Mkazi mmoja wa
Dodoma anayejitangaza kama nabii, Tito Machija amesema watu wasimuone kuwa hana
akili kutokana na mahubiri yake ambayo yanatofautiana kwa kiasi kikubwa na
imani za waumini wa dini nyingine, hasa Wakristo.
Machija, ambaye anajulikana kama ‘Nabii Tito’ anahamasisha
kuoa mke zaidi ya mmoja, ikiwa ni pamoja na kutembea na wafanyakazi wa ndani;
anatumia pombe kunasa waumini na anadai hataki nyimbo za injili kwenye ‘ibada’
zake, ambazo nyingi hufanyikia baa.
Nabii’ huyo anaonekana kwenye mitandao ya kijamii akiwa
amevalia kanzu nyeupe yenye misalaba miwili, chupa ya bia na kitabu kitakatifu
aina ya Biblia.
“Nawashangaa wanaoniona mimi sina akili, niko timamu kabisa
na ninaelewa ninachokifanya,” alisema alipozungumza na MCL Digital.
“Narudia tena kusisitiza kuwa walevi ndio watakaoingia ‘mbinguni’
na mafundisho ninayoyatoa ni sahihi
Tito amekuwa akionekana kwenye mitandao ya kijamii, hususani
kwenye video fupifupi za Instagram, akiwa amevalia mavazi kama ya kichungaji na
kucheza muziki huku akinywa bia na akiwa ameshika biblia.
Nabii’ huyo, mwenye wake watano na watoto 12, amedai kuwa
kwa sasa hitaji lake kubwa ni kumuoa mwigizaji Wema Sepetu ili aungane naye
katika huduma zake.
Wema ni msichana mzuri wa sura na umbo nataka nimuoe awe sehemu
ya kanisa langu na nina imani watu wengi wataongezeka kwenye ibada ili kuja
kumuona yeye na wake zangu hawana tatizo na hilo hata mmoja wao ananisaidia
kumshawishi ili tuungane naye,” alisema Tito.
Tito anakiri kuwa ‘kanisa’ lake halijasajiliwa ila anadai
kwamba anapata ufadhili kutoka kwa walevi mbalimbali.
Tito amedai kuwa ‘kanisa’ lake lipo karibu na Chuo
Kikuu cha Dodoma na mara nyingi ibada zake huwa anazifanya kwenye baa na ana
wafuasi wengi kiasi cha kutojua idadi yao
Amesema kabla ya ibada kufanyika kwenye baa husika, huanza
kwa kupeleka vipeperushi kwa mmiliki ili kuwapa taarifa waumini wake siku hasa
ya ibada kufanyika katika baa hiyo.
“Siku ya ibada ikifika naenda pale nikiwa na bia zangu za
(anaitaja aina ya bia) ambazo nimeshaziombea. Zina ‘upako’. Kila anayetaka
kuingia kwenye ibada analipa kiingilio cha Sh12,500. Ukilipa pesa hiyo unapata
bia zako tano ndiyo huduma inaendelea usipotoa unafukuzwa,” alisema
Tito anajinasibu kuwa ana waumini wengi ambao hujitokeza
kusikiliza mafundisho yake ambayo kwa kiasi kikubwa yanahamasisha ulevi na
mapenzi kwa wasichana wa kazi wa majumbani.
Amesema kwenye huduma zake nyimbo za injili hazina nafasi
kwa kuwa huwaburudisha waumini wake kwa nyimbo za kisasa.
Mtu akishaweza safari zake kichwani ukimuwekea bongofleva
anacheza na kufurahi huku ibada inaendelea,” alisema.
Nabii huyo amedai kuwa hakuna anachokizungumza kutoka
kichwani mwake bali anasimamia mistari ya vitabu vitakatifu.
“Wapo wengi wanaopinga huduma zangu ila nawaambia
sijakurupuka nafanya kitu ambacho kipo na wala sioni kama ninakosea,” alisema.
Kwanini ‘ibada’ kwenye baa
Tito amedai kuwa anaingia makubaliano na wenye baa kwa kuwa
ndiyo sehemu ambayo walevi hukutana na kwake ni mahali sahihi pa kutoa huduma.
Pale nakwenda na bia zangu kadhaa kwa ajili ya waumini
watakaoingia kwenye ‘ibada’. Zikiisha naondoka zangu, nawaacha wanaendelea
kununua za baa hapo ndipo mwenye baa anaponufaika,” alisema.
Watu wengi wamekuwa wakilaumu mafundisho ya Tito kuwa
yanapotosha na wameiomba Serikali kuchukua hatua.
‘ Nabii Tito’: wafadhili wangu ni walevi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
January 22, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment