Mkuu wa Mkoa wa
Manyara, Alexander Mnyeti amewataka wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite
kuiga kampuni ya TanzaniteOne kwa kusaidia miradi ya jamii na kuachana na
mtindo wa kuchuma na kuondoka bila kuchangia chochote.
Mnyeti aliyasema hayo wakati akizindua madarasa matano ya shule ya msingi Songambele Mji mdogo
wa Mirerani, Wilayani Simanjiro, yaliyojengwa na kampuni ya TanzaniteOne.
Alisema wamiliki wengi
wa madini ya Tanzanite huwa wanachimba na wakipata wanakwenda kuwekeza kwenye
mikoa ya jirani ya Arusha na Kilimanjaro.
"Wamiliki wa
migodi mnapaswa kubadilika igeni mfano wa kampuni ya TanzaniteOne ambayo
inasaidia jamii kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo," alisema
Mnyeti.
Alisema jamii ya eneo
hilo ingefurahi kuona faida ya uwepo wa madini hayo kwa wamiliki hao kurudisha
kidogo walichokipata kwa kuchangia maendeleo.
Mwalimu mkuu wa shule
hiyo, Mwanahamisi Musa alisema TanzaniteOne imejenga madarasa hayo baada ya
kubaini baadhi ya wanafunzi wanasoma nje sababu ya mafuriko yaliyotokea Machi
mwaka 2013 na kuharibu vyumba saba.
Mwalimu Musa alisema
mafuriko hayo pia yaliharibu ofisi ya walimu, choo cha wanafunzi na nyumba
mbili za walimu.
"Vyumba saba vya
madarasa vilizuiwa na mhandisi wa wilaya hiyo visitumike kutokana na nyufa
zilizohatarisha usalama wa wanafunzi," alisema mwalimu Musa.
Alisema kutokana na
uharibifu wa mafuriko hayo, shule hiyo ilibakiwa na vyumba vitano pekee ambavyo
walivitumia kufundishia wanafunzi 1,158.
Alisema shule hiyo
iliyoanzishwa mwaka 2002 ina wanafunzi 1,158 wavulana 602 na wasichana 556
hivyo madarasa hayo yatapunguza msongamano.
Alisema wanaishukuru
kampuni ya TanzaniteOne kwa kukamilisha madarasa hayo ila wanawaomba wamalizie
vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu na kisima cha maji kama
walivyoahidi.
Ofisa mahusiano wa
kampuni ya TanzaniteOne, Halfan Hayesh alisema atafikisha salamu za pongezi
zilizotolewa na mkuu huyo wa mkoa kwa viongozi wake.
Hayeshi alisema pia
atafikisha ombi la kutakiwa wamalizie vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya
walimu na kisima cha maji kama walivyoahidi.
RC MNYETI AWATAKA WAMILIKI WA MADINI KUIIGA KAMPUNI YA TANZANITEONE
Reviewed by KUSAGANEWS
on
January 27, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment