohusika na ujenzi wamesaini makubaliano ya kuanza  ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Isaka hadi Kigali ifikapo Oktoba mwaka huu.

Tukio hilo limewakutanisha mawaziri watatu wa Tanzania ambao ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga pamoja na Waziri wa Ujenzi wa Rwanda, James Musoni huku wakiwa wameongozana na wataalamu mbalimbali wa miundombinu kutoka nchi hizo.

Kabla ya kusaini  makubaliano hayo yaliyofanyika leo Januari 20,2018 ,jijini Dar es salaam, mawaziri wamepokea rasimu ya ujenzi wa reli hiyo na kuijadili kabla ya kupitisha rasmi.

Reli hii ni biashara, lazima tufanye haraka, itasaidia kukuza uchumi nchini, kuongezeka fedha za kigeni, barabara zetu zitadumu, watu wetu watakuza biashara zao, "amesema Waziri Mpango

Kwa mujibu wa mapendekezo ya rasimu hiyo iliyoandaliwa na makatibu wakuu kutoka Rwanda na Tanzania, mradi huo ulioanza mchakato wake miaka mitatu iliyopita, sasa utaanza ujenzi wake rasmi baada ya kuwekwa jiwe la msingi Oktoba mwaka huu na marais wa nchi hizo.

Makubaliano yaliyofanyika leo Jumamosi ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya wakuu wa nchi hizo mbili kupitia ziara ya rais Paul Kagame Januari 12, mwaka huu.

Akiwasilisha rasimu hiyo kabla ya kupitishwa, Mkurugenzi wa Miundombinu kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi  na Mawasiliano, Rogatus Mativila amesema rasimu imependekeza njia mbili za ufanikishaji wa mradi huo wenye urefu wa kilometa 521.

Mativila amesema njia ya kwanza ni kushirikisha sekta binafsi na njia ya pili ni kutumia bajeti za serikali mbili kwa kila nchi kugharamia kipande kilicho katika nchi yake


Kabla ya kusaini, Waziri Mpango amesema Januari 29, viongozi hao wanakutana tena katika vikao vya ndani kwa ajili ya kujadili upatikanaji wa  gharama za mradi.
Ujenzi wa reli ya Tanzania Rwanda kuanza Mwezi wa kumi mwaka huu Ujenzi wa reli ya Tanzania Rwanda kuanza Mwezi wa kumi mwaka huu Reviewed by KUSAGANEWS on January 20, 2018 Rating: 5

No comments: