MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu jijini Nairobi alijitokeza Alhamisi na kukiri
kwamba yeye ni mmoja wa wanaotumiwa na polisi wa trafiki kuwakusanyia pesa
kutoka kwa madereva barabarani.
Mwanamume huyo mwenye
umri wa miaka 33 alifika katika afisi za Taifa Leo katika Nation Centre,
Nairobi na kusema aliitwa na maafisa waliokuwa wakikagua magari katika barabara
ya Haile Sellasie jijini Nairobi na kumpa kazi ya kukusanya pesa kutoka kwa madereva.
“Nilikuwa nikitoka
kazini wakati afisa huyo aliponiita na kuniambia alitaka kuninunulia chai.
Sikujua alivyomaanisha hadi aliponiagiza nimkusanyie pesa kutoka kwa madereva
wa matatu na wa magari ya kibinafsi aliyosimamisha,” alisema mwanamume huyo ambaye
hatuwezi kumtaja jina kwa usalama wake.
Alisema kwa muda wa saa
moja, aliweza kukusanya zaidi ya Sh11,000. “Nimeamua kufichua kisa hiki baada
ya kusoma habari katika gazeti la Taifa Leo kwa sababu ninaamini sio haki.
Inasikitisha kuna watu
wanaounda pesa nyingi bila jasho, huku watu walio na digrii wakipiga lami na
wengine wakifanya kazi ya ulinzi na kulipwa Sh6,000 kwa mwezi,” alisema
mwanamume huyo, ambaye ni mwanafunzi katika chuo kikuu kimoja jijini Nairobi.
Alisema baada ya
kukusanya pesa hizo, afisa huyo alimwelekeza katika hoteli moja kando ya
barabara hiyo walipokutana msalani kumkabidhi hela alizokusanya.
“Alinipa Sh400 alizosema
ni za kununua chai. Aliniambia pesa hizo hazikuwa zake bali za mkubwa wake
aliyekuwa akimsubiri kwenye gari lililoegeshwa hatua chache kutoka nilikokuwa
nikisimama baada ya kushuka kwenye gari kupokea pesa,” alidai mwanamume huyo.
Sio haki
Alisema anafanya kazi ya
ulinzi kupata pesa za karo na kutunza familia yake na sio haki kwa watu kutumia
njia za mkato kujipatia maelfu ya pesa.
Kulingana naye, madereva
walikuwa wakimpatia kati ya Sh100 na 3,000 walivyokuwa wamekubaliana na afisa
huyo ambaye alikuwa ameandamana na wenzake wawili.
“Ni makosa sana kwa mtu
kutumia njia haramu kupata pesa nyingi huku watu wengine wakiteseka na hata
kukosa pesa za chakula. Nikipewa nafasi, ninaweza kusaidia Tume ya Maadili na
Ufisadi (EACC) kuwakamata maafisa hao nikihakikishiwa usalama wangu,” alieleza.
Alisema aligundua
maafisa hao huwa wanawatumia vijana wasio na kazi kuwakusanyia pesa kutoka kwa
madereva, ili kuficha wasikamatwe kwa kula rushwa.
“Polisi hao hubadilisha
watu wa kuwakusanyia pesa na siku hiyo nilijua sikuwa wa kwanza kupatiwa kazi
hiyo,” alieleza.
MWANAFUNZI ASIMULIA ALIVYOTUMIWA NA POLISI KUWACHUKULIA HONGO
Reviewed by KUSAGANEWS
on
January 25, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment